|
Mkutano wa ngazi ya kibalozi kati ya Russia na NATO ulimalizika tarehe 26 mjini Moscow, pande mbili zilifanya mazungumzo kuhusu masuala ya usalama, likiwemo suala la mfumo wa kukinga makombora barani Ulaya na "Mkataba wa kupunguza nguvu za kijeshi barani Ulaya", lakini mazungumzo hayo hayakupata mafanikio.
"Mkataba wa kupunguza nguvu za kijeshi barani Ulaya" ulitiwa saini mwaka 1990. Huu ni mkataba wa kwanza kati ya makundi mawili ya kijeshi, iliyokuwa Jumuyia ya Warsaw na NATO, baada ya vita vya pili vya dunia. Baada ya Jumuyia ya Warsar na Urusi ya zamani kusambaratika, mwaka 1999 jumuyia ya ushirikiano wa usalama ya Ulaya ilipitisha "makubaliano ya kurekebisha mkataba wa kupunguza nguvu za kijeshi barani Ulaya", na Russia iliidhinisha makubaliano hayo, lakini hadi sasa hakuna nchi hata moja mwanachama wa NATO iliyoidhinisha makubaliano hayo. Isitoshe, NATO imeharakisha upanuzi wake kuelekea sehemu ya Ulaya ya mashariki, na nchi za Ulaya ya mashariki ambazo hapo zamani zilikuwa sehemu ya katikati kati ya Urusi ya zamani na NATO zimejiunga na NATO, Hali hiyo pamoja na mpango wa Marekani wa kuweka mfumo wa kukinga makombora katika nchi za Poland na Czech, inaifanya Russia ione kuwa inatishiwa.
Rais Putin wa Russia mwezi Aprili kwenye ripoti ya hali ya taifa alisema, kutokana na nchi zilizokuwa wanachama wa jumuyia ya Warsar kujiunga na NATO, na hali mpya ya kisiasa katika kanda hiyo, Russia ina haja ya kusimamisha kutekeleza "mkataba wa kupunguza nguvu za kijeshi barani Ulaya". Waziri wa mambo ya nje wa Russia Bw. Sergei Lavrov kwenye mkutano huo alisema, "mkataba wa kupunguza nguvu za kijeshi barani Ulaya" ni msingi wa usalama barani Ulaya na pia ni mkataba wa pande nyingi, lakini hali ilivyo sasa inaonesha kuwa Russia ni nchi pekee inayotekeleza mkataba huo. Bw. Sergei Lavrov alisema, tokea mwaka 1999 "makubaliano ya kurekebisha mkataba wa kupunguza nguvu za kijeshi" ulipopitishwa hadi sasa, hakuna nchi hata moja ya NATO iliyoidhinisha makubaliano hayo, na baadhi ya nchi za NATO zinaongeza nguvu za kijeshi na kuitishia Russia kutokana na kutoidhinisha makubaliano hayo.
Kwenye mkutano huo, katibu mkuu wa jumuyia ya NATO Bw. Hoop Scheffer pia hakutaka kulegeza msimamo wake kuhusu suala hilo. Alisema pande mbili hazikufikia makubaliano lakini mazungumzo yataendelea, na NATO inaona kuwa kuidhinisha "makubaliano ya kurekebisha mkataba wa kupunguza nguvu za kijeshi barani Ulaya" ni lazima kuendana na "makubaliano ya Istanbul" ambayo yanataka Russia iondoe majeshi yake kutoka Georgia na Moldova.
Na misimamo ya pande mbili kuhusu mfumo wa kukinga makombora barani Ulaya inatofautiana kabisa. Kamanda mkuu wa majeshi ya Russia Yuri Baluyevsky aliwahi kusema, kutokana na Russia kuishauri Marekani kutumia kituo cha rada kilichopo Azerbaijian kwa pamoja, Marekani inapaswa kusimamisha kuweka mfumo wa kukinga makombora katika sehemu ya Ulaya ya mashariki, kama Marekani inakataa pendekezo hilo, "watu wote wanaelewa kwamba mfumo wa kukinga makombora unaotaka kuwekwa na Marekani unamlenga nani". Wakati wa mkutano huo naibu waziri mkuu wa Russia Bw. Sergei Ivanov aliwaambia waandishi wa habari kuwa Russia imeanza kutengeneza aina mpya za makombora, na kuingia katika kipindi kipya cha nguvu za nyuklia.
Ingawa misimamo ya pande mbili inagongana, lakini hali ya sasa inaonesha kuwa pande mbili hazitaki kuacha kabisa mazungumzo. Tarehe 26 rais Putin alisema mazungumzo kati ya Russia na NATO yanasaidia kuleta usalama na amani duniani. Alisema ni kawaida kuwepo kwa matatizo kati ya Russia na NATO, na ana uhakika kwamba pande mbili zinaweza kutatua suala hilo kwa njia ya mazugumzo. Bw. Hoop Scheffer pia alisema NATO haina chaguo jingine ila kuwa na uhusiano wa kawaida na wa kirafiki na Russia. Hii ina maana ya kuwa pande mbili zinatumai kutatua tofauti zao kwa njia ya mazungumzo.
|