Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-09 19:09:06    
Wimbi la kujifunza Kichina lapamba moto nchini Ujerumani

cri

Tarehe 7 Julai shughuli za siku ya China zilifanyika kwenye Chuo cha Confucius Nurnberg-Erlangen nchini Ujerumani, ambapo maonesho ya utamaduni wa China kama vile sanaa ya dansi, maandishi ya Kichina na uchoraji picha kwa mtindo wa Kichina, dawa na tiba za Kichina na vitu vidogo vinavyotengenezwa kwa kutumia mikono, yaliwavutia mamia ya watu wa Ujerumani.

(sauti 1) Mliyosikia ni lugha sanifu ya Kichina. Amini usiamini, watu waliokuwa wanaongea ni Wajerumani ambao walikuwa wanatoa hotuba kwa Kichina, mashindano hayo ya kutoa hotuba yalikuwa shughuli mojawapo ya siku ya China iliyoandaliwa na chuo cha Confucius Nurnberg-Erlangen. Kwenye mashindano hayo yaliyofanyika nchini Ujerumani katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, jopo la wataalamu lilichagua makala 8 zilizoshinda kutoka kwenye makala mamia kadhaa. Makala hizo zilitungwa na Wajerumani kwa lugha ya Kichina, zikieleza mambo mbalimbali waliyoshuhudia waandishi wenyewe walipoitembelea China.

Kuhusu shughuli hizo za siku ya China na mashindano hayo ya kutoa hotuba, mkuu wa chuo hicho kutoka China Bw. Zhang Xuezeng alisema (sauti 2) "Tuliandaa shughuli hizo za siku ya China ili marafiki zetu wa Ujerumani wapate ufahamu mwingi zaidi kuhusu utamaduni wa China na kuvutiwa nao. Tunalenga kuonesha utamaduni wetu na kuhimiza maingiliano kati ya utamaduni wa nchi hizo mbili."

Wimbi la kujifunza Kichina linaendelea kupamba moto nchini Ujerumani. Hivi sasa vyuo vikuu zaidi ya 30 nchini Ujerumani vimeanza kufundisha lugha ya Kichina, na kuwavutia wanafunzi elfu 3. Mbali na hayo, vyuo visivyo rasmi zaidi ya 100 na shule 70 za sekondari nchini Ujerumani zimeanza kufundisha lugha ya Kichina. Kuhusu hali hiyo mkuu wa chuo cha Confucius Nurnberg-Erlangen kutoka upande wa Ujerumani Bw. Michael Schimmelpfennig ambaye pia ni mtaalamu wa taaluma ya Kichina, alieleza maoni yake akisema (sauti 3) "Sababu ya wazi ni kwamba, kutokana na kuongezeka kwa maingiliano ya kiuchumi kati ya Ujerumani na China, Wajerumani wanapata nafasi nyingi zaidi za kuifahamu China. Nchi hizo mbili siku zote zina mawasiliano makubwa katika mambo ya utamaduni. Kwa mfano, hivi sasa Wajerumani wengi wanakwenda China kufanya kazi au kutalii. Sababu nyingine muhimu ni kuwa Wajerumani wana tabia ya kuheshimu lugha kutoka nje ya Ulaya. Baada ya kusoma kwenye chuo cha Confusius, Wajerumani wameona kwamba, si vigumu sana kujifunza Kichina. Kwa uhakika chuo cha Confusius kitatoa mchango katika kuondoa vizuizi vya kijiogrofia vinavyozuia maingiliano kati ya lugha na utamaduni tofauti."

Chuo cha Confusius kimeanzishwa kwa ajili ya kueneza mafunzo ya lugha ya Kichina na utamaduni wa China, na hakina lengo la kupata faida. Chuo cha Confucius Nurnberg-Erlangen kilianzishwa mwezi Mei, mwaka 2006 kutokana na ushirikiano kati ya chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Beijing cha China na chuo kikuu cha Erlangen cha Ujerumani. Mpaka hivi sasa kimewavutia wanafunzi wa Ujerumani zaidi ya 200. Hivi sasa baadhi ya wanafunzi wamepata maendeleo makubwa na kuweza kuongea Kichina sanifu. Kijana Rene Bernard alipata tuzo ya kwanza kwenye mashindano hayo ya hotuba, alieleza kwa nini aliamua kujifunza Kichina. Alisema (sauti 5) "Nafurahia kujifunza Kichina. Mwanzoni nilikumbwa na shida kubwa, lakini sasa hakuna shida tena, kwani nimezoea, hamna tatizo. Awali nilitaka kujifunza lugha moja ya kigeni tu, lakini pia navutiwa na uchumi wa China, kwa hiyo niliamua Kichina iwe taaluma yangu. "

Idhaa ya Kiswahili 2007-07-09