Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-02 19:38:16    
Hali ya utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia ya Umoja wa Mataifa

cri

Baraza la uchumi na jamii la Umoja wa Mataifa tarehe 2 Julai huko Geneva limetoa ripoti likijumuisha hali ya kipindi cha katikati cha utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia ya Umoja wa Mataifa katika miaka saba iliyopita. Ripoti hiyo imesema nchi mbalimbali duniani, hasa nchi na sehemu zilizo nyuma kabisa kimaendeleo zimepata maendeleo mazuri, lakini kama malengo ya maendeleo ya milenia yanatakiwa kutimizwa kikamilifu ifikapo mwaka 2015, nchi mbalimbali zinatakiwa kufanya juhudi kubwa zaidi.

Malengo ya maendeleo ya milenia ya Umoja wa Mataifa yalitolewa mwaka 2000, yanataka idadi ya watu maskini duniani ipunguzwe kwa nusu ndani ya miaka 15. Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imekusanya pamoja takwimu zilizotolewa na shirika la afya duniani, shirika la biashara duniani, na shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, kujumuisha kikamilifu hali ya utekelezaji wa malengo manane ya maendeleo. Ripoti hiyo itawasilishwa kujadiliwa kwenye mkutano wa mwaka wa baraza la uchumi na jamii la Umoja wa Mataifa unaotazamiwa kufunguliwa siku hiyo huko Geneva.

Ripoti hiyo imeozungumzia mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia ya Umoja wa Mataifa. ikisema, mwaka 2004 idadi ya watu maskini duniani ilichukua asilimia 20 ya idadi yote ya watu duniani kutoka ile ya theluthi moja ya mwaka 1990. Kama mwelekeo huo utadumishwa, ifikapo mwaka 2015, lengo la kupunguza idadi ya watu maskini kwa nusu huenda litaweza kutimizwa.

Nchi mbalimbali pia zimepata mafanikio kadhaa katika kueneza elimu ya msingi, kuhimiza usawa wa kijinsia, kupunguza idadi ya watoto wanaokufa kutokana na magonjwa na kupambana na maradhi. Mwaka 2005 kiasi cha watoto waliosoma kwenye shule ya msingi kilifikia asilimia 88 kutoka kile cha asilimia 80 cha mwaka 1991, na kiasi cha watoto waliokufa pia kilionekana kupungua mwaka hadi mwaka.

Ripoti hiyo pia imeeleza changamoto kubwa inayoukabili utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia duniani. Katika miaka ya hivi karibuni idadi ya watu waliokufa kutokana na ugonjwa wa Ukimwi imekuwa inaongezeka mwaka hadi mwaka, ambapo watoto yatima wa ukimwi mamilioni kadhaa wamebaki. Hivi sasa kila mwaka wanawake laki tano duniani wanakufa kutokana na ujauzito na kujifungua. Watoto milioni 300 duniani wanakumbwa na utapiamlo, wengi wao wako katika sehemu ya Asia ya kusini na bara la Afrika.

Ripoti hiyo inazihimiza nchi mbalimbali kuweka malengo ya maendeleo ya milenia katika mkakati wa kitaifa, serikali na sekta mbalimbali za jamii kufanya juhudi za pamoja ili kuhimiza uzalishaji na kuendeleza uchumi kwenye mazingira yenye utulivu.

Mambo makubwa mawili yanayokwamisha utimizaji wa malengo ya maendeleo ya milenia ni kuzorota kwa hali ya mazingira duniani, na nchi zilizoendelea kutotekeleza ahadi zao za kutoa misaada ya maendeleo kwa serikali. Ripoti hiyo imedhihirisha kuwa, malengo ya maendeleo ya milenia ni mpango mzuri ulioandaliwa kwa pamoja na nchi mbalimbali duniani, nchi zote zinawajibika kufanya juhudi katika kutimiza malengo hayo. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon amesema, kama nchi mbalimbali zitaonesha vya kutosha nia yao ya kisiasa, na kuchukua hatua mwafaka na kuzitekeleza kivitendo, basi malengo ya maendeleo ya milenia yataweza kutimizwa kwa wakati.