Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-06-19 15:22:42    
Barua 0617

cri

Msikilizaji wetu Ali Hamisi Kimani ametuletea barua akisema kuwa, salamu nyingi zitufikie kutoka kwake yeye na marafiki zake, hawajambo huku wakiwa na matumaini kuwa nasi pia tu wazima kama kigongo, na tunaendelea kuchapa kazi vizuri.

Anasema madhumuni yake hasa ya waraka huu kwanza ni kutujulisha kuwa amekuwa akipokea barua zetu, lakini kwa kupitia anwani yake ya zamani, sasa angependa tutumie anwani yake mpya. Pili ni kutaka kutujulisha kuwa vyote tulivyomtumia hivi karibuni, vikiwemo bahasha zilizolipiwa, kadi za salamu, picha za ndege pamoja na wadudu wanaopatikana nchini China na jarida la china pictorial amevipata.

Ama kweli yeye hana budi ila kutunyooshea mkono wa tahania. Anasema tumemdhihirishia dhahiri shahiri kuwa kutokako wema hurudi wema, kwani hii ndio radio pekee inayoridhika na juhudi za wasikilizaji wake na hatimaye kuwaridhisha. Endeleeni vivyo hivyo na Mungu atatupa jaza yetu. Nao wasikilizaji wataendelea kutegea sikia idhaa hii kila kukicha.

Bwana Ali Hamisi Kimani anasema katika barua yake nyingine kuwa mbali na kutupongeza kwa juhudi zetu za kuwahakikishia usikilizaji mzuri wa vipindi vyetu, angependa kutoa maoni kama yafuatayo:

1. Ingekuwa jambo bora kuwatumia wasikilizaji majibu sahihi ya maswali ya chemsha bongo mara tu baada ya kutangaza washindi. Hili litawawezesha kujua wapi walikosea.

2. Ikiwezekana, kuanzishwa mpango wa kuwatumia mashabiki na wakereketwa wa idhaa hii picha za watangazaji ambao wanawasikia tu sauti zao.

3. Amewahi kuomba kuwa ikiwezekana tumsaidie kupata nafasi ya kufundisha lugha ya Kiswahili nchini China hususan kwa wale wanaoienzi lugha hii.

4. Anashukuru sana kwa kupata nafasi ya tatu katika chemsha bongo iliyopita. Lakini anatamani sana kuja China ili kujionea mandhari mbalimbali ya nchi ya China ambayo huwa tunasimulia katika kipindi cha Safari nchini China, hivyo ni matumaini yake kuwa safari hii ataweza kupata nafasi maalumu katika chemsha bongo ambayo matokeo yake wanayasubiri kwa hamu na ghamu.

Tunamshukuru kwa dhati Bwana Ali Hamisi Kimani kwa barua yake na maoni na mapendekezo yake kwa vipindi vyetu hasa kuhusu chemsha bongo, kama wasikilizaji wengine walivyotoa. Tutafanya juhudi kwa tuwezavyo ili kuwafurahisha wasikilizaji wetu. Lakini kwa kweli hivi sasa kazi za idhaa yetu zimeongezwa kwa kiasi kikubwa, kila siku tunachapa kazi kujitahidi kukamilisha kazi zinazowekwa. Kama bado kuna madosari kwenye kazi tulizofanya tunaomba radhi kwa wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Mwalimu Wabwire Anthony Namude wa sanduku la posta 50409 Nambale Kenya ametuletea barua akisema kuwa, anazidi kuvutiwa na matangazo na vipindi vya Radio China Kimataifa. Matangazo yanachambuliwa vyema na kwa kina inayostahili jambo ambalo linamtosheleza msikilizaji kimawasiliano. Masuala kuhusu bara la Afrika hushughulikiwa vyema hii ni ishara kuwa bara la Afrika liko mawazoni mwa wachina na pia wanawathamini wazalendo wake kwa hali na mali. Utafiti huwa wa kina na maelezo hutoa picha halisi na bora masikioni mwa msikilizaji.

Na masimulizi kuhusu nchi ya China haswa tamaduni za kale huwa mwafaka, maelezo huwa yamepangwa vyema na kwa mtiririko unaomwelekeza msikilizaji kufuatilia masimulizi kuanzia mwanzo hadi mwisho. Anatushukuru kwa kazi nzuri, anasema endeleeni kuwaletea wasikilizaji habari motomoto kuhusu nchi ya China na ulimwengu kwa jumla.

Tunamshukuru Mwalimu Wabwire Anthony Namude kwa barua yake na maoni yake kwa matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, ambayo yametutia moyo na kutuhimiza kuchapa kazi zaidi kwa ajili ya wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Damas M. Bundala C/o Fabian Amasi P. O. Box 46116 Dar es Salaam Tanzania ametuletea barua akisema kuwa Salamu nyingi zitufikie sisi sote hapa Beijing, China. Matumaini yake sisi sote ni wazima wa Afya na Mungu anaendelea kutubariki. Yeye ni mzima, anamshukuru Mungu, na anaendelea na masomo yake vizuri.

Anashukuru sana, kwa Certificate pamoja na zawadi ambayo tulimtumia kwa kushika nafasi ya pili katika shindano la chemsha bongo kuhusu "miaka 65 ya Radio China Kimataifa", mwaka 2006. alivipata vyote viwili, yaani cheti na zawadi kwa usalama na alivifurahia sana, kwani ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuweza kupata zawadi kama hiyo. Alishiriki mashindano mengine nyuma lakini hakuweza kufanikiwa hivyo, ndiyo maana alifurahi sana alipopata zawadi hiyo.

Anasema samahani, kwa kuchukua muda mrefu kidogo kuweza kutujibu. Hakuweza kufanya hivyo mapema kutokana na sababu za hapa na pale, ambazo hazikuweza kuzuilika. Alipenda sana kushiriki shindano la chemsha bongo la vitutio vya "Mkoa wa Sichuan, Maskani ya Panda", lakini amechelewa kujibu shindano hilo. Hata hivyo, anategemea kujibu chemsha bongo zijazo na kufanya vizuri zaidi hata kushika nafasi ya kwanza. Anatutakia sote kazi njema na Mungu atubariki, tuendelee kuiboresha Radio China Kimataifa.

Tunamshukuru sana Damas M. Bundala kwa barua yake, ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza vizuri matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa pamoja na kushiriki kwenye chemsha bongo, kutoa maoni na mapendekezo, na kudumisha mawasiliano na urafiki kati yetu.

Dominic Nduku Misholo S.L.P 397 Kakamega (P.C. 50100) Kenya ametuletea barua akisema kuwa, salamu zake zitufikie hapa Beijing China kutoka hapo Kakamega, Kenya. Akitarajia ni wazima kwa uwezo wake mwenyezi mungu.

Anatupongeza kwa kazi nzuri tunayoifanya hapo studio na pia kuiboresha Radio China Kimataifa na kuwa maarufu zaidi miongoni mwa Radio nyingine za kimataifa. Kwa miaka ya hivi karibuni iliyopita, Radio China Kimataifa imepata mafanikio makubwa hasa Kenya, na hata nchi nyingine ambazo zina uhusiano wa kimaendeleo na China zote zinufaika kimaendeleo.

Anasema hao wasikilizaji wa Radio China Kimataifa wanazidi kupata wasikilizaji wapya wenzao wanaotaka kuandika barua na hata kutuma salamu kwa jamaa na marafiki katika sehemu mbalimbali duniani.

Hii inatokana na jinsi wanavyoona wakihudumiwa na Radio China Kimataifa kwa wakati. Pia anatoa maoni kwa idara husika kuongeza vituo zaidi vya kujifunza lugha ya Kichina kwa mikoa yote nane ya nchi ya Kenya, hivyo itawawezesha vijana wao kupata ajira, na pia kuwaunganisha na kuitambua Radio China Kimataifa kama Radio pekee ya kimataifa duniani. Anaishia hapa kwa kututakia heri njema na afya bora na kueleza matumaini yake kuwa vipindi vya Radio China Kimataifa vyote vitakuwa vizuri.

Tunamshukuru sana Nduku Misholo kwa barua yake. Kuhusu maoni yake ya kujifunza Kichina, hapa tunapenda kumwambia kuwa, Darasa la matangazo la Confucius lilizinduliwa rasmi asubuhi ya tarehe 8 Juni huko Nairobi Kenya. Darasa hilo ni mradi wa huduma za mafunzo ya lugha ya Kichina zisizotafuta faida, mafunzo hayo yatatolewa kwenye matangazo ya Kiingereza na Kiswahili ya 91.9 FM ya Radio China Kimataifa ili kukidhi mahitaji ya watu wa sekta mbalilbmali wa Nairobi Kenya, na kuongeza mawasiliano na ushirikiano kati ya China na Kenya pamoja na mashirika mbalimbali ya kimataifa. Kama ikiwezekana, wasikilizaji wetu watapata fursa mpya ya kujifunza Kichina, tukishamaliza maandalizi, matangazo ya vipindi vya kujifunza Kichina kwenye darasa hilo, tutatangaza pia kwenye matangazo yetu yanayotolewa kila siku kwa kupitia radio KBC.

Msikilizaji wetu Jackline Andeyo Savala wa S.L.P.64 Mautuma?Kenya Anaanza na salamu nyingi kwa wafanyakazi wa RADIO China Kimataifa na pia anatoa pongezi kwa watayarisha wa kipindi cha Salamu zenu kwani anasema kinatia fora sana na kwa vile muda umeongezwa wa wasikilizaji kusalimiana anashukuru sana.Pia anatoa pongezi kwa washindi wote waliofanikiwa kushinda na kuja nchini China Anasema anaendelea kuwa msikilizaji wetu na tumtumie kadi za salamu ili aweze kuwasalimia na wengine ili kipindi kiendelee kuwa kizuri na cha kudumu.Anatumai na yeye siku moja kuwa mshindi na kufika nchini China kutembea.Mwisho anasema ni hayo tu machache kwa leo. Anatutakia kila la kheri katika kazi zetu za kila siku.

Idhaa ya kiswahili 2007-06-19