Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-06-11 15:36:21    
Matembezi kwenye msitu wa mianzi wa Shunan mkoani Sichuan

cri

Karibuni wasikilizaji wapendwa katika kipindi hiki cha safari nchini China. Watalii wanaotembelea China, husema: "watu wanaofika kwenye sehemu ya kusini mashariki mwa China wanaangalia bahari, wanaofika sehemu ya kaskazini mashariki wanaangalia misitu, wanaofika kaskazini magharibi wanaangalia mchanga na wanaofika kusini magharibi wanaangalia mianzi".

Sehemu yenye mandhari nzuri ya msitu wa mianzi wa Shunan iko nje ya mji wa Yibing mkoani Sichuan, sehemu hiyo licha ya kuwa na mandhari nzuri ya msitu wa mianzi, pia ina mabaki ya kiutamaduni ya kale. Eneo la sehemu hiyo ni kiasi cha kilomita za mraba 120, milima midogo zaidi ya 500 iliyoko kwenye sehemu hiyo imefunikwa na msitu wa mianzi ya aina ya Nan, wenye eneo la mita za mraba zaidi ya elfu 70, msitu huo mkubwa wa mianzi unaonekana kama ni bahari ya rangi ya kijani, hivyo pia unajulikana kama "bahari ya mianzi". Mfanyakazi wa sehemu hiyo Bw. Lin Wei alisema,

"Mianzi mingi zaidi inayoota kwenye msitu wa mianzi wa Shunan ni mianzi ya aina ya Nan. Kati ya mianzi hiyo kuna mianzi dume na jike, mkulima mwenye uzoefu anaweza kutofautisha mianzi ya jike na dume, kila mwanzi unaweza kuchipua vijitawi kwenye pingili la kwanza, mwanzi unaochipua kijitawi kimoja ni dume, na ule unaochipua vijitawi viwili ni mwanzi wa jike."

Sehemu yenye mandhari nzuri ya msitu wa mianzi wa Shunan ina mianzi ya zaidi ya aina 400, mbali na mianzi inayoota kwa wingi sana, kuna aina za mianzi adimu. Moja yake ni mianzi yenye sura ya binadamu, pingili za mianzi zinakua zikipanuka kwa pembeni, lakini pingili za mianzi yenye sura ya binadamu zinakua kwenda juu kwa kuelekea upande, kila pingili ya mwanzi inafanana na uso wa mtoto, ingawa mianzi hiyo inapindapinda kwenye sehemu ya pingili, lakini kwa jumla inaota kuelekea juu. Watalii wengi waliofika huko kwa mara ya kwanza, hawakujua ile mianzi ni ya aina gani, ila tu kuambiwa na mwongoza watalii.

Katika sehemu ya msitu wa mianzi wa Shunan limejengwa jumba la makumbusho ya mianzi, ambapo watalii wanaweza kuona aina 58 za mianzi adimu. Jumba hilo la makumbusho lilijengwa mwaka 1986, na ni jumba la makumbusho la kwanza kuhusu mianzi peke yake nchini China, jumba la makumbusho lina eneo la mita za mraba 3,800. Sehemu muhimu ya jumba la makumbusho imejengwa kwenye maji, jengo hilo ni lenye mtindo wa jadi wa nyumba za wakazi wa kawaida wa China, lakini jumba la makumbusho limejengwa kuwa na nyumba yenye ghorofa, jukwaa na vibanda, ambavyo vinaunganishwa kwa ujia. Mfanyakazi wa sehemu ya mandhari ya msitu wa mianzi wa Shunan Bw. Lin Wei alisema, ukumbi wa maonesho ya vitu vya sanaa vilivyotengenezwa kwa mianzi, unaonesha vielelezo vya aina mbalimbali za mianzi, silaha za mianzi na ala za muziki za mianzi. Vitu vyote hivyo vya sanaa vilitengenezwa kwa mianzi bora iliyoota kwenye msitu wa Shunan.

