Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-06-21 15:23:54    
Jumba la sinema kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa macho

cri

Jumba la sinema ni mahala zinapooneshwa filamu. Je, watu wenye ulemavu wa macho wanaweza kupata burudani kwenye jumba la sinema? Jibu ni ndiyo. Hapa mjini Beijing, kuna jumba la sinema linalowahudumia watu wenye ulemavu wa macho. Hivi karibuni mwandishi wetu wa habari alitembelea jumba hilo la sinema.

Katika jumba hilo kuna chumba chenye eneo lisilozidi mita 30 za mraba. Tofauti na majumba ya kawaida, hakuna kioo, isipokuwa televisheni moja, mtambo wa kuonesha DVD na kipaza sauti. Wageni wa jumba hilo wote ni watu wenye ulemavu wa macho ambao wanasikiliza filamu, ambapo watu wa kujitolea wanatoa masimulizi ya hadithi na picha za filamu.

Jumba hilo dogo la sinema linawaletea furaha watu wengi wenye ulemavu wa macho. Mama Li Guizhi mwenye umri wa miaka 48 anatembelea jumba hilo la sinema mara kwa mara. Mwaka 2001 jicho lake moja lilipoteza uwezo wa kuona, na jicho jingine linakaribia kupofuka kabisa.

Alisema "Siwezi kutazama televisheni hata nikivaa miwani. Nyumbani kwangu mtoto anasoma shule, na mume anakwenda kazini, kwa hiyo hakuna mtu anayeweza kunielezea vipindi vinavyooneshwa kwenye televisheni. Masimulizi ya filamu ya hapa yananivutia sana."

Mzee Hou Jianguo mwenye umri wa miaka 68 vile vile ni mgeni wa jumba hilo la sinema. Ingawa inamchukua saa zaidi ya 2 kwenda jumba hilo la sinema kutoka nyumbani kwake, mzee huyo anafurahia.Alisema "Picha zote za filamu zinasimuliwa, hali ambayo ni sawa na kusikiliza hadithi. Navutiwa sana."

Watu wenye ulemavu wa macho wanapata burudani bila malipo kwenye jumba hilo la sinema. Tangu mwezi Julai mwaka 2005 jumba hilo maalumu la sinema lianzishwe hadi hivi sasa, watu zaidi ya 200 wenye ulemavu wa macho wameburudishwa na filamu 40 kwenye jumba hilo. Filamu hizo ni pamoja na filamu za Kichina na za nchi za nje.

Mwanzilishi wa jumba hilo la sinema ni bwana Dawei mwenye umri wa miaka 48. Yeye pia ni mmojawapo kati ya watu wanaojitolea kusimulia filamu kwa ajili ya walemavu wa macho.  Alisema "Nafurahia kusimulia filamu. Ninawaeleza dunia hii inaonekana namna gani, kwa hiyo wanaweza kuhisi hali halisi ya dunia wanayoishi."

Pamoja na kuanzisha jumba hilo maalumu la sinema, Bw. Dawei pia alianzisha shirika moja lisilo la kibiashara la kutoa elimu kwa watu wenye ulemavu wa macho.

Mara kwa mara Bw. Dawei anatembea huku akiwa amezibwa macho akisaidiwa na mke wake, ili aweze kuhisi kama watu wenye ulemavu wa macho wanavyohisi. Kwa hiyo anaweza kusimulia vizuri filamu.

Alisema "Ninapotembea barabarani wakati macho yangu yamezibwa, nimehisi sehemu zisizo na uhakika moyoni mwangu, nikawa maswali mengi. Hivyo ndivyo marafiki wenye ulemavu wa macho wanavyohisi. Wanapoburudishwa na filamu wanaweza kufahamishwa mambo mengi na kupata hisia za uhakika."

Hivi sasa watu wengi wamejiunga na shughuli za sinema hiyo za kuwahudumia watu wenye ulemavu wa macho kutokana na mfano mzuri aliotoa Bw. Dawei. Wakili Wen Qiufang ni mmoja kati ya watu hao wa kujitolea. Alikumbuka kuwa siku moja katika wiki ya pili tangu aanze kutoa huduma kwenye jumba hilo la sinema, ambapo ilianguka theluji kubwa kabisa katika mwaka 2006 hapa Beijing.

Alisema "Siku hiyo ilianguka theluji kubwa. Hata hivyo wageni zaidi ya 10 walikuwa wamefika, wakisema wamesafiri kwa saa mbili hadi tatu na njiani walibadilisha mabasi kwa mara mbili na tatu. Wakati huo huo niliona wajibu mkubwa ninaobeba kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa macho, sina sababu yoyote ya kutofanya kila niwezalo kuwasimulia filamu."

Karibu wafanyakazi wote wa jumba hilo la sinema ni watu wa kujitolea. Kijana Shen Quan ni mhitimu wa chuo kikuu, amekuwa akijitolea kuwahudumia walemavu bila malipo kwenye jumba hilo kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja. Maneno yake yanakubalika na wafanyakazi wengi wa sinema hiyo, akisema "Ukiwasiliana mara kwa mara na walemavu, unaona wanatuhitaji sana tuwahudumie. Kutokana na hali hiyo, tunajikuta kuwa tunayofanya sasa ni kazi yenye maana na thamani kubwa."

Kutokana na upendo wao mkubwa, watu wa kujitolea wanawaelezea watu wenye ulemavu wa macho dunia yenye rangi mbalimbali. Na wakitumia sauti zao, wanawafanya walemavu hao waweze kutazama filamu.

Hivi sasa jumba hilo la sinema linalowahudumia watu wenye ulemavu wa macho inajulikana hapa mjini Beijing. Jumba hilo linatoa huduma bila kutoza malipo, kwa hiyo mwanzilishi wake Bw. Dawei hajapata faida yoyote. Alisema hazingatii faida, bali anataka kufanya mambo halisi ya kuwasaidia watu wanaohitaji misaada. Hivi sasa ana mpango wa kurekodi masimulizi ya filamu kwenye CD ili watu wenye ulemavu wa macho wanaoishi pembezoni pia waweze kupata burudani kutokana na filamu mbalimbali.

Idhaa ya kiswahili 2007-06-21