Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-10 14:53:39    
Makampuni binafsi nchini China yawapatia Wachina nafasi nyingi za ajira

cri

Kutokana na maendeleo ya kasi ya makampuni binafsi nchini China, hivi sasa makampuni binafsi yamekuwa nguvu muhimu ya kutoa nafasi za ajira. Kuanzia mwaka 2001 hadi mwaka 2006, makampuni binafsi yamekuwa yanatoa nafasi mpya za ajira milioni 5 hadi milioni 6 kwa mwaka, ambazo zinachukua robo tatu ya nafasi mpya za ajira mijini, hivyo makampuni binafsi yanafuatiliwa na watu wengi zaidi.

Takwimu zinaonesha kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2006, makampuni binafsi nchini China yalifikia zaidi ya milioni 30, ambayo yalikuwa yanatoa kodi zaidi ya yuan bilioni 550 kwa mwaka. Makampuni hayo yametoa nafasi nyingi za ajira kwa jamii ya China, na yamekuwa njia kuu ya kuongeza nafasi za ajira nchini China.

Bibi Li Lanyun anaishi katika mtaa wa Hepin mjini Tianjin. Mwaka 1994 baada ya kupunguzwa kazini alianza kufanya kazi za kutoa huduma na kufanya usafi majumbani, baadaye alianzisha kampuni ya kutoa huduma majumbani. Hivi sasa kampuni hiyo inayoitwa "Lantu" ina mali zisizohamishika zenye thamani ya yuan milioni moja, na inaweza kupata yuan milioni 4 kwa mwaka. Bibi Li Lanyun amekuwa meneja maarufu wa kampuni binafsi mjini Tianjin. Alisema,

"Kampuni yangu ina wafanyakazi zaidi ya mia 6 ambao walipunguzwa kazini. Mimi nimewahi kupunguzwa kazini, ninafanya kazi pamoja nao."

Mafanikio ya Bibi. Li Lanyun yanatokana na sera ya serikali ya China ya kuhimiza maendeleo ya makampuni binafsi. Katika miaka ya hivi karibuni, miji mbalimbali ya China imechukua hatua kadhaa zikiwemo kujenga vituo vya huduma za kutafuta ajira tena, kupunguza au kufuta kodi husika, kutoa dhamana kwa kuomba mikopo midogo ili kuwahimiza na kuwaunga mkono watu wajitafutie ajira na kuanzisha makampuni. China pia imetoa sera za kuhimiza maendeleo ya uchumi binafsi katika matumizi ya ardhi, usajiri wa biashara, upunguzaji wa kodi na mageuzi ya makampuni ya kiserikali. Sera hizo zinawaunga mkono kihalisi watu wanaoanzisha makampuni binafsi kama Bibi Li Lanyun, pia zimeinua kiwango cha maisha ya watu wanaofanya kazi katika makampuni binafsi.

Licha ya kuyaunga mkono kisera moja kwa moja makampuni binafsi, China pia imeanzisha shughuli mbalimbali za kuyasaidia makampuni binafsi kuwaajiri watu wenye ujuzi. Katika siku za karibuni, mkutano wa 3 wa "wiki ya ajira kwenye makampuni binafsi nchini kote" ulioandaliwa na idara za serikali za China na mashirika ya kijamii, ulifanyika katika sehemu mbalimbali nchini China. Mjini Tianjin makampuni binafsi zaidi ya elfu 1 yalishiriki kwenye mkutano wa ajira bila ya malipo. Bibi Liu anayeshughulikia ajira katika kampuni ya kemikali ya makaa ya mawe ya Jun'an ya Tianjin alimwambia mwandishi wa habari kuwa, mkutano huo unawasaidia watu wengi zaidi kuyafahamu makampuni binafsi na kufanya kazi katika makampuni hayo, na kuhimiza ongezeko la nafasi za ajira, alisema,

"Makampuni binafsi yanafurahia njia hiyo ya kuwaajiri wafanyakazi, yanaweza kukutana na watu wengi wanaotafuta ajira, hivyo inayasaidia kupunguza muda wa kufanya kazi za ajira."

Maendeleo ya haraka ya makampuni binafsi yamewavutia watu wengi wenye ujuzi wakiwemo wanafunzi waliohitimu kutoka vyuo vikuu na hata watu waliosoma katika vyuo vikuu vya nchi za nje. Wanafunzi wengi waliohitimu kutoka vyuo vikuu walishiriki kwenye mkutano wa 3 wa "wiki ya ajira katika makampuni binafsi nchini kote". Bw. Zhu Chenglin mwenye shahada ya kwanza ambaye alikuja Tianjin kutoka mji wa Guangzhou anaona kuwa atapata fursa nzuri zaidi ya kujiendeleza kwenye makampuni binafsi, alisema,

"Kuna fursa nyingi zaidi za maendeleo kwenye makampuni binafsi, hivyo nikifanya kazi kwenye kampuni binafsi itanichukua muda mfupi kujiendeleza."

Makampuni binafasi yametoa matakwa kwa watu wanaotafuta kazi. Kwenye mkutano wa 3 wa "wiki ya ajira kwenye makampuni binafsi nchini kote" uliofanyika mjini Tianjin, Bi Quan kutoka kampuni ya vifaa vya kulehemu ya Jinqiao ya mji wa Tianjin alisema,

"Watu zaidi ya mia 1 wametoa maombi ya kufanya kazi katika kampuni yetu, tumepanga kuwaajiri watu thelathini hadi hamsini. Tunazingatia zaidi uwezo wa wafanyakazi, kwenye msingi huo kama wanathamini kazi zao, na wana hamu ya kufanya kazi, tunaamini kuwa watafanya kazi vizuri."

  

Habari zinasema mwaka 2006 wanafunzi zaidi ya milioni 1.2 waliohitimu kutoka vyuo vikuu bado hawajapata ajira, kwa ujumla mwaka huu idadi ya wanafunzi wanaotafuta ajira itakuwa zaidi ya milioni 6. Katika hali hiyo, maendeleo ya makampuni binafsi yatapunguza shinikizo la ajira kwa kiasi fulani. Naibu mwenyekiti wa shirikisho la wanaviwanda na wafanyabiashara wa China Bw. Chu Ping anaona kuwa, kuwaajiri watu wenye ufundi wa ujuzi kutasaidia kuongeza nguvu ya makampuni binafsi, pia kutawasaidia wanafunzi wengi waliohitimu kutoka vyuo vikuu kupata ajira, alisema,

"Wanafunzi waliohitimu kutoka vyuo vikuu wanasaidia kuinua uwezo wa makampuni binafsi, na makampuni binafsi yanaweza kutoa nafasi nyingi za ajira kwa wanafunzi hao."

Bw. Chu pia alisema shirikisho la wanaviwanda na wafanyabiashara wa China litawaongoza mameneja wengi zaidi wa makampuni binafsi kueleza maendeleo ya makampuni yao kwenye vyuo vikuu ili kuwahimiza wanafunzi wengi zaidi kutafuta kazi katika makampuni hayo.

Idara husika inakaridia kuwa katika mwaka 2007 shinikizo la ajira bado ni kubwa, na kutakuwa na nafasi milioni 15 za ajira nchini China. Makampuni binafsi yatatoa mchango mkubwa katika kutoa nafasi za ajira.