Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-06-11 15:16:31    
Mwongoza michezo ya kuigiza Li Guoxiu

cri

Katika siku za tamasha la "Kukutana Mjini Beijing" mchezo wa kuigiza wa Shamlet ulioongozwa na Bw. Li Guoxiu aliyetoka kisiwani Taiwan ulitimiza maonesho yake mara 100. Mchezo huo umewapatia watazamaji wa Beijing nafasi adimu ya kuufurahia mchezo wa kuigiza kutoka kisiwa cha Taiwan.

Mwaka 1992 kundi la waigizaji la Li Guoxiu lilianza kuonesha mchezo wa kuigiza wa Shamlet katika kisiwa cha Taiwan, hadi sasa watazamaji wa mchezo huo wamezidi laki moja. Mchezo huo umehaririwa kwa mujibu wa mchezo wa tanzia wa kuigiza "the Tragedy of Hamlet" uliotungwa na mwandishi mkubwa William Shakespeare wa Uingereza, unaeleza kuwa kutokana na uhusiano mbaya kati ya waigizaji, wakati waigizaji walipocheza mchezo wa Hamlet walibadilishana mara kwa mara, kwa hiyo walikosea maneno wanayotakiwa kusema jukwaani na kusababisha vichekesho.

Bw. Li Guoxiu alisema anapenda mchezo wa Hamlet, lakini hataki kuonesha moja kwa moja michezo ya nchi za nje bila kuhariri upya. Alisema,

"Nimebadilisha mchezo wa tanzia wa Hamlet kuwa mchezo wa kuchekesha wa Shamlet. Mvuto wa mchezo wa Shamlet unatokana na vituko vingi vya kuchekesha."

Bw. Li Guoxiu alizaliwa mwaka 1955, anajulikana kwa kuwa mwongozaji wa michezo ya kuigiza. Lakini hapo awali alikuwa ni mwigizaji. Alipokuwa na umri wa miaka 18 wakati alipokuwa akisoma katika chuo kikuu alianza kuigiza michezo jukwaani, na aliwahi kuigiza watu 22 katika mchezo mmoja. Hii ni rekodi pekee ambayo hadi sasa hakuna mwigizaji yeyote aliyeivunja kisiwani Taiwan.

Mwaka 1986 alianzisha kundi lake la uigizaji michezo na alianza kuandika na kuongoza michezo yake. Kwa sababu aliwahi kuwa mwigizaji anafahamu namna ya kuchochea hisia za watazamaji. Michezo iliyoigizwa na kundi lake ni ya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na michezo ya dhihaka, michezo ya kufurahisha na michezo ya kuhuzunisha.

Mwaka 1990 kwa mujibu wa tukio ambalo msichana mmoja aliyefanya utalii kisiwani Taiwan aliuawa alitunga mchezo wa kuigiza Shirika la Kuliokoa Taifa, ukieleza mambo mbalimbali ya kijinga yaliyotokea katika upelelezi wa kesi hiyo. Baada ya miaka mitano kupita, Bw. Li Guoxiu alijiwa na wazo jipya kuhusu utungaji wake, alianza kufuatilia watu waliopuuzwa katika jamii na maisha yao. Alisema,

"Niliacha michezo ya dhihaka, kwa sababu naona michezo ya dhihaka haisaidii kuifundisha jamii, nilianza kuzingatia kuonesha watu wema jukwaani. Kisiwani Taiwan kuna askari wengi wazee ambao wanapuuzwa na wanaishi maisha ya kusikitisha. Kutokana na hali yao nimetunga mchezo mmoja wa kuigiza."

Mchezo huo unaeleza kuwa katika jumba la burudani la nyimbo mwimbaji mmoja mwanamke aliwaimbia askari hao wazee wimbo wa kukumbuka nyumbani. Askari hao wazee waliposikiliza wimbo huo walitokwa na machozi, baada ya wimbo kumalizika walipanda jukwaani na kumpa zawadi ya fedha mwimbaji huyo. Mchezo huo wa askari wazee na mwimbaji ulioneshwa mara nyingi kisiwani na watazamaji huwa wanarowa kwa machozi.

Michezo aliyotunga Bw. Li Guoxiu yote inatokana na maisha halisi. Alisema,

"Michezo yangu ya kuigiza inatokana na uchunguzi wa maisha, na kila mchezo una mtindo wake kutokana na mahitaji ya mchezo wenyewe."

Hadi sasa Bw. Li Guoxiu ametunga michezo ya kuigiza zaidi ya 30. Alisema michezo iliyotungwa mwanzoni ilikuwa na dosari lakini baadaye nilirekebisha kwa makini kila michezo hiyo ilipooneshwa. Bw. Li Guoxiu ni mtu asiyeridhika na mafanikio yake, bali anajitahidi kujiendeleza ili kuwaletea watazamaji michezo ya kuvutia zaidi. Alisema,

"Katika miaka 21 iliyopita nimeandika michezo ya kuigiza zaidi ya 30. Baadhi ya marafiki waliniuliza, ni mchezo gani ninaridhika nao? Mimi huwajibu, 'mchezo unaofuata'. Siku zote siridhiki na michezo yangu na siku zote najitahidi kutunga michezo inayoshinda michezo yangu ya zamani."

Bw. Li Guoxiu alisema, atatosheka na maisha yake kama akiweza kutimiza tumaini moja, nalo ni kustawisha kundi lake la waigizaji na kuwavutia watazamaji wengi zaidi. Alisema, kwa kutumia fursa ya tamasha la "Kukutana Mjini Beijing" alionesha mchezo wake Shamlet. Huu ni mwanzo wa ustawi wa kundi lake, na ni fursa nzuri kwake kubadilishana mawazo na waongozaji, waandishi na watazamaji wa michezo ya kuigiza wa China bara.

Idhaa ya kiswahili 2007-06-11