Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-03 18:29:01    
Barua 0701

cri

Msikilizaji wetu Paul Mungai Mwangi wa sanduku la posta 69, Kinangop Kaskazini injinia, Kenya ametuletea barua akianza kwa salamu zake kwa watangazaji na wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa. Anasema hana shaka kwamba sote tu buheri wa afya, na yeye pamoja na familia yake wote ni wazima. Anasema anapenda kutumia fursa hii kuwasalimia wasikilizaji na mashabiki wenzake wote wanaokienzi kituo hiki cha Radio China Kimataifa.

Anasema anapenda pia kuwapongeza mabwana Mutanda Ayub Shariff na Franz Manko Ngogo kwa kujishindia nafasi maalum katika chemsha bongo ya mwaka wa 2006, na kupata nafasi ya kuzuru China ili kuwawakilisha wasikilizaji wengine wa Afrika mashariki katika sherehe za kuadhimisha miaka 65 ya Radio China Kimataifa.

Bw Mwangi anasema hawezi kuhitimisha barua hii kabla hajatoa shukrani zake za dhati kwa watangazaji na wafanyakazi wa Radio China Kimataifa kwa vipindi vya kusisimua ambavyo vinadhihirisha vya kutosha umahiri wa kikazi. Anavutiwa sana na kipindi cha Safari nchini China, ambacho humfanya ajihisi kama yeye mwenyewe anatembelea mandhari mbalimbali ya kuvutia nchini China, anapendekeza kuwa, kama inawezekana kipindi hiki kiwe ni cha kila siku. Mwisho anaomba tumtumie picha za watangazaji wote pamoja na historia ya ukuta mkuu wa China.

Tunamshukuru Paul Mungai Mwangi kwa barua yake na maoni yake kwa vipindi vyetu, tumefurahi kuona wasikilizaji wetu wengi wanapenda kusikiliza kipindi cha Safari nchini China, jinsi kama wachina wengi wanavyopenda mandhari nzuri barani Afrika, tutaendelea na juhudi zetu kuandaa vizuri vipindi vyetu ili wasikilizaji wetu waweze kupenda kuvisikiliza.

Msikilizaji wetu Emmanuel Bernard wa kemogemba sanduku la posta 71 Tarime Mara TANZANIA ametuandikia barua akisema anatoa salamu zake kwa wasikilizaji na wafanyakazi wa Radio China kimataifa, na ana matumaini kuwa salamu zake zitapokelewa kwa moyo mmoja. Pia anatoa pole na pongezi nyingi kwa kazi nzuri ya kurusha matangazo katika bara la Afrika na hasa kwa Afrika mashariki. Anasema aliwahi kumsikia kwa mara ya kwanza mtangazaji Fadhili Mpunji, Radio Tanzania Dar es Salaam miaka 1990, wakati huo alikuwa na umri wa miaka 8 na alikuwa akipeleka salamu katika kipindi cha asubuhi. Anatumai kuwa kwa sasa Fadhili Mpunji ni mzee sana, kwani umri umekwenda. Anaomba amtumie viatu vya mpira wa miguu jozi moja au soksi tu zinatosha kwa kuwa yeye ni mwanasoka mashuhuri katika wilaya yao. Anasema kuna methali inayosema akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli. Mwisho anamaliza barua yake kwa kumtakia kazi njema na mungu ambariki katika kazi yake, na iko siku wataonana ana kwa ana kama Ras Manko Ngogo alivyokuja China kutalii.

Haya Bw Emmanuel Bernad nakushukuru sana kwa kufuatilia matangazo yetu, ni kweli kuwa miaka ya 90 nilikuwa Radio Tanzania na sasa naendelea kufanya kazi na ndugu zetu wachina. Nimesikia ombi lako la jozi ya viatu au jozi ya soksi za mpira. Naweza kusema sio vigumu kukutumia jozi ya soksi, lakini wasiwasi ni wangu ni kuhusu uhakika wa kuweza kukufikia kwa soksi hizo. Kama kutakuwa na utaratibu rahisi na wa uhakika wa kukutumia, sitasita kufanya hivyo. Kwa hiyo la muhimu kwa sasa ni kusubiri fursa hiyo kutokea, na tuendelee kukumbushana.

Bw Bernard anasema kwenye barua yake nyingine kuwa anashukuru sana kwa kumtumia kadi za salamu pamoja na karatasi ya maswali ya chemsha bongo. Lakini anasema kuwa aliwahi kutuandikia barua nyingine kuhusu kutuomba vifaa vya michezo lakini barua zake hazikujibiwa.

Anamaliza barua yake kwa kuomba kalenda na majarida ya mwaka huu ambayo yana matukio ya mambo ya China. Hana la zaidi ila anawatakia kila la heri watangazaji na wasikilizaji wenzake wa Radio China Kimataifa.

