Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-05 20:06:17    
Mmea unaoweza kuwa tiba ya kudumu ya malaria

cri

Wataalamu wa afya wamekuwa mstari wa mbele kuisaidia serikali ya Tanzania kutafiti vyanzo mbalimbali vya mimea na miti kama hatua ya kutokomeza kabisa tatizo la ugonjwa wa malaria, ambao unaua watu wengi. Mmea wa Artemesia Annua ambao jina lake mama ni Asteraceae, pia hujulikana kwa majina kama Wormwood, Sagewort au Quinghao na umeanza kulimwa kwenye maeneo mbalimbali nchini Tanzania, baada ya utafiti kuonesha kuwa mmea huo umeleta mafanikio makubwa katika nchi mbalimbali duniani.

Mbali ya kutibu malaria wataalamu wa afya wanasema kuwa mmea huo una uwezo wa kutibu magonjwa mbalimbali pamoja na saratani ya matiti na umekuwa ukitumika kama dawa ya kutibu magonjwa hayo kwa zaidi ya miaka 2000 hapa nchini China na nchi nyingine za bara la Asia. Mtaalamu mmoja wa mimea na miti dawa ambaye pia ni daktari wa miti shamba nchini Tanzania Dk. Edwin Stevern Shunda, anasema hapa China dawa inayotoka kwenye mmea huo hujulikana kwa jina la Quinghaosu au Artemisinin kwa lugha ya kitaalamu.

Dawa hiyo ndiyo inayotumika kutengenezea dawa za malaria aina ya Arinate, Cotexcin, Artemether na dawa mseto (ALU) ambazo hutumika kwa kutibu kwa mtindo unaotambulika kitaamu kama Artemisinin Combined Therapies (ACT) pamoja na mchanganyiko wa dawa ya Artemether na Lumefantrine (ALU). Kutokana na mabadiliko mbalimbali `Ugonjwa wa malaria umekuwa sugu kwa kutumia dawa za Chloroquine, SP na nyinginezo. Baada ya tafiti mbalimbali kufanywa, imedhihirishwa kuwa matibabu yanaweza kufanywa kwa ufanisi kwa kutumia dawa mchanganyiko (ACT.

Dk Edwin Shunda amesema pamoja na kutibu malaria, dawa ya Artemesia Annual ina uwezo wa kuongeza kinga ya mwili kwa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi, hivyo kuwafanya wawe na afya nzuri ya kuweza kuepuka kushambuliwa na magonjwa nyemelezi.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limebainisha kwamba mahitaji ya dawa mchanganyiko za kutibu malaria yameongezeka kwa kiasi kikubwa hadi kufikia dozi milioni 30 mwaka 2004 ikilinganishwa na dozi milioni 2 mwaka uliotangulia wa 2003 ambapo watu wengi zaidi walikuwa wakitibiwa kwa dawa zisizo mchanganyiko.

Kwa mfano nchini Tanzania, dozi moja ya kutibu wagonjwa wa malaria hugharimu kati ya dola za Kimarekani milioni 121 ambazo ni zaidi ya Shilingi za Tanzania bilioni 121 kwa mwaka kupambana na kutokomeza malaria.

Akielezea zaidi kuhusu mmea huo, Dk.Shunda alisema mmea huo hulimwa na kustawi katika nchi mbalimbali duniani, na umeingia nchi za Afrika baada ya kuonekana kuleta mafanikio ya tiba ya malaria katika nchi hizo. Katika nchi za Afrika Mashariki, Tanzania inalimwa kwa wingi mmea huo kwenye maeneo yenye mwinuko kama Arusha, Tanga, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Njombe na maeneo ya maziwa hasa Bukoba mkoani Kagera na Musoma mkoani Mara. Utatafiti umeonesha kuwa ubora wa dawa ipatikanayo kwenye artemesia annua inayolimwa Tanzania ni mara kumi kuliko ule wa mmea huo unaolimwa kwenye baadhi ya nchi za Asia.

Utafiti wa masuala wa kisanyansi unaohusiana na aina ya udongo na uzalishaji mazao ya kilimo nao unaonesha kwamba wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, ni sehemu inayoweza kutoa artemisia annua yenye ubora wa hali juu ikilinganishwa na maeneo mengine. Upatikanaji wa mmea huo kwenye nchi za Afrika Mashariki unatokana na ubunifu wa wataalamu wa afya, mimea na miti dawa mingine kutokana na tatizo sugu la ugonjwa wa malaria kuwa tishio kwenye eneo hilo, na kutokana na kuwa matibabu ya malaria kutumia dawa mbalimbali zilizokuwepo kwa muda mrefu umeonekana kutowezekana.

Kutokana na mafanikio hayo shirika la afya duniani WHO, limekuwa mstari wa mbele kuhamasisha ulimaji na uhifadhi endelevu wa artemisia annua kwa ajili ya kukidhi mahitaji. Yote hii ni kusaidia upatikanaji wa malighafi kwa viwanda vya dawa kwa nchi za Afrika badala ya kununua kutoka nje.