Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-02 15:11:09    
Maisha ya furaha yanapatikana kutokana na kuwa na ndoto

cri

Tarehe 19 kundi la China la wasanii walemavu lilifanya maonesho ya mwisho mjini Berlin, na kumaliza maonesho yake ya mzunguko katika nchi tano za Ulaya.

Dansi ya "Ndoto Yangu" iliyochezwa na wasanii hao ilipomalizika tu, mara makofi yalipigwa kwa muda mrefu ndani ya ukumbi wa ubalozi wa China mjini Berlin Ujerumani. Watazamaji wa Wachina na Wajerumani walivutiwa na kufurahia maonesho hayo ya ajabu. Hayo ni maonesho ya mwisho katika maonesho ya mzunguko katika nchi tano barani Ulaya.

"Watu huwa na matumaini katika maisha yao, maonesho yetu ya michezo yote yanatoka ndani ya mioyo yetu na kila muziki unaimbwa kutoka kwenye damu zetu."

Sauti ya msanii huyo ni tofauti na sauti ya kawaida, hii ni sauti ya msichana mwenye ulemavu wa kutosikia. Msichana huyo anayeitwa Tai Lihua ana umri wa miaka 29, alipoteza uwezo wake wa kusikia alipokuwa na umri wa miaka miwili. Yeye ni mmoja wa wasanii muhimu wanaocheza dansi katika kundi hilo, ingawa hawezi kusikia lakini ni mcheza dansi aliyewahi kupanda kwenye jukwaa katika jumba la muziki la Marekani Carnegie na jumba la michezo ya kuigiza Skara nchini Italia. Baada ya maonesho kumalizika, aliwaambia waandishi wa habari kwa ishara za mikono,

"Dansi ya 'Ndoto Yangu" inawaeleza watazamaji kuwa kila mtu ana ndoto yake lakini kutimiza ndoto kunahitaji juhudi."

Kundi la wasanii walemavu ni kundi pekee nchini China, mada ya michezo yao ni kuthamini maisha na kupenda amani. Mjini Berlin walionesha mchezo wao wa dansi wa 'Mungu wa kike mwenye mikono elfu moja' na muziki wa piano uitwao "mbalamwezi" na wimbo "marafiki". Ingawa maonesho yao hayakuwa na muda mrefu, lakini moyo wao wa kujiimarisha na usiokubali kushindwa mbele ya shida, uligusa sana hisia za watazamaji.

Wimbo uitwao "Pepo" ulioimbwa na mlemavu asiyeona Yang Haitao ulishangiliwa kwa makofi ya muda mrefu, ingawa watazamaji Wajerumani hawakuelewa alichoimba, lakini sauti yake tamu na uchangamfu wake vilmvutia kila mtazamaji. Aliwaambia waandishi wa habari alisema,

"Nilipenda sana muziki toka nilipokuwa mtoto mdogo kutokana na kuwa muziki unanifurahisha. Nilikuwa na ndoto ya kuwa mwimbaji, na mara kwa mara nilikuwa nasikiliza na kuimba imba mpaka sasa."

Ingawa Yang Haitao hawezi kuona lakini moyoni mwake sio giza. Nchini China anasifiwa kuwa ni "mwimbaji wa peponi". Ikilinganishwa na furaha anayopata kutokana na kuimba tatizo la kimwili alilonalo ni dogo sana, aliwaambia waandishi wa habari kwamba ameweza kuimba hata nyimbo kwa lugha ya Kijerumani.

Dansi iliyochezwa na wasanii walemavu wasiosikia Zhao Ligang na Tai Lihua ilieleza hadithi ya mapenzi ya kuhuzunisha, waliwaambia waandishi wa habari kuwa, jukwaa ni mahali pa wao kuonesha jinsi walivyo, wanaposimama jukwaani na kuangaliwa na watazamaji, wengi wanakuwa wamezama katika mada ya dansi yao.

Wakati maonesho yanapomalizika, watazamaji wanasimama na kuwapigia makofi kwa muda mrefu, mtizamaji wa Ujerumani Bw. Ulrich Ralf alitulia pale alipokaa bila kutaka kuondoka, aliwaambia waandishi wa habari, akisema,

"Maonesho haya yananisisimua kweli, hasa kwa kuwa yanafanywa na walemavu, wao ni tofauti na sisi, ni shida kwao kufanya vitendo mbalimbali. Maonesho yao ni ya kusisimua kweli."

Balozi wa China nchini Ujerumani Bw. Ma Canrong kabla ya maonesho alisema

"Maonesho mazuri ya kundi la China la wasanii walemavu yamethibitisha kuwa, walemavu pia wanaweza kupata mafanikio katika utamaduni, sanaa na michezo sawa na watu wengine."

Idhaa ya kiswahili 2007-07-02