Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-06-26 14:42:31    
Viwanda vya magari vyenye hakimiliki ya ubunifu vya mkoa wa Anhui vyaendelea kwa kasi

cri

Walikuwepo wataalam wa kiuchumi waliosema kuwa viwanda vya magari ni "uti wa mgongo wa viwanda", kwa maana fulani viwanda vya magari vinaonesha kiwango cha viwanda vya nchi. Katika miaka ya hivi karibuni, China pia inafanya juhudi kuendeleza viwanda vya magari, hasa kutilia maanani kuendeleza viwanda vya utengenezaji magari yenye hakimiliki ya ubunifu, na mkoa wa Anhui ulioko katikati ya China unaongoza katika sekta hiyo. Kampuni ya magari ya Jianghuai inayouza malori kwa wingi kabisa nchi za nje, na kampuni ya magari ya Chery inayouza magari kwa wingi kabisa nchi za nje zilianzishwa mkoani Anhui, China.

Kampuni ya magari ya Jianghuai ilianzishwa mwaka 1999, ambayo inatengeneza magari ya mizigo na magari ya biashara. Kila mwaka inaweza kutengeneza magari zaidi ya laki 2. Tangu ianzishwe kampuni hiyo, inafanya juhudi kutengeneza magari yenye hakimiliki yake ya ubunifu. Hivi sasa magari ya kampuni hiyo licha ya kuuzwa nchini China, vilevile yanauzwa katika nchi za kusini mashariki ya Asia, Amerika ya kusini na Afrika. Wakati huohuo, kampuni ya magari ya Jianghuai imeanzisha kituo cha utafiti na uendelezaji nje ya nchi, na kuajira watu wenye ujuzi wa huko kufanya usanifu wa magari. Ofisa mhusika wa kampuni hiyo Bw. Wang Dongsheng alidokeza kuwa, gari dogo litakalotengenezwa katika nusu ya pili ya mwaka huu na kampuni hiyo linasanifiwa na kituo chake cha utafiti na uendelezaji cha nje. Alisema:

"Tumeanzisha vituo vya utafiti na uendelezaji katika nchi mbalimbali, na kupitia vituo hivyo tutaweza kupata teknolojia ya kisasa duniani, kuajiri watu wenye ujuzi, na kufanya ushirikiano na sehemu hizo. Kituo chetu cha utafiti nchini Italia kimeajiri watafiti wengi wa huko, na gari dogo litakalotengenezwa linasanifiwa na kituo hicho."

Mkoani Anhui kampuni nyingine yenye hakimiliki ya ubunifu ni kampuni ya magari ya Chery. Mwaka 2006 kampuni hiyo ilitengeneza magari zaidi ya laki 3, na magari yake yanauzwa katika nchi na sehemu zaidi ya 50 duniani, na uuzaji wake wa magari nchi za nje ulichukua nafasi ya kwanza nchini China. Jambo linalowafanya wafanyakazi wa kampuni hiyo waone fahari ni kuwa, wanapata maendeleo makubwa katika utafiti wa injini, ambalo ni jambo muhimu katika utengenezaji wa magari. Hivi sasa, kampuni ya Chery ina viwanda viwili vya kutengeneza injini, ambavyo vinatengeneza injini za aina 30 zenye uwezo mkubwa za mifumo mitatu, ikiwemo injini ya mfumo wa ACTECO.

Imefahamika kuwa, injini ya mfumo huo ni injini ya kwanza yenye hakimiliki ya ubunifu ya China, na karibu vifaa vyote vya injini ya mfumo huo vinatengenezwa kwa aluminium, hivyo injini hizo ni nyepesi, zinahimili mtikisiko na hazina kelele kubwa. Aidha, usanifu wa injini ya mfumo huo unafuata kabisa kigezo No. 4 cha utoaji wa hewa chafu cha Ulaya.

Injini ya aina ACTECO ya kampuni ya Chery inakubalika katika soko la kimataifa. Kuanzia mwezi Machi mwaka 2006, injini zaidi ya 10,000 ya mfumo wa ACTECO ziliuzwa katika soko la Marekani. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa kampuni ya magari ya China kuuza injini kwa wingi katika nchi zilizoendelea. Mwezi Oktoba mwaka 2006, kampuni ya magari ya Chery ilisaini makubaliano ya ushirikiano kuhusu kutoa injini laki 1 kila mwaka kwa kampuni ya FIAT ya Italia. Inakaridiwa kuwa katika miaka kadhaa ijayo, kiasi cha injini laki 3 za Chery zitatumika katika magari yanayotengenezwa na kampuni ya FIAT.

Msemaji wa kampuni ya Chery Bw. Jin Gebo alisema, moja ya sababu muhimu za Chery kupata mafanikio ni kushikilia mkakati wa kutengeneza magari yenye hakimiliki ya ubunifu. Alisema:

"Uvumbuzi unaifanya kampuni ya Chery iwe na uwezo wa kutengeneza magari yake yenyewe. Tumekuwa na magari ya aina 8 kwenye soko, na mwaka huu pia tutauza magari ya aina 6 sokoni. Kampuni ya Chery itakuwa moja ya makampuni zenye aina nyingi zaidi za magari nchini China, halafu tunaweza kuuza magari katika masoko mbalimbali, na kupata sehemu kubwa zaidi kwenye soko. Hizo ndizo faida tunazopata kutokana na kufanya utafiti na uvumbuzi sisi wenyewe."

Ili kuunga mkono makampuni ya magari ya Jianghuai na Chery kuendeleza magari yenye hakilimiki ya ubunifu, serikali za ngazi mbalimbali mkoani Anhui zimechukua hatua nyingi kuyasaidia, mojawapo ni kuhimiza maendeleo ya shughuli za utengenezaji wa vipuri vya magari, ili kuondoa matatizo ya makampuni ya magari. Ofisa mhusika wa kamati ya usimamizi wa eneo la maendeleo ya uchumi ya Wuhu mkoani Anhui Bw. Wang Qing alisema, kwa kuzingatia mahitaji ya kampuni ya magari ya Chery, sehemu hiyo ilitekeleza sera ya kuhimiza maendeleo ya viwanda vinavyohusika, ambayo inavutia viwanda vingi vya kutengeneza vipuri vya magari kuingia katika sehemu hiyo. Alisema:

"Kwa viwanda husika vya magari vinavyoingia mjini Wuhu, tunafuata sera za eneo la uendelezaji wa uchumi la ngazi ya taifa, na tutatimiza ahadi zetu. Kadiri utengenezaji wa magari ya kampuni ya Chery unavyoongezeka, ndivyo viwanda vingi husika vinaingia katika sehemu hiyo, hivyo inatubidi kuweka mazingira mazuri zaidi ya utoaji huduma. Tunatoa huduma nzuri kwa viwanda vinavyotaka kusajiliwa katika sehemu hiyo ambavyo vinaweza kumaliza utaratibu wote wa kuanzishwa kwake katika ofisi za jengo letu moja tu. Aidha, tunatoa huduma za ufuatiliaji katika uzalishaji wa viwanda hivyo."

Naibu mkurugenzi wa idara ya biashara mkoani Anhui Bw. Zhang Jian alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, licha ya kuongeza hakimiliki ya ubunifu, serikali ya mkoa wa Anhui pia inayahimiza makampuni ya magari kufanya ushirikiano wa teknolojia na nchi za nje.

Idhaa ya kiswahili 2007-06-26