"Jumba la makumbusho la msitu wa mianzi wa Shunan ni jumba la kwanza la makumbusho kuhusu mianzi peke yake, kwenye pande mbili za jumba hilo, kuna mianzi adimu ya aina 58. Mianzi ya aina hii ni mianzi ya rangi ya kijani, ambayo ni mianzi midogo kabisa duniani, unene wake ni kati ya milimita 1 na milimita 2. Mianzi ya Nan ni mianzi mikubwa, katika msitu wetu wa mianzi inaonekana mianzi ya aina mbalimbali."

Kutoka lango la jumba la makumbusho, watalii wakitembea kufuata barabara iliyojengwa ndani ya sehemu ya mandhari, watafika kwenye lango la "bahari iliyoko kwenye bahari". Lango hilo lilijengwa kwa kufuata lango la jadi la sehemu ya Sichun ya nchini China, ambalo ni lango kubwa na la mtindo wa kale. "Bahari iliyoko kwenye bahari" ni bonde moja lililoko kwenye msitu wa mianzi wa Shunan, bonde hilo limezungushiwa ukingo uliojengwa na binadamu, na kuwa ziwa moja lenye eneo la kiasi cha mita za mraba 400. Ziwa hilo kubwa linaonekana kama bahari ndogo ndani ya "bahari ya misitu". Mfanyakazi anayeongoza watalii kwenye msitu wa mianzi wa Shunan, Bw. Hu Tonglin alisema, watalii wanaona raha sana wakitembezwa kwenye maji juu ya mianzi iliyofungwa pamoja huku wakiburudishwa kwa mandhari nzuri ya huko.

"Sasa niko kwenye msitu mkubwa wa mianzi unaoonekana kama bahari ya rangi ya kijani, na ziwa hilo ambalo wakazi wa hapa wanaliita bahari, ni bahari ndogo iliyoko kwenye 'bahari ya mianzi' kwa hiyo inajulikana kwa jina la "bahari iliyoko kwenye bahari'. Tukitazama kwenye sehemu ya katikati ya ziwa, tunaona pande zote ni mianzi."

Watalii wanaofika kwenye msitu wa mianzi wa Shunan, hawakosi kushiriki kwenye "karamu ya panda". "karamu ya panda" pia inaitwa kuwa karamu ya mianzi, vitoweo vyote vya karamu hiyo vinapikwa kwa vitu vinavyohusiana na mianzi, aina za vitoweo vyake zinafikia zaidi ya 100. Supu moja ya "karamu ya panda" inapikwa kwa kutumia uyoga wa mianzi, siyo tu inaonekana maridadi, tena ni yenye vitu vingi vya kujenga mwili.

Katika duka moja dogo la mtindo wa kale kwenye kando ya barabara, mwenye duka Bw. Zhang Liangtian aliwashauri watalii waonje aina ya chakula cha huko kinachojulikana kwa jina la Huang Ba, ambacho ni cha aina ya mchele unaonata, kinafungwa ndani ya magamba ya chipukizi za mianzi na kuchemshwa kwa maji.

Bw Zhang :"Ni chakula kitamu chenye harufu nzuri ya mianzi."

Mwongoza safari: "Naomba nijaribu moja, ehen, safi sana! Tena ni tamu kama yenye sukari, chakula hiki kina harufu nzuri, je kimefungwa kwa majani gani?"

Bw Zhang: "Mchele umefungwa ndani ya mabamba ya chipukizi ya mianzi, ni chipukizi ya mianzi ya aina ya Nan."

Kwa kawaida, watalii waliofika kwenye sehemu ya mandhari ya msitu wa mianzi wa Shunan, hupenda kukaa kwa siku kadhaa kwenye hoteli zilizojengwa humo ndani, ili kujiburudisha kwa nyakati nyingi zaidi kwenye msitu wa mianzi wa Shunan.

Wasikilizaji wapendwa, sehemu ya mandhari ya msitu wa mianzi wa Shunan inapendeza sana, hali ya hewa ya huko pia ni nzuri, wastani wa joto kwa mwaka ni nyuzi 15 tu, watalii wanaofika huko katika majira tofauti wanaona msitu wa mianzi wenye umaalumu tofauti. Wasikilizaji wapendwa, kipindi hiki cha safari nchini China kinaishia hapa kwa leo, Tukutane tena wiki ijayo wakati kama huu, asanteni kwa kutusikiliza, kwaherini.

Idhaa ya kiswahili 2007-06-11