Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-10 15:15:33    
Barua 0708

cri
Leo kwanza tunawaletea habari kuhusu matokeo ya tuzo maalum ya mashndano ya chemsha bongo kuhusu ujuzi wa "Mkoa wa Sichuan, maskani ya Panda".

Mkutano wa kutangaza tuzo maalum ya mashindano ya chemsha bongo kuhusu ujuzi wa "Mkoa wa Sichuan, maskani ya Panda" umefanyika tarehe 4 hapa Beijing, ambapo washindi 10 waliochaguliwa kutoka miongoni mwa wasikilizaji wa Radio China Kimataifa wa nchi za Marekani, India, Mongolia, Vietnam, Ujerumani, Italia, Morocco, Iran, Russia na Romania wamepewa tuzo maalum na naibu mwenyekiti wa Baraza la mashauriano ya kisiasa la China Bwana Luo Haocai.

Habari zinasema tarehe 6 Julai washindi hao 10 watakwenda mkoa wa Sichuan kufanya matembezi ya wiki moja.

Na matokeo ya tuzo ya nafasi ya kwanza, pili na tatu ya wasikilizaji wetu yatajulikana hivi karibuni kwenye kipindi hiki cha sanduku la barua.

*********

Msikilizaji wetu Bw. Ali Hamisi Kimani wa sanduku la posta 34 Ndori Kenya, anaanza barua yake kwa salamu kwa watangazaji na wasikilizaji wenzake. Yeye na familia yake anasema ni wazima na matumaini makubwa kuwa hatujambo na tunaendelea kuchapa kazi barabara. Anasema lengo hasa la barua yake ni kutujulisha kuwa anaendelea kufurahia matangazo na vipindi vyetu kila siku, na hivyo imembidi kununua radio ndogo ya mfukoni ili asikose uhondo wa matangazo ya Radio China kimataifa. Pia anatuambia kuwa amepokea kwa mikono miwili picha mbili nzuri za viwanja ambavyo michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 itafanyika hapa Beijing.

Anasema ama kweli ufundi uliotumika kwenye viwanja hivyo ni wa hali ya juu na anaulinganisha na ule uliotumika katika uwanja wao wa Kasarani ambao ulijengwa na wachina. Anasema kwa kweli picha tulizomtumia zimemfanya apate hamu ya kutembelea nchi ya China. Hivyo basi anasema, ni kwanini tusitoe chemsha bongo maalumu kuhusu michezo ya Olimpiki ili waweze kuwania nafasi maalumu ya kuja China ili kushuhudia ujenzi huo wa ajabu mbali na michezo ya Olimpiki. Anamaliza barua yake kwa kushukuru kwa kadi za salamu na bahasha zilizolipiwa tunazomtumia mara kwa mara.

Tunamshukuru sana Ali Hamisi Kimani kwa barua yake ya kutuelezea usikivu wake wa matangazo yetu ambao unatutia moyo kuchapa kazi zaidi ili kuandaa vizuri zaidi vipindi vyetu vya kupendwa na wasikilizaji wetu. Na maoni na mapendekezo yake ni mazuri, tutayawasilisha kwa ofisi husika, ni matumani yetu kuwa mawasiliano na urafiki kati yetu utadumishwa.

Msikilizaji wetu mwingine ambaye ametutumia barua ni Jackline Andeyo Savala wa sanduku la posta 64 Mautuma Lugari, Kenya. Naye ameanza kwa kutusalimu, na kutoka shukurani kwa yote tunayofanya kuhakikisha kuwa matangazo yetu yanawafikia wasikilizaji wetu, na anaomba tuendelee hivyo hivyo bila kurudi nyuma wala kukata tamaa.

Mbali na hayo anasema wasikilizaji wenzake huko Mautuma wanaendelea kuyaunga mkono matangazo yetu, na wanaomba tusivunjike moyo na mungu awe pamoja nasi katika kuendeleza matangazo haya. Pia anatuambia kuwa wasikilizaji wenzake wanaomba tuwatumie kadi ili waweze kutuma maoni yao na salamu zao kwa wasikilizaji wengine.

Lakini pia anasema kuna tatizo upande wake, anashangaa ni kwanini barua anazotutumia zinachukua muda sana kusomwa na haelewi ni kwa nini. Hata hivyo anasema hatakata tamaa, hata kama barua hizo zikichelewa kusomwa, kwa sababu wahenga hawakukosea waliposema mtu anayetanga sana na jua mwisho hujua. Anatoa shukurani kwa matangazo ambayo yalianza kusikika tarehe 27 Aprili.

Anatuambia kuwa huko Mautuma wana furaha kubwa na isiyo kifani, na wana matumaini makubwa ya kujifunza kichina kweli kweli. Na anapenda kutoa salamu kwa watu wafuatao:- Ayub Mutanda ? Bungoma, Violet Ajema ? Luandeti, Mbaruku Msabaha ? Dubai Falme za kiarabu, Raymond Sirengo ? Bungoma, Daisy Maliaka ? Makutano, Goldah Jendeka ? Bungoma, Japhetha Martiuas ? Mlimani, Humphrey Adhiambo ? Eldoret.

Tunamshukuru Jackline Andeyo Savala kwa barua yake ya kutuambia kwamba wasikilizaji