Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-06-27 21:40:37    
Ngoma ya "Huadeng" ya kabila la Wa-Tu waishio mkoani Guizhou

cri

Wakazi wa kabila la Tu wa mji wa Xujiabei wa wilaya ya Sinan, mkoani Guizhou wakisikia muziki wa ngoma wanajua kuwa, ngoma ya "Huadeng" itachezwa. Kwenye ua mmoja wa familia ya mkulima, watazamaji walijaa, wakiwaangalia wachezaji waliovaa mavazi ya rangi mbalimbali wakichezea vipepeo na vitambaa walivyoshika mikononi huku wakiimba nyimbo kwa furaha.

Mji wa Xujiabei ni maskani ya ngoma ya "Huadeng", ambayo ilianzishwa katika enzi ya Tang miaka zaidi ya 1000 iliyopita. Ngoma ya "Huadeng" ya kabila la Wa-Tu huonesha shughuli zao za maisha ya kila siku, kama vile shughuli za matambiko, shughuli za kilimo, kuchuma majani ya chai, na kusherehekea mavuno mazuri, hata kuwaelimisha wakazi wafuate maadili. Naibu mkurugenzi wa idara ya uenezi ya wilaya ya Sinan Bwana Meng Qingsheng alisema:

"Ngoma ya 'Huadeng' inapendwa na wakazi wengi kutokana na kuwa, ngoma hiyo si kama tu inaweza kuchezwa jukwaani, bali pia inaweza kuchezwa kwenye ua wa nyumba za wakulima, hata kwenye nafasi za wazi mashambani. Na umaalum wake mwingine ni kuwashirikisha watu wote, yaani baadhi ya watu wanaimba huku wengine wakicheza kwa kufuata midundo ya nyimbo hata makofi."

Bw. Meng Qingsheng alifahamisha kuwa, katika mchakato wa uendelezaji, ngoma ya "Huadeng" ilikuwa imeonesha umaalum wa uchangamfu na midundo mikali ya muziki wa jadi wa kabila la wa-Tu. Mwaka 2006 ngoma ya "Huadeng" ya kabila la Tu iliorodheshwa kuwa urithi wa utamaduni usioonekana nchini China.

Bwana Xu Chaozheng ni msanii maarufu wa ngoma ya "Huadeng" wa kabila la wa-Tu katika wilaya ya Sinan. Maonesho yake huwachekesha watazamaji kwa uimbaji wake wenye vichekesho ukiambatana na vitendo vya kutia chumvi. Ili kurithisha ustadi wake wa kuchezea ngoma ya "Huadeng", amewafundisha wanafunzi wengi ambao tayari wamekuwa hodari katika fani hiyo, baadhi yao hata walinyakua nafasi katika mashindano ya ngoma ya "Huadeng" ya mkoani Guizhou.

Hivi sasa katika wilaya ya Sinan kuna vikundi vikubwa na vidogo 200 hivi vya ngoma ya "Huadeng". Kucheza ngoma ya "Huadeng" kumekuwa shughuli za maisha ya kila siku kwa watu wa kabila la wa-Tu. Si kama tu inachezwa katika sikukuu maalum, bali pia inachezwa wakati wa kufanya shughuli za maadhimisho au wakati wa mapumziko ya kilimo. Asubuhi watu wanacheza ngoma ya "Huadeng" ili kujenga mwili, na jioni wanacheza ngoma hiyo kwa kuondoa uchovu. Mkurugenzi wa mji wa Xujiabei Bwana Shao Jianfeng alisema, ngoma ya "Huadeng" ya kabila la Tu si kama tu inawafurahisha wakazi wa huko, bali pia inawavutia watalii wengi wa nchini China na nchi za nje. Alisema:

"Tarehe 15 Januari ya mwaka huu wa jadi, mji wetu ulifanya maonesho makubwa ya ngoma ya "huadeng" ya taa zilizotengenezwa kwa umbo la dragon na la Simba, maonesho hayo yaliwavutia watalii wengi kutoka sehemu nyingine nchini China."

Hivi sasa wilaya ya Sinan iko mbioni kuenzi zaidi chapa maalum ya ngoma ya "Huadeng" ya kabila la wa-Tu, kuendeleza michezo ya jadi ya ngoma hiyo na kuieneza wilayani kote, ili ichezwe katika mitaa ya miji, vijiji na shule.

Wasikilizaji wapendwa, mkiwa na nafasi mnakaribishwa kutembelea katika wilaya ya Sinan kujionea wenyewe umaalum wa ngoma ya "Huadeng" ya kabila la wa-Tu. Katika wilaya ya Sinan, si kama tu kuna ngoma ya "Huadeng", bali pia kuna mandhari nzuri ya kimaumbile, genge maarufu la Mto Wu, mapango ya Gange na misitu ya mawe, pamoja na mji mzuri wa Sinan.