Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-06-18 18:32:13    
Mapambano ya kisiasa kati ya Abbas na kundi la Hamas yapamba moto

cri

Serikali ya dharura ya Palestina tarehe 17 adhuhuri huko Ramallah, magharibi ya Mto Jordan iliapishwa kwa mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Mahmoud Abbas ili kushika madaraka badala ya serikali ya muungano wa kitaifa ya Palestina ambayo imevunjwa na Bwana Abbas usiku wa tarehe 14 Juni.

Vyombo vya habari vimesema, tarehe 16 Juni, Bwana Abbas alitoa amri maalumu ya mwenyekiti ili kutandika njia kwa ajili ya Bwana Salam Fayyad, waziri mkuu wa serikali ya dharura aliyeteuliwa na Abbas kuunda Baraza la mawaziri bila kuzuiliwa na Kamati ya utungaji wa sheria ambayo kundi la Hamas lina viti vingi zaidi kwenye kamati hiyo, ili serikai ya dharura iliyoanzishwa tarehe 17 iweze kufanya usimamizi wa mambo yote kando ya magharibi ya Mto Jordan na ukanda wa Gaza kutokana na sheria ya hali ya hatari na sheria nyingine.

Vyombo vya habari viliona kuwa, baada ya kuanzishwa kwa serikali ya dharura, serikali hiyo iliungwa mkono mara moja na Marekani, Israeli, nchi za Ulaya na nchi nyingi za kiarabu, ambapo nchi kadhaa za kimagharibi na jumuia kadhaa za kimataifa ambazo ziliiwekea vikwazo serikali ya muungano wa kitaifa ya Palestina iliyoongozwa na kundi la Hamas, pia zimeahidi kuiunga mkono serikali mpya ya Palestina. Hii inamaanisha kuwa, hatua husika zitakazotekelezwa na serikali ya dharura ya Palestina si kama tu zitapata misaada ya hali na mali na idara husika, na mazingira ya serikali hiyo yatakuwa mazuri sana kuliko ile iliyoongozwa na kundi la Hamas ambayo mpaka sasa haijatambuliwa na jumuia ya kimataifa.

Bwana Abbas alitangaza kuwa jeshi la kundi la Hamas ni jeshi haramu, hili ni pigo kubwa alilopiga dhidi ya Hamas. Bwana Abbas alipotoa amri ya mwenyekiti alisema, kwa kuwa "kikosi cha utendaji" chini ya kundi la Hamas na jeshi lake la "Izz A Din al Qassam Brigades" lilifanya uasi wa kijeshi na kukiuka sheria na utaratibu wa Palestina, hivyo ameamua kutangaza jeshi hilo kuwa ni jeshi haramu, ambapo watu waliohusika wataadhibiwa kutokana na sheria ya hali ya hatari. Wachambuzi wanaona kuwa, hii kwa kweli ni Abbas kuchukua fursa ya kulaani vitendo vya jeshi la Hamas vya kufanya uasi wa kijeshi, tena anataka kutatua kabisa suala la madaraka ya udhibiti wa jeshi la Palestina, ambalo ni chanzo cha kusababisha migogoro mara kwa mara kati ya makundi mawili ya Hamas na Fatah na kusababisha hali ya mafarakano ya hivi leo.

Habari kutoka Ramallah zimesema kuwa, baada ya kuanzishwa kwa serikali ya dharura, Bwana Abbas atachukua mbinu ya kukataa kufanya mazungumzo na upande wa Hamas. Wakati huo huo atajitahidi kujipatia uungaji mkono wa jumuia ya kimataifa kwa serikali ya dharura, pia atafanya chini juu kuzishawishi nchi husika kuimarisha kazi ya kufunga ukanda wa Gaza na kutia shinikizo, ili kuishurutisha Hamas irudi nyuma katika masuala yanayohusika. Israeli na Misri zimeeleza kuelewa mpango huo wa Abbas. Habari zilisema, mwishoni mwa wiki iliyopita Bwana Abbas alikataa ombi la mazungumzo la Bwana Masha el, kiongozi wa ofisi ya siasa ya kamati ya Hamas. Na msaidizi wa Bwana Abbas alidokeza kuwa, hakuna uwezekano wa kuanzisha mazungumzo kati ya pande hizo mbili, ila tu kundi la Hamas kuvunja "kikosi cha utendaji" kilicho chini ya uongozi wake, na kukiacha kikosi cha usalama cha Palestina kipangiwe upya kwenye sehemu ya Gaza.

Hivi sasa kundi la Hamas linakataa kuitambua serikali ya dharura, likisema serikali hiyo si ya halali, na halitafanya ushirikiano nayo. Aidha, msemaji wa Hamas Bwana Sami Abu Zuhri alisema, Hamas imeota mizizi mioyoni mwa wananchi wa Palestina, harakati za mapambano za Hamas zitaendelea kufanyika.

Wachambuzi wamedhihirisha kuwa, katika mapambano ya kisiasa kati ya makundi makubwa mawili ya Palestina, hivi sasa kundi la Fatah linaloongozwa na Abbas linaonekana kuwa na nguvu zaidi, hasa limepata uungaji mkono na jumuiya ya kimataifa katika hatua yake ya kuanzisha serikali ya dharura. Lakini kuhusu suala la madaraka ya udhibiti wa jeshi, kundi la Hamas haliwezi kurudi nyuma kirahisi kuhusu kuvunja jeshi lake na kuwaadhibu watu waliohusika, kwani kundi hilo limeonesha hadhi yake ya kimkakati huko Gaza muda si mrefu uliopita. Hivyo katika siku zijazo mapambano makali zaidi yataonekana pia katika suala hilo.