|
Mkutano wa 16 wa Asia ya mashariki wa baraza la uchumi, unaofanyika kwa siku mbili ulifunguliwa tarehe 24 mjini Singapore. Kauli-mbiu ya mkutano huo ni "kuimarisha uwezo wa kuongoza, na kuanzisha karne ya Asia".
Maofisa wa serikali pamoja na wawakilishi zaidi ya 300 wa sekta za siasa, biashara na wasomi kutoka nchi 26, wanashiriki kwenye mkutano huo. Maofisa hao watajadili mchakato wa Asia kuwa ncha moja muhimu duniani, mwelekeo wa maendeleo ya Asia katika siku za baadaye, pamoja na jinsi Asia itakavyofanya kazi ya kuongoza katika mchakato wa utandawazi duniani. Rais Gloria Arroyo wa Philippines alipozungumzia mstakabali wa Asia katika hotuba aliyotoa wakati wa ufunguzi wa mkutano, alisema,
"Nina imani kubwa kuhusu Asia, pia nina imani kuhusu mafanikio ya Asia katika miaka 20 ijayo. Enzi yetu imewadia, Asia na watu wake watafanya kazi muhimu ya kuongoza katika shughuli za kiuchumi na kisiasa duniani."
Hivi sasa Asia ni sehemu yenye maendeleo ya kasi zaidi ya uchumi duniani, licha ya hayo hatua za utandawazi wa eneo hilo pia zinaharakishwa. Katika miaka ya hivi karibuni mikataba mingi ya biashara huria ya pande mbili, na ya kikanda ilisainiwa. Takwimu zinaonesha kuwa, kwenye sehemu ya Asia ya mashariki, mikataba ya biashara huria iliyosainiwa, inayofanyiwa mazungumzo hivi sasa, pamoja na ile inayochunguzwa imefikia 109. Kuhusu hali hiyo, waziri wa biashara wa Indonesia Bibi Mari Elka Pangestu alisema,
"Asia ya mashariki inaongoza katika shughuli za biashara na utandawazi duniani, na inahimiza maendeleo ya Asia. Suala lililopo hivi sasa ni jinsi Asia inavyoendelea kufanya kazi ya kuongoza. Ninaona sehemu ya Asia ya mashariki inatakiwa kufanya kazi ya kuongoza, inatakiwa kusawazisha mikataba mingi ya biashara huria ya kikanda na ya pande mbili. Siyo serikali tu, sekta ya biashara pia inatakiwa kushiriki."
Hivi sasa nchi za Asia pia zinakabiliwa na changamoto nyingi katika ujenzi wa miji, pamoja na kuharakishwa kwa ujenzi wa miji katika nchi mbalimbali, idadi kubwa ya wakazi wa sehemu ya vijiji wanahamia mijini, serikali za nchi mbalimbali zinakabiliwa na matatizo ya maendeleo ya miji yakiwemo ya mawasiliano na usafirishaji, mpango wa mji, mtindo wa maendeleo ya miaka mingi iliyopita na ujenzi wa miundo-mbinu. Ongezeko la mfululizo la idadi ya watu barani Asia linazidisha matatizo ya maendeleo ya miji. Kuhusu suala hilo waziri wa mambo ya nje wa Singapore Bw. George Yeo Yong Boon alisema,
"maendeleo ya ujenzi wa miji kwenye Asia ni jimbo lisiloonekana mara kwa mara katika historia ya dunia, migongano inazidi kadiri tofauti inavyopanuka kati ya mapato ya watu, ambayo baadhi yake ni migongano ya kisiasa na kiuchumi, lakini pia kuna migongano mingine ya kijamii, kidini na kikabila. Utatuzi wa matatizo hayo unategemea uongozi na usimamizi wa ujenzi wa miji."
Washiriki pia walitoa maoni yao kwenye mkutano kuhusu jinsi Asia inavyofanya kazi muhimu katika dunia. Ofisa mkuu mtendaji wa kampuni mbili za magari za Nissan ya Japan na Renault ya Ufaransa Bw. Carlos Ghosn alisema,
"Baadhi ya masuala tunayotarajia nchi za Asia kuyafikiria ni pamoja na jinsi Asia itakavyochukua nafasi ya kuongoza katika karne ya 21, na kubuni ajenda na mpango kamili. Siyo tu kulenga matatizo yanayoikabili sehemu ya Asia tu, bali pia kushughulikia masuala yanayofuatiliwa na nchi mbalimbali. Kwa mfano, kuongezeka kwa joto duniani, uwiano wa kiuchumi, uwekezaji, usafirishaji bidhaa kwa nchi za nje na kuhimiza ununuzi wa nchini ili kuifanya Asia isiwe sehemu muhimu katika uzalishaji tu, bali pia ni mnunuzi muhimu.
|