Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-04 17:41:46    
"Mfugaji Xibao Ligao na mpango wake wa kujiendeleza kwa familia kwenye ardhi ya mchanga

cri

Xibao Ligao ni mkulima anayeishi katika wilaya ya Naiman ya mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani. Maskani yake yako kwenye sehemu yenye mchanga ya Kerqin, ambayo ni sehemu yenye ardhi kubwa kabisa ya mchanga nchini China. Ili kuhifadhi mazingira ya kimaumbile na kujiendeleza kiuchumi, Bw. Xibao Ligao na familia yake walianzisha njia ya sambamba ya kujiendeleza na kuhifadhi mazingira.

Nyumba ya familia ya Bw Xibao Ligao ina vyumba vinne, mbele ya nyumba yake yalianikwa mahindi, kwenye pembe moja ya ua wa nyumba yake iliegeshwa pikipiki, pembeni mwa nyumba yake kuna zizi la mifugo, milio ya ng'ombe na kondoo ilikuwa inasikika wazi. Kwenye sehemu iliyo karibu na nyumba hiyo imepandwa miti ya Poplar yenye urefu wa zaidi ya mita kumi na vichaka vya willow, na mbali zaidi kuna mashamba. Ukiona hali ya ustawi kama hiyo, kabisa huwezi kuamini kuwa sehemu hiyo ilikuwa ya vilima vya mchanga.

"Hiyo ilikuwa ni sehemu ya vilima vya mchanga, upepo ukivuma mchanga ulikuwa unapeperushwa hadi kufika ndani ya nyumba na hata kuziba mlango. Ni vigumu kumudu maisha bila kupambana na mchanga. Mwanzoni tulikumbwa na matatizo makubwa katika kupambana na mchanga, tukipanda miti leo, siku chache baadaye miti hiyo ikafunikwa na mchanga au kung'olewa na upepo."

Mwaka 1987, Bw. Xibao Ligao alihitimu elimu ya msingi alipokuwa na umri wa miaka 15 na kuamua kubaki nyumbani kufanya kazi za kilimo, na aliamua kupambana na mchanga ili kuokoa maskani yake. Kutokana na nia yake madhubuti, wazazi wake pia walishiriki kwenye shughuli za kupambana na mchanga. Bw. Xibao Ligao alifahamu kuwa, njia mwafaka ya kupambana na mchanga ilikuwa ni kutumia njia za kisayansi, hivyo aliwaomba wataalamu husika wamsaidie kubuni mpango maalum wa kujenga uchumi wa familia kwenye ardhi ya mchanga.

Kujenga uchumi wa familia kwenye mazingira ya ardhi ya mchanga kunatakiwa kuwashirikisha watu wa familia moja au familia kadhaa kushughulikia ardhi ya mchanga, wakati wakifanya shughuli za uzalishaji wa kilimo na ufugaji kwenye eneo moja moja lenye hekta 7 hivi. Kwenye sehemu ya kiini cha eneo la uchumi yenye ukubwa wa hekta 2 ni makazi ya binadamu, shamba la kilimo, shamba la mifugo na eneo la miti. Sehemu hiyo inazalisha chakula, nishati, majani ya mifugo na mbolea kwa ajili ya familia za wakulima. Nje ya sehemu hiyo ni sehemu ya hifadhi ya maumbile, na kwenye sehemu hiyo yenye hekta 5 vimepandwa vichaka na majani ili kuzuia mchanga unaohamahama. Pembezoni mwa sehemu ya hifadhi ya maumbile umejengwa ukanda wa miti unaokinga upepo wenye mchanga. Bw. Xibao Ligao alisema:

"Ili tuweze kujimudu kimaisha tunapaswa kupambana na mchanga. Kila familia ina eneo lake la uchumi, ambapo mara nyingi familia zinakuwa na mifugo ya ng'ombe na kondoo, kulima mahindi na kupanda miti."

Kutokana na kupanuka kwa mradi wa kushughulikia ardhi ya mchanga, ndivyo Bw. Xibao Ligao alivyopanua wazo lake la kujiendeleza. Hivi sasa licha ya kujinufaisha kutokana na ufanisi wa kujiendeleza kwenye ardhi ya mchanga, yeye alianza kusafirisha bidhaa zilizosukwa kwa vipande vya miti ya willow nchini Japan na Korea ya Kusini.

Mbali na hayo, Bw. Xibao Ligao alitangulia kufuata njia ya kuzalisha mazao ya kilimo kwa ajili ya kulisha mifugo, inamaanisha kuwa anatumia magugu kuwalisha mifugo yake. Hivi sasa eneo la familia yake la kujiendeleza kwenye ardhi ya mchanga limepanuka hadi kufikia hekta 87, asilimia zaidi ya 90 ya eneo hilo limefunikwa na mimea, miti na majani, amefuga ng'ombe zaidi ya 300 na kondoo zaidi ya 600. Mkuu wa idara ya misitu ya wilaya ya Naiman ya mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani Bwana Zhang Chunmin alisifu sana njia ya Xibao Ligao ya kujiendeleza.

"Njia hiyo ya kujiendeleza kwa familia kwenye eneo la ardhi ya mchanga kumetambuliwa na serikali ya China na shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, si kama tu ni njia mwafaka ya kuwawezesha wakulima na wafugaji kuondoa umaskini, bali pia ni njia nzuri ya kushughulikia ardhi ya mchanga na kuharakisha ujenzi wa mazingira ya viumbe."

Ofisa husika wa idara ya misitu ya China Bwana Wei Yongxin alifahamisha kuwa, uchunguzi uliotolewa na idara ya misitu ya China unaonesha kuwa, baada ya kujengwa kwa eneo la kujiendeleza kwa familia katika ardhi ya mchanga, eneo lililofunikwa na majani limeongezeka kwa asilimia 70 hadi 80 kutoka lile la asilimia 10 hadi 20 la miaka minne iliyopita, ambapo wastani wa mapato ya wakulima na wafugaji umeongezeka na kufikia Yuan 1,680.

Hivi sasa kujenga eneo la kujiendeleza kwa familia kwenye ardhi ya mchanga kumekuwa ni njia muhimu kwa wakazi wa huko kushughulikia ardhi ya mchanga na kujiendeleza kiuchumi. Hivi sasa katika wilaya ya Naiman ya mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani zimejengwa sehemu zaidi ya 460 za aina hiyo, sehemu iliyokuwa na ardhi ya mchanga hivi sasa imefunikwa na majani.