Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-06-12 18:42:40    
Barua 0610

cri
Msikilizaji wetu Jim Godfrey Mwanyama wa Mobile Fans Club S.L.P 1097 Wundanyi Taita nchini Kenya, anaanza barua yake kwa kutoa salamu nyingi kwa watayarishaji wa vipindi na watangazaji wote wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, kutoka kwake na marafiki zake, hasa mashabiki wa Radio China kimataifa, ambayo imekuwa ni ya kupendeza sana, huko kwao Kenya,anaendelea kusema kuwa idhaa hii imewafunza, kuwaelimisha, na inawajulisha mengi kutoka duniani.

Bwana Manyama pia anaishukuru sana idhaa ya Kiswahili ya CRI, kwa kudumisha uhusiano naye akiwa ni shabiki wa muda mrefu na ambaye, bado anazidi kuendeleza ushabiki wake, antushukuru kwa kumtumia kalenda maridadi, ambapo kila mtu aliyeiona aliifurahia sana.

Anasema kwa leo hana mengi ila, anawatakia wafanyakazi wote wa CRI kila la kheri kwa mwaka huu wa 2007, ili uwe mwaka wa mafanikio, ili tuendelee na huo moyo wa kuwahudumia wasikilizaji vilivyo.

Msikilizaji wetu Jim Godfrey Mwanyama katika barua yake nyingine anasema anapenda kutoa shukurani za dhati kwa kukubaliwa kuwa mwanachama wa CRI. Anazidi pia kutoa pongezi kwa watangazaji wote wa CRI kwa kazi nzuri wanayoifanya bila ya kuchoka kwa sababu wamejizatiti kuhakikisha kuwa wanawahudumia wasikilizaji na mashabiki inavyostahili. Pia anaipongeza CRI kwa utaratibu wa hali ya juu wa vipindi maana vimepangwa kwa ustadi unaomwezesha msikilizaji kufuatilia vyema na kuelewa mambo.

Zaidi ya hayo yeye kama shabiki wa siku nyingine wa CRI,anasema anafurahishwa na mwakilishi wa CRI ambaye yupo Nairobi nchini Kenya, Bwana Xie, ambaye anawahudumia watu wote bila kujali umri, kabila, uraia, na kimo, na anamuaomba aendelee hivyo hivyo ili CRI iweze kuwa na heshima kubwa duniani

Jambo la tatu anaomba atumiwe kadi za salamu zaidi na bahasha za CRI, ili aweze kuwapa marafiki zake ambao wana ari ya kujiunga na CRI. Pia atumiwe nakala ya kitabu cha vipindi vyetu ili aweze kuvifuatilia vipindi kwa umakini zaidi.

Mwisho anaomba salamu zake ziwafikie wafuatao,Mzee Alfred Awinja, mama Concepta Nakhumicha, Godfrey Oyaro, Thaddeus Mtoro, Brigit Ondeche, Helen Nelima,Kennedy Wechuli, Michel Wechuli,Ben Wechuli, sarah Wanjala, Hesbon Namwacha na mwisho Mama Selina Awinja, Mungu awabariki sana CRI, ndivyo anavyomalizia barua yake.

Tunamshukuru kwa dhati Bwana Jim Godfrey Mwanyama kwa barua yake ya kutuambia kuwa mshabiki huyo wa idhaa ya kiswahii ya Radio China Kimataifa anazidi kuendeleza ushabiki wake, hii inatutia moyo sana, na kueleza maoni yake kuhusu matangazo ya Idhaa ya Kiswahii ya Radio China Kimataifa, ambayo yanatuhimiza tupache kazi zaidi ili kuandaa vipindi vizuri zaidi kwa ajili ya wasikilizaji wetu.

Ni matumaini yetu kuwa mawasiliano na urafiki kati yetu utadumu daima.

Msikilizaji wetu Shadrack Etyangimo wa Cheptais Elite S.L.P 66 Cheptais nchini Kenya ametuletea barua akianza kuwatakia watangazaji wote wa CRI heri na baraka za mwaka huu wa 2007.

Msikilizaji wetu anasema samahani sana kwa kushindwa kushiriki katika chemsha bongo ya mwaka uliopita kutokana na sababu zisizozuilika. Anaendelea kusema kuwa katika eneo alilokuwa anaishi katika wilaya ya mlima Elgon kulitokea mapigano ya kugombea mashamba, ambapo majambazi yalitumia fursa hiyo kuwaua wananchi na hata maofisa usalama waliotumwa kutuliza mapigano hayo.

Na baada ya hapo maofia wa serikali kwa hasira walizochoma moto nyumba zote zilizokuwa karibu na mlima Elgon ambapo watu walipoteza mali nyingi sana, na kwa bahati mbaya nyumba yao ilikuwa miongoni mwa zilizochomwa. Hivyo bahasha na kadi za salamu ziliteketea pamoja na nyumba yao. Hata hivyo anasema ataendelea kuwa pamoja na CRI.

Anamalizia barua yake kwa kuomba kutumiwa kadi za salamu pamoja na bahasha ambazo tayari zimelipiwa.

Tunamshukuru Bwana Shadrack Etyangimo kwa barua yake ya kutuelezea sababu ya kushindwa kwake kushiriki katika chemsha bongo, tunampa pole, ni matumaini yetu kuwa yeye na jamaa zake na marafiki zetu wote watachukua tahadhari katika maisha yao ili kukwepa madhara na hasara. Ingawa tuko mbali, lakini kutokana na maelezo ya wasikilizaji wetu, tunaweza kuelewa hali ya maisha na kazi ya wasikilizaji wetu, kweli tunawafuatilia kila wakati. Hapa tunawatakia wasikilizaji wetu kila la kheri.

Msikilizaji wetu Yakub Said Idambira anatunziwa barua na Kakamega Fans Club, S.L.P 2519 Kakamega nchini Kenya anasema katika barua aliyotutumia kuwa, "Pokeeni salamu nyingi toka kwangu nikitaraji mu wazima kwa uwezo wake mwenyezi Mungu" ndivyo anavyoanza barua yake msilikizaji wetu huyu.

Katika barua yake hii anapenda kutoa shukurani zake na pongezi za dhati kwa watangazaji na wasimamizi wa idhaa ya Kiswahili ya CRI kwa mawasiliano anayopata kwa njia ya radio na barua za kawaida kwa ajili ya kuboresha matangazo na vipindi.

Aidha anashukuru sana kwa kutumiwa gazeti la China Pictorial, gazeti hilo limesheheni mambo mbali mbali ya kiuchumi,kiutamduni, kitalii,huduma, michezo na mambo ya kitaalamu ya China. Anawaomba wachapishaji wafikirie kupunguza bei au wayatoe bure kwani kuna baadhi ya wasomaji hawawezi kumudu gharama zake kutokana na umaskini na kukosa ajira.

Pendekezo lake ni kuwa, uongozi wa Radio China Kimataifa uanzishe utaratibu wa wasikizaji kupiga simu bila ya kulipia gharama, kwa kupitia utaratibu huu ana matumaini kwamba kutachangia matangazo na vipindi vya Radio China Kimataifa kwa njia mwafaka kabisa kwani maswali, mapendekezo, ushauri na maoni kutoka kwa wasikilizaji wengi yatajibiwa kwa urahisi. Ni vigumu kujibu maelfu ya barua zinazowafikia kwa wakati kutokana na shughuli kuwa nyingi. Anawatakia kila la heri na ufanisi katika kazi za kila siku.

Tunamshukuru kwa dhati Bwana Yakub Said Idambira ambaye jina lake hilo linasikika kila mara kwenye matangazo yetu, yeye ametoa maoni kuhusu matangazo yetu, anapendekeza Radio China Kimataifa inaweza kuanzisha utaratibu wa wasikilizaji kupiga simu bila kulipia gharama, hili ni pendekezo zuri, lakini kwa kweli hatujui pendekezo hilo likiwasilishwa kwa ofisi husika ya Radio China Kimataifa, litaweza kukubaliwa mapema au la. Na sisi tulijitahidi sana kuwapigia simu wasikilizaji wetu, lakini hatujui ni kutokana na sababu gani, kila mara ni vigumu kuwapigia simu labda ni kutokana na mawasiliano magumu ya njia ya simu au vipi. Lakini tutajihidi tena ama tutachukua njia nyingine ili kudumisha mawasiliano kati yetu na wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Richard Chenebei Mateka wa S.L.P 65 Kaptateny nchini Kenya anaanza barua kwa kutoa salamu kwa watangazaji na wasikilizaji wote wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa. Anafurahi kwa kupata kalenda ya mwaka 2007 na anaipongeza Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kwa kazi nzuri.

Ombi lake anaiomba CRI ifungue kituo Mlima Elgon cha watalii kitakachoweza kutumika kama makao makuu ya wachina, hoteli na chumba cha kuuzia bidhaa za wachina kama vile vifaa vya umeme, mitambo, na vifaa vya kilimo. Anasema, yeyote ambaye yupo tayari awasiliane naye kwa njia ya barua.

Tunamshukuru Richard Chenebei Mateka kwa barua yake na mashauri yake, ikiwezekana tutawasikilisha mashauri yake kwa idara husika. Ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza matangazo yetu kwa makini na kutoa maoni na mapendekezo yake.