Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-06-13 20:25:11    
Mapigano yamezuka katika ukanda wa Gaza kati ya makundi mawili makubwa nchini Palestina

cri

Tarehe 12 alasiri, chama cha Hamas nchini Palestina kilitoa onyo la mwisho la kutaka jeshi la usalama la Palestina linaloongozwa na chama cha Fatah, liondoke kwenye ukanda wa Gaza, kisha kilianzisha mashambulizi dhidi ya shabaha kadhaa yakiwemo makao makuu ya jeshi la usalama la Palestina yaliyoko sehemu ya kaskazini mwa Gaza. Mwenyekiti wa mamlaka ya taifa la Palestina Bw. Mahmoud Abbas alikilaumu chama cha Hamas kwa kujaribu kuanzisha mapinduzi ya kiserikali katika ukanda wa Gaza.

Mapigano hayo yalikuwa makali toka mwanzoni, ambayo hayakuweza kuzuiliwa na mkataba uliosainiwa tarehe 11 mwezi Juni kuhusu usimamishaji wa mapigano. Toka kuzuka kwa mapambano tarehe 5 mwezi Juni hadi kuzuka mapigano ya pande zote tarehe 12, ingawa muda huo ni mfupi wa wiki moja tu, lakini watu karibu mia moja waliuawa au kujeruhiwa. Katika siku mbili zilizopita, majeshi ya pande hizo mbili yalianzisha kwa nguvu mashambulizi dhidi ya miundo ya serikali na viongozi wa ngazi za juu wa upande mwingine.Misri, ambayo imekuwa ikifanya usuluhishi kati ya makundi hayo mawili, ilisema, Hamas na Fatah hivi sasa zote zimekataa kufanya mazungumzo katika ukanda wa Gaza kuhusu kusimamisha mapigano.

Watu wanaona kuwa chanzo cha kuzuka hali hiyo ni mgongano kati yao kuhusu udhibiti juu ya majeshi ya Palestina. Katika mapambano dhidi ya ukaliaji wa Israel, Hamas iliimarisha nguvu za jeshi lake katika ukanda wa Gaza, wakati Fatah ilikuza athari zake kwenye sehemu ya magharibi mwa ukingo wa mto Jodarn na kudhibiti jeshi la usalama la Palestina kwa kutumia nafasi ya kuongoza katika mamlaka ya kitaifa ya Palestina. Mwaka jana, Hamas ilishinda katika uchaguzi na kujenga "jeshi la utekelezaji", na ilijitahidi kuimarisha hadhi yake halali. Tokea hapo, makundi hayo mawili hayakuacha kuchuana kuhusu uondoaji wa "jeshi la utekelezaji" na udhibiti wa jeshi la usalama la Palestina.

Mapigano ya pande zote yaliyozuka kati ya makundi mawili makubwa ya nchi ya Palestina, bila shaka yataathiri iwe kwa hali ya ndani ya Palestina au kwa hali ya kikanda.

Serikali ya umoja wa kitaifa ya Palestina imekumbwa zaidi na mgogoro huo. Usiku wa manane wa siku hiyo, mwenyekiti Abbas wa mamkala ya kitaifa ya Palestina aliitisha mkutano wa dharura wa kamati kuu ya chama cha Fatah, na kuamua kuwataka mawaziri wote wa Fatah watoke katika serikali ya umoja wa kitaifa, hatua ambayo inahatarisha serikali hiyo ya Palestina.

Pamoja na hayo, baadhi miradi ya misaada iliyoanzishwa kuhusu idara za serikali pia itaathiriwa vibaya. Kwa mfano, mapatano yaliyosainiwa na Umoja wa Ulaya na wizara ya fedha ya Palestina yatakwama baada ya serikali ya sasa kuvunjika, kwani serikali inayopewa msaada haipo tena. Suala la mshahara na suala la misaada ya ubinadamu pia yataathiriwa, hali ya uchumi wa Palestina na msukosuko wa kibinadamu itakuwa mbaya zaidi.

Aidha, mapigano pia yataathiri hali ya ukanda wa Gaza. Habari zinasema, mapigano ya makundi kwenye ukanda wa Gaza yametoa nafasi kwa kundi lenye msimamo mkali wa kisiasa, milipuko ya kigaidi dhidi ya sehemu za umma zikiwemo Internet cafe na maduka ya vinyozi imeongezeka. Watu wana wasiwasi mkubwa kuwa ukanda wa Gaza ukishindwa kudhibitiwa, makundi mengi kama ya Al qaida yatajitokeza na kuharibu utulivu wa sehemu nzima ya mashariki ya kati.

Mbali na hayo, kutokana na kuwa, mgogoro wa nchini Palestina umekwamisha tena na tena mazungumzo kati ya viongozi wa Palestina na Israel, hivyo mapigano yanayozuka safari hii bila shaka yataathiri mazungumzo ya amani ya baadaye pamoja na mazungumzo yatakayofanyika mwishoni mwa mwezi huu kati ya pande nne za mashariki ya kati na viongozi wa Palestina na Israel.

Kuzidi kwa hali ya ndani ya Palestina kuwa mbaya pia kumefuatiliwa na jumuiya ya kimataifa. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alitoa taarifa tarehe 12 mwezi huu ikieleza kuzingatia mapigano kati ya Hamas na Fatah katika ukanda wa Gaza. Taarifa hiyo inatoa wito wa kutaka makundi hayo yasimamishe mapigano mara moja, waunge mkono uongozi wa mwenyekiti Abbas wa mamlaka ya kitaifa ya Palestina na kuirudisha nchi hiyo katika hali ya utulivu.