|
Mkutano wa mazungumzo kati ya kundi la nchi nane na viongozi wa nchi zinazoendelea ulifanyika tarehe 8 Juni huko Heiligendamm, kaskazini mwa Ujerumani. Mkutano huo ulijadili hasa masuala kuhusu uchumi wa dunia na mabadiliko ya hali ya hewa. Rais Hu Jintao wa China alihudhuria Mkutano huo na kueleza zaidi maoni na mapendekezo ya China kuhusu masuala hayo.
Kuhusu suala la uchumi wa dunia, Rais Hu Jintao alipotoa hotuba alidhihirisha kuwa, hivi sasa utandawazi wa uchumi unaendelea kwa kina duniani, ambao umeleta fursa nyingi kwa ongezeko la uchumi wa dunia, pia umeleta changamoto mbalimbali, ametoa mapendekezo manne juu ya kuimarisha ushirikiano kwenye sekta ya uchumi wa kimataifa.
Rais Hu alisema, kwanza hali isiyo ya uwiano katika maendeleo ya uchumi wa dunia, na kuongezeka kwa sababu mbalimbali zisizosaidia utulivu wa soko la fedha, yote hayo yameongeza hatari na mgogoro katika mambo ya uchumi wa dunia. Jumuia ya kimataifa inapaswa kubeba wajibu wa pamoja kufanya juhudi za kuhimiza marekebisho yanayofanyika kwa utaratibu ili kudhidibiti hali isiyo ya uwiano katika mambo ya uchumi wa kimataifa; kupinga hatua za kujilinda kibiashara na kuhimiza mazungumzo ya Doha yafikie makubaliano mapema.
Pili, lazima kuimarisha ushirikiano na kuleta manufaa na maendeleo kwa kila upande. Rais Hu alisema, jumuia ya kimataifa inapaswa kuzidisha ushirikiano katika sekta za uchumi na teknolojia, na kusukuma mbele maendeleo ya pamoja; inapaswa kuhimiza utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia, kupunguza pengo kati ya kusini na kaskazini, hasa kukidhi mahitaji maalumu kwa maendeleo ya Afrika; na nchi zilizoendelea zinapaswa kuongeza zaidi misaada kwa nchi zinazoendelea, kupunguza au kusamehe madeni yao, kufungua soko na kuhamisha teknolojia.
Tatu, rais Hu alisema, jumuia ya kimataifa inapaswa kutekeleza maoni ya pamoja yaliyofikiwa kwenye Mkutano wa wakuu wa dunia kuhusu maendeleo endelevu, kuhimiza mambo ya uchumi yapate ongezeko bila kuchafua mazingira, kuendeleza uchumi wa mzunguko, na kujenga jamii ya kubana matumizi ya nishati na kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Nne, rais Hu alisema, jumuia ya kimataifa ingeongeza mashauriano ya kidemokrasia, na kutatua kimwafaka migongano na tofauti. Kwani maendeleo duniani siyo ya aina moja, jumuia ya kimataifa inapaswa kuheshimu haki ya nchi mbalimbali ya kuchagua mifumo ya jamii na njia ya maendeleo, na kuzisaidia zaidi nchi zinazoendelea ziongeze uwezo wao wa kujiendeleza. Mageuzi ya mfumo wa uchumi wa kimataifa yanapaswa kuonesha mabadiliko ya miundo ya uchumi wa dunia, na kuongeza sauti na uwakilishi wa nchi zinazoendelea.
Kuhusu suala la mabadiliko ya hali ya hewa, Rais Hu Jintao alidhihirisha kuwa, mabadiliko ya hali ya hewa ni suala la mazingira, lakini kihalisi ni suala la maendeleo. Lazima kushikilia kanuni kuhusu majukumu ya pamoja na yenye tofauti zilizothibitishwa kwenye "Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa". Kutokana na kanuni hiyo, nchi zilizoendelea zinapaswa kutimiza malengo ya utoaji wa hewa zinazosababisha kuongezeka kwa joto duniani yaliyowekwa kwenye "Makubaliano ya Kyoto" na kutoa misaada kwa nchi zinazoendelea. Rais Hu Jintao alisisitiza kuwa, ili kutimiza malengo ya maendeleo, mahitaji ya nishati ya nchi zinazoendela yataongezeka, hili ni sharti la kwanza kwa maendeleo ya nchi zinazoendelea. Ndiyo maana haifai kuzilazimisha nchi zinazoendelea kupunguza hewa za carbon dioxide katika kipindi cha hivi sasa. Wakati huo huo nchi zinazoendelea zinapaswa kutoa mchango kwa ziwezavyo ili kusukuma mbele maendeleo endelevu ya uchumi wa dunia nzima.
Rais Hu Jintao alisema, ingawa hivi sasa wastani wa utoaji wa carbon dioxide kwa kila mchina bado haujafikia theluthi moja ya ule wa nchi zilizoendelea, lakini serikali ya China inatilia maanani sana mabadiliko ya hali ya hewa na kuchukua sera na hatua mbalimbali za kupunguza utoaji wa hewa carbon dioxide, na China itazitekeleza kwa makini. Alisisitiza kuwa, China ina nia imara ya kushika njia ya maendeleo endelevu, na itaendelea na juhudi za kufanya ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya mabadiliko ya hali ya hewa, na kuimarisha ushirikiano na nchi zinazoendelea.
|