Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-03 17:17:57    
Mkutano wa marais wa Russia na Marekani utakuwaje?

cri

Tarehe mosi Julai rais George Bush wa Marekani na rais Vladimir Putin wa Russia walikutana nyumbani kwa rais Bush kwenye jimbo la Maine nchini Marekani, na walifanya mazungumzo kuhusu mpango wa Marekani wa kuweka mfumo wa kukinga makombora Ulaya ya Mashariki na suala la Iran. Vyombo vya habari vinaona kuwa, hii ni mara ya mwisho kwa marais hao kukutana kuboresha uhusiano wa wasiwasi kati ya nchi mbili, kabla ya wao kuondoka madarakani.

Baada ya mkutano huo rais Putin aliwaambia waandishi wa habari kwamba haoni kama kuna haja ya kuweka mfumo wa kukinga makombora katika nchi za Czech na Poland, lakini kwa ajili ya kutatua tatizo hilo, kuna haja ya kuziingiza nchi nyingi zaidi za Ulaya zinazohusika na tatizo hilo kwenye mazungumzo ya "Russia na NATO", alipendekeza nchi za Russia na Marekani zianzishe kituo cha maingiliano ya habari. Bw. Putin alisema kwa kufanya hivyo uhusiano kati ya Russia na Marekani utainuka zaidi.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Marekani ilitoa pendekezo la kuweka mfumo wa kukinga makombora katika nchi za Czech na Poland kwa hoja ya kujikinga na makombora kutoka Iran, mpango huo ulipingwa na Russia. Kwenye mkutano wa kilele uliofanyika mwezi Juni, rais Putin bila kutarajiwa alipendekeza kwa Marekani iweke mfumo huo nchini Azerbaijan na kusema kwamba Russia inapenda kutumia kituo chake cha rada kilichopo huko pamoja na Marekani. Serikali ya Bush haikujibu lolote kuhusu pendekezo hilo, na uhusiano kati ya nchi hizo mbili ukawa katika hali ya kutoelewana. Sasa rais Bush amemkaribisha rais Putin nyumbani kwake, vyombo vya habari vinaona kuwa hizi ni juhudi za rais Bush kwa ajili ya kutatua mgongano kati yao. Hadi sasa haijajulikana kama mkutano huo utafanikiwa kwa kiasi gani. Mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani Bw. Stephen Hadley alisema, marais wawili hawakufikia makubaliano sana kuhusu suala la kuweka mfumo wa kukinga makombora, lakini Russia ilipendekeza kutumia kituo cha rada cha Azerbaijan na kuanzisha kituo cha mawasiliano ya habari, na kuzijumuisha nchi nyingi zaidi kwenye kituo hicho, hii ina maana kuwa Russia ina moyo wa kushirikiana na Marekani.

Licha ya mfumo wa kukinga makombora, marais hao walijadiliana suala la Iran. Kwenye mkutano na waandishi wa habari rais Bush alikataa kudokeza habari yoyote kuhusu suala hilo, ila tu alisema nchi hizo mbili zina msimamo wa namna moja kuhusu suala la nyuklia la Iran.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa ushauri likizihimiza Russia na nchi nyingine wajumbe wa Baraza hilo zichukue hatua kali zaidi dhidi ya Iran. Ushauri huo unasema bidhaa zote zinazotoka na kuingia nchini Iran zikaguliwe ili kuhakikisha hakuna bidhaa za nyuklia na silaha haramu. Vyombo vya habari vinasema maofisa wa Marekani na maofisa wengine wa Russia na Baraza la usalama wamejadili ushauri huo, lakini Bw. Bush na Bw. Putin hawakusema kama wamefikia makubaliano kuhusu hatua hizo mpya.

Kuhusu uhusiano kati ya nchi hizo mbili, kwenye mkutano na waandishi wa habari marais walionekana wakijitahidi kuwaambia waandishi wa habari kwa uhusiano wa nchi hizo mbili ni mkubwa na wa utulivu. Rais Bush alisema walifanya mazungumzo mazuri, baadhi ya masuala wanaafikiana na kwenye masuala mengine wanapingana. Alisema msimamo wa Putin ni wazi na yeye ni mtu anayeaminika. Rais Putin alisema, anafurahia mazungumzo yao, ambayo yanajitahidi kutafuta maslahi yao ya pamoja.

Mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani Bw. Hadley alisema, nchi hizo mbili zimeafikiana kuhusu ushirikiano wa nishati ya nyuklia kwa ajili ya uchumi, na Jumanne wiki hii mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili watasaini makubaliano hayo.

Vyombo vya habari vinaona kuwa uhusiano kati ya Marekani na Russia umekuwa mbaya kabisa tokea "vita vya baridi" kumalizika. Bw. Putin ni rais wa kwanza kutembelea nyumbani kwa rais Bush. Rais Bush alisema "mazungumzo yao ni ya muda mrefu na ya kimkakati". Vyombo vya habari vya Marekani vinasema hayo yote hayawezi kuficha ukweli kwamba mgongano uliosababisha uhusiano kuwa na wasiwasi haukutoweka katika mazungumzo hayo.

Idhaa ya kiswahili 2007-07-03