Mkutano wa kimataifa kuhusu suala la Darfur, Sudan ulifanyika tarehe 25 Juni huko Paris, Ufaransa. Watu waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na wajumbe kutoka Marekani, Uingereza, Ufaransa, China na mashirika ya kimataifa yakiwemo Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Umoja wa nchi za kiarabu, benki ya dunia na benki ya maendeleo ya Afrika.
China inatilia maanani sana suala la Darfur. Msaidizi wa waziri wa mambo ya nje Bw. Zhai Jun aliizuru Sudan kwa nyakati tofauti mwezi Januari na Aprili mwaka huu, na mwezi Mei mwaka huu serikali ya China ilimteua mwanadiplomasia mwenye uzoefu Bw. Liu Guijin kuwa mjumbe maalumu anayeshughulikia suala la Darfur. Bw. Liu ameitembelea Darfur mara mbili, ambapo alijionea hali ya huko na kuzungumza na viongozi wa Sudan, pia alipeleka ahadi na misaada kutoka kwa serikali ya China.
Bw. Liu Guijin alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari, alisema "Serikali ya China imeamua kutuma kikosi cha askari wahandisi 275 kutokana na matakwa ya Umoja wa Mataifa. Tumetoa msaada wa kibinadamu wenye thamani ya dola milioni 10 za kimarekani milioni 10 kwa jimbo la Darfur. Pia tutazihamasisha kampuni za China zilizoko Sudan zitoe msaada."
Pamoja na msaada, serikali ya China imetunga mpango wa muda mrefu wa kuisaidia Darfur. Nchini Sudan hususan kwenye jimbo la Darfur, kuna upungufu wa maliasili ya maji, malisho na mashamba, hali hiyo mbaya inachangia migongano na mapambano kati ya makabila tofauti.
Bw. Liu Guijin alisema "Serikali ya China imetuma tume ya wataalamu, tutajenga kituo cha vielelezo vya ufundi wa kilimo nchini Sudan. Kwani hivi sasa asilimia 21 tu ya ardhi ya Sudan inatumika kwa uzalishaji. Mbali na hayo, kampuni za China zinashiriki kwenye mradi wa kupeleka maji huko Daurfur."
Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika baada ya mkutano huo, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki Moon aliipongeza serikali ya China kwa juhudi na mchango iliotoa katika suala la Darfur. Alipofanya majumuisho ya mkutano huo, alitaja maoni yaliyofikiwa na wajumbe wa pande mbalimbali, kwamba Darfur inapaswa kupewa misaada ya kibinadamu, kuweka jeshi la pamoja la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, pia inapaswa kufuatilia suala la maendeleo ya muda mrefu ya Sudan, na kuhimiza utatuzi wa kisiasa wa suala la Darfur. Maoni hayo yanalingana na yale ya China.
Kuhusu malalamiko kutoka kwa vyombo vya habari vya magharibi na wanasiasa wa nchi za magharibi dhidi ya China, kuwa serikali ya China haijafanya juhudi katika kutafuta ufumbuzi wa suala la Darfur. Bw. Liu Guijin alijibu malalamiko hayo, akisema "Serikali ya China imetoa mchango katika kuhimiza mchakato wa amani ya Darfur, hususan China ilifanya jitihada kuishawishi serikali ya Sudan ikubali mpango wa vipindi vitatu uliotolewa na Bw. Kofi Annan, serikali ya Sudan tarehe 12 Juni ilikubali kuwekwa kwa jeshi la pamoja, hivyo ni hatua kubwa. Katika utekelezaji wa mpango huo, zitatokea shida mbalimbali, China inapenda kushirikiana na jumuiya ya kimataifa kuendelea kutoa mchango."
|