"Taarifa kuhusu idadi ya watu duniani mwaka 2007" iliyotolewa na shirika la utoaji misaada kuhusu idadi ya watu la Umoja wa Mataifa tarehe 27 mwezi Juni kwenye makao makuu yake mjini New York inasema, idadi ya wakazi wa mijini itafikia bilioni 3.3 ifikapo mwaka 2008, na ni mara ya kwanza kwa idadi hiyo kuzidi nusu ya jumla ya idadi ya watu duniani. Taarifa hiyo inatoa wito wa kutaka nchi mbalimbali zijiandae kubadilisha athari mbaya kuwa nguvu ya kujenga ili kupunguza kadiri iwezavyo athari mbaya inayoletwa na mchakato wa ujenzi wa miji.
Taarifa inasema katika miaka ya hivi karibuni ujenzi wa miji duniani unaendelezwa kwa kasi kubwa isiyowahi kuonekana hapo kabla. Idadi ya wakazi wa mijini itafikia bilioni 5 ifikapo mwaka 2030, ambapo idadi ya wakazi wa miji ya nchi zinazoendelea itaongezeka kwa haraka zaidi, hivi sasa ongezeko la idadi ya wakazi wa miji ya nchi za Asia litafikia kiasi cha milioni moja kwa wiki. Kutoka mwaka 2000 hadi mwaka 2030, idadi ya wakazi wa miji ya nchi za Asia itaongezeka na kufikia bilioni 2.6 kutoka bilioni 1.4, wakati idadi ya wakazi wa miji barani Afrika itaongezeka kufikia karibu milioni 750 kutoka milioni 300, idadi ya wakazi wa miji ya Latin Amerika na sehemu ya Caribbean itaongezeka na kufikia milioni 600 kutoka milioni 400. Kwa ufupi ni kuwa, idadi ya wakazi wa miji ya Asia na Afrika itaongezeka maradufu katika kipindi cha kizazi kimoja.
Kuhusu idadi ya watu wa China, taarifa hiyo inasema hivi sasa ujenzi wa miji nchini China umefikia kileleni. Katika miaka 10 ijayo, kiasi cha wachina milioni 870 wataishi mijini ikichukua nusu ya jumla ya idadi ya watu wa China. Kwa upande mwingine, katika muda wa miaka 10 ijayo, China itakuwa na miji 87, ambayo idadi ya wakazi wa mji itazidi laki 7.5. Taarifa hiyo inapendekeza kuwa, wakati wa kubuni mpango wa maendeleo inatakiwa kuzingatia athari zinazoletwa kwa miji ya pwani kutokana na kuongezeka kwa maji ya baharini inayosababishwa na ongezeko la joto la dunia, kwani idadi hiyo ya watu wanaishi katika miji ya pwani.
Taarifa pia inasema, matatizo yanayoambatana na mchakato wa ujenzi wa miji ni ongezeko la idadi ya watu maskini pamoja na kuongezeka kwa matatizo mbalimbali yakiwemo upungufu wa nyumba za wakazi na mazingira, hususan maeneo ya vibanda hafifu vya watu maskini ya mijini, ambayo 90% yake yako katika nchi zinazoendelea, na Asia ya kati na ya kusini zinachukua nafasi ya kwanza, zikifuatwa na Asia ya mashariki na sehemu ya kusini mwa Sahara barani Afrika. Watu hao wanakosa ajira hata mahali pa kujisetiri.
Taarifa hiyo pia inasema mchakato wa ujenzi wa miji unanufaisha zaidi miji hiyo yenyewe, isipokuwa miji hiyo inashindwa kutoa ajira za kutosha, hususan ni kuwa wanawake wanabaguliwa katika shughuli muhimu za kijamii, watoto wa kike watakuwa wa kundi la kwanza la watoto wanaoshindwa kwenda shule. Watu hao wanyonge wananyimwa nafasi mbalimbali zinazoletwa na mchakato wa ujenzi wa miji. Idara za serikali zikitaka kutatua au kuepusha matatizo hayo, basi zinatakiwa kubuni mipango mapema, ili ziweze kutoa huduma za kimsingi za elimu, ajira na nyumba kwa watu waliomiminikia mijini. Tukitaka kufanikisha mpango huo, tutakabiliwa na changamoto kubwa, kwani hali hiyo inahusika na suala kubwa la mgawanyo wa raslimali za jamii. Utatuzi wa masuala hayo, licha ya kuhitaji serikali za nchi mbalimbali kufanya ushirikiano mkubwa na jumuiya za kimataifa na kiserikali, pia unahitaji kujenga uhusiano wa kiwenzi wa ushirikiano duniani, na kuzihamasisha sekta mbalimbali za jamii kushiriki kwa juhudi.
Ofisa wa shirika la utoaji misaada kuhusu idadi ya watu la Umoja wa Mataifa Bw. Ann Leoncavallo siku hiyo alisema, ingawa tunashindwa kuzuia ongezeko la idadi ya watu na mchakato wa ujenzi wa miji, lakini ikiwa athari mbaya zinazoletwa na mchakato wa ujenzi wa miji zitaweza kurekebishwa kwa wakati, basi mchakato wa ujenzi wa miji utahimiza kwa nguvu maendeleo ya uchumi wa dunia.
|