Mwenyekiti wa Mamlaka ya utawala wa Palestina Bwana Mahmoud Abbas tarehe 18 aliongea kwa njia ya simu na rais Bush wa Marekani akidai kurudisha mara moja mazungumzo ya amani ya mashariki ya kati. Na waziri mkuu wa Israel Bwana Ehud Olmert ambaye yuko ziarani nchini Marekani tarehe 17 alisema, Israel inapenda kufanya mawasiliano na serikali ya Palestina iliyoanzishwa hivi karibuni. Wachambuzi wanaona kuwa, viongozi wa pande hizo mbili wana haraka ya kuanzisha mazungumzo ya amani katika hali ya hivi sasa.
Israel inaona kuwa, serikali ya dharura ya Palestina iliyoanzishwa hivi karibuni ni serikali yenye msimamo wa katikati ambayo imeachana na kundi la Hamas lenye msimamo wa siasa kali, kimsingi inaweza kukubali kanuni tatu za mazungumzo ya amani zilizotolewa na pande 4 zinazohusika na masuala ya mashariki ya kati yaani kuitambua Israeli, kuacha nguvu za kimabavu na kukubali makubaliano ya amani yaliyofikiwa zamani kati ya Palestina na Israel. Hata hivyo, serikali hiyo mpya ya Palestina itakuwa nguvu kubwa ya kuzuia kundi la Hamas baada ya mgogoro wa Gaza kutokea. Bwana Ehud Olmert anaona kuwa, hali ya hivi sasa inayosaidia mazungumzo ya amani haikutokea katika miaka kadhaa ya hivi karibuni, hivyo ni lazima kushika fursa hii.
Kwa upande wa Palestina, kuanzishwa kwa serikali ya dharura kumethibitisha tena hadhi na heshima ya Bwana Abbas na kundi la Fatah linaloongozwa naye kote nchini Palestina. Waziri wa habari wa serikali ya dharura Bwana Riyad al Malki tarehe 18 alisema kwenye Mkutano wa kwanza wa Baraza la mawaziri kuwa, bila kujali mabadiliko gani yatatokea katika hali ya Gaza, mamlaka ya serikali mpya itaonekana kote Palestina ikiwemo Gaza. Hii imetangaza kuwa mamlaka ya Hamas kwenye sehemu ya Gaza si ya halali, na pia imethibitisha tena hadhi ya Bwana Abbas ambaye atawakilisha wananchi wote wa Palestina wakiwemo watu wa kando ya magharibi ya Mto Jordan na ukanda wa Gaza kufanya mazungumzo na Israel, ambapo hatazuiliwa tena na Hamas, na masuala kadha wa kadha kama vile kusimamisha vita kando ya magharibi ya Mto Jordan yataweza kutatuliwa kirahisi zaidi ?
Lakini wachambuzi wamedhihirisha pia kuwa, hivi sasa bado kuna matatizo kadhaa kwa kurudisha kihalisi mazungumzo ya amani kati ya Palestina na Israel. Chini ya hali ambayo sehemu ya Gaza bado inadhibitiwa na kundi la Hamas, hivyo mazungumzo kuhusu mipaka ya mwisho, hadhi ya Jerusalem na kuwarudisha wakimbizi hayataweza kufanikiwa.
Aidha, ingawa serikali ya dharura ya Palestina imeahidi kuendelea kufanya usimamizi kwenye sehemu ya Gaza, lakini jinsi ya kutekeleza sera yake kwenye sehemu ya Gaza inayodhibitiwa na kundi la Hamas bado haijajulikana, na hali kadhalika kwa utekelezaji wa makubaliano na maelewano yaliyofikiwa kati ya Palestina na Israeli kote nchini Palestina.
Watu wa Ramallah walidokeza kuwa, serikali ya dharura ilianzishwa hivi karibuni tu, hivi sasa hali ya kando ya magharibi ya Mto Jordan bado haijawa ya utulivu, na jeshi la Hamas bado linajipenyeza zaidi kando ya magharibi ya Mto Jordan na kujaribu kuidhibiti, hivyo kazi kuu ya serikali mpya ya Palestina bado ni kudhoofisha nguvu ya Hamas, na kujitahidi kutuliza hali ya mambo haraka iwezekanavyo. Tarehe 18 waziri mkuu wa serikali ya dharura ya Palestina ambaye pia ni waziri wa fedha Bwana Salam Fayyad alifunga akaunti ya fedha ya serikali ya Hamas, na Bwana Abbas alivunja Kamati ya usalama wa taifa ambayo kiongozi wa Hamas Bwana Hania alikuwa mjumbe wa kamati hiyo. Hatua hizo si kama tu zimechukuliwa kwa ajili ya kuimarisha hadhi ya serikali ya dharura, bali pia ni kwa kuonesha nia ya dhati ya kuafanya mazungumzo ya amani na Israeli.
Hivi sasa Upande wa Israel umeahidi kulegeza masharti kando ya magharibi ya Mto Jordan inayodhibitiwa na serikali ya dharura ya Palestina, ili kutimiza maendeleo makubwa ya uchumi na jamii kwenye sehemu hiyo, na kuweka mfano wa kuigwa kwa sehemu ya Gaza, ikiwa ni kuliwekea shinikizo kundi la Hamas. Waziri mkuu wa Israel Bwana Ehud Olmert alisema, kwa hatua ya kwanza Israel itaanza kurudisha mawasiliano na Bwana Abbas kila baada ya muda fulani ili kutatua masuala ya kawaida, halafu kuelekea utatuzi wa masuala makubwa.
Palestina na Israel zote zinataka kushika fursa ya hivi sasa kurudisha mazungumzo ya amani.
|