Tunakushukuru sana Bw Bernard kwa barua yako. Tunafurahi kuona kuwa wewe ni mfuatiliaji wa matangazo yetu. Tunakumbuka kuwa tulipata barua yako yenye maombi kuhusu vifaa vya michezo. Maombi yako hatukujibu kwa njia ya maandishi, lakini tulijibu kwa njia ya kipindi hiki. Kwa kweli tunakuomba wewe na wasikilizaji wengine mtuelewe kuwa, sisi kazi yetu ni kutangaza habari na vipindi vingine, mambo ya vifaa vya michezo na misaada inayohusiana na vifaa vya michezo vinashughulikiwa na idara nyingine tofauti. Tungependa sana kuwafurahisha wasikilizaji wetu kwa kuwapa zawadi kama hizo, lakini tunasikitika kuwa zawadi kama hizo zinatolewa na idara nyingine, sisi kazi yetu inahusiana na matangazo tu, tunaomba mtuelewe.

Msikilizaji wetu mwingine kutoka klabu ya wasikilizaji ya Kemogemba Francis Nyakaira wa Sanduku la posta 71 Tarime Mara, Tanzania, kwenye barua aliyotuandikia ana maoni kuhusu chemsha bongo ya mkoa wa Sichuan, maskani ya Panda. Anasema China ni nchi inayoendelea yenye mabonde na milima, miji na vijiji vingi vinavyopendeza.

Anaendelea kusema kuwa kinachompa moyo na nia ya kutaka kuwa mmoja ya washindi watakaozuru maskani ya Panda, ni ule uthabiti wa utunzaji wa mandhari nzuri zenye mvuto na hata kupata msukumo mkubwa wa kuwa na hadhi ya urithi wa kimaumbile duniani na hivyo kuwekwa kwenye orodha ya kudumu mwaka 1992.

Pia anasema toka awe msikilizaji wa Radio China Kimataifa, anaipenda Radio China kama anavyoipenda nafsi yake kwa sababu China ina mikoa na vitu mbalimbali vya kuvutia kuliko nchi nyingine duniani. Ametoa mfano wa eneo la Sanxingdui lilivyowahi kung'ara kwa miaka 2000.Anasema duniani kuna mengi yanayoweza kuwa mazuri licha ya sehemu moja hadi nyingine. Mwisho anamaliza barua yake kwa kusema asante Radio China Kimataifa kwa kutupa chemsha bongo hiyo.

Tunamshukuru Francis Nyakaira kwa barua yake ya kuelezea jinsi alivyoshiriki katika mashindano ya chemsha bongo yaliyoandaliwa na Radio China Kimataifa na kuongeza ujuzi kuhusu hali ya nchini China, ni matumaini yetu kuwa, wasikilizaji wetu wataendelea kusikiliza vipindi vyetu na kutoa maoni na mapendekezo yao, na kudumisha mawasiliano na urafiki kati yetu.

Msikilizaji wetu Okongo Okeya wa S.L.P 381 Iganga nchini Uganda anaanza barua yake kwa kusema "Mungu ibariki Radio China kimataifa". Anasema Radio China Kimataifa imekuwa mkombozi wa nyoyo za wasikilizaji wake popote pale ulimwenguni na imekuwa daraja la kuyaunganisha mataifa yote ulimwenguni. Radio China Kimataifa haina ubaguzi, kwani haijali dini kabila wala rangi ya mtu yoyote, ni radio ya watu duniani. Katika umri wake wa miaka 65, Radio China kimataifa imewaweka wasikilizaji wake kote ulimwenguni pamoja.

Mwisho anatoa pongezi za dhati kwa viongozi na watangazaji wote wa Radio China kimataifa kwa kazi nzuri sana wanayoifanya. Vipindi motomoto vinavyoelimisha, kufundisha, na kuburudisha vinaifanya Radio China kimataifa iwe daraja la urafiki duniani na iwe tofauti na radio zingine. Bwana Okeya pia anatoa mwito kwa watu ulimwenguni kuitegea sikio Radio China Kimataifa kila siku ili waweze kuelimika, kuburudika na kujua mambo yanayojiri China na duniani kwa ujumla, na mwisho anawatakia kila la heri wafanyakazi wote wa Radio China katika kazi zao na wazidishe juhudi bila kuchoka.

Tunamshukuru Okongo Okeya kwa barua yake ya kututia moyo, Bwana Okongo Okeya kila mara ametuandikia barua kadhaa kueleza usikivu wake na maoni na mapendekezo yake, kweli ufuatiliaji wa wasikilizaji wetu unatuhimiza tuchape kazi zaidi ili kufurahisha wasikilizaji wetu na kuongeza maelewano na urafiki kati ya wasikilizaji na Radio China Kimataifa.