Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-06-18 15:05:34    
Mtungaji muziki wa opera ya Huangmei Bw. Shi Bailin

cri

Opera ya Huangmei ni opera muhimu katika mkoa wa Anhui, mkoa uliopo katikati ya China. Opera hiyo inaimbwa kwa lahaja ya kimkoa. "Ndoa ya Malaika" ni hadithi ya kusisimua na kuchezwa kwa opera ya Huangmei, ni opera ambayo inajulikana sana kati ya opera zote za Haungmei. Nyimbo katika opera hiyo zilitungwa na mwanamuziki Shi Bailin nusu karne iliyopita. Katika muda wa miaka hamsini hivi, Bw. Shi Bailin pamoja na wasanii wa opera ya Huangmei walifanikiwa kuifanya opera ya Huangmei kutoka opera ya kienyeji kuwa opera muhimu inayopendwa na watu wote wa China.

Siku chache zilizopita, mwandishi wetu wa habari alifika nyumbani kwa Bw. Shi Bailin. Ndani ya nyumba yake ambayo si kubwa zilijaa sahani za santuri. Bw. Shi Bailin alizaliwa mwaka 1927 katika familia ya wakulima, alipenda muziki toka alipokuwa mtoto na aliweza kuimba nyimbo nyingi za kwao. Alisema,

"Nyumbani kwetu kuna aina nyingi za michezo ya sanaa ya opera za kienyeji, nilisikiliza mengi na niliweza kuimba mengi wakati niliposoma katika shule ya msingi. Niliposoma katika shule ya sekondari nilikuwa katika mikoa ya Henan na Shanxi, mikoa ambayo inayujulikana kwa opera za aina nyingine ambazo nazipenda vile vile, kwa hiyo nilipokuwa mwanafunzi wa shule ya msingi na sekondari nililelewa kimuziki, hasa muziki wa opera."

Lakini hapo awali Bw. Shi Bailin hakuwa na nia ya kushughulikia muziki maishani mwake. Alisema,

"Hapo awali sikuwa na nia ya kushughulika na muziki kwa sababu wakati huo watu walioshughulika na michezo ya opera wote walikuwa na maisha magumu, na hawakuheshimiwa katika jamii, nilikuwa na hamu ya kufanya kazi ya tafsiri kwa lugha ya kigeni, nilikwenda kanisani kusoma Kiingereza."

Ingawa Bw. Shi Bailin alipata Kiingereza, lakini hakufanya kazi ya tafsiri. Mwaka 1951 Shi Bailin alijiunga na Chuo Kikuu cha Muziki cha Shanghai kusomea utungaji wa muziki. Alisema,

"Walimu wangu wote waliwahi kusoma katika nchi za nje kwa hiyo muziki nilioelimishwa ulikuwa wa kimagharibi tu uliotungwa na wanamuziki wakubwa kama Bach, Mozart na Beethoven, na ala niliyojifunza pia ni ya kimagharibi, filda. Lakini mwanamuziki mmoja wa China aligeuza maisha yangu, mwanamuziki huyo alikuwa ni He Luding, ambaye alithamini sana muziki wa Kichina, na aliwataka wanafunzi wake wote wajifunze muziki na nyimbo za Kichina."

Shi Bailin alipokuwa katika chuo kikuu hicho aliwahi kutazama opera ya Huangmei, nyimbo za opera hiyo zilimvutia sana.

Miaka ya 60 hivi ya karne iliyopita ilikuwa ni kipindi cha kilele kwa Bw. Shi Bailin kutunga muziki. Katika kipindi hicho alitunga muziki kwa ajili ya opera nyingi za Huangmei, moja kati ya opera hizo ilikuwa ni "Ndoa ya Malaika", wimbo mmoja kati ya nyimbo za opera hiyo unajulikana sana nchini China, wimbo huo unaitwa "ndege kwenye tawi la mti huwa wawili wawili".

Mwanzoni mwa miaka ya 80 ya karne iliyopita, wakati China ilipokuwa mwanzoni mwa mageuzi, Bw. Shi Bailin alikuwa katika kipindi chake cha pili cha ufanisi wa kazi. Katika kipindi hicho aliandika na kuhariri vitabu kumi vikiwemo "Muhtasari wa nadharia ya muziki wa opera ya Huangmei" na "Mkusanyiko wa muziki wa opera mkoani Anhui China", na vile vile alitunga muziki kwa ajili ya filamu nyingi zinazoeleza mambo ya kale ya China.

Mzee Shi Bailin ana umri wa miaka 80, lakini afya yake ni nzuri. Miaka kadhaa iliyopita kwenye makala yake ya "njia yangu ya muziki niliyopitia" aliandika kwamba opera ya Huangmei pamoja na opera za aina nyingine za China zimemlea, na opera ya Huangmei imemsaidia kutimiza ndoto yake ya opera ya kienyeji iwe ya taifa la China.

Idhaa ya kiswahili 2007-06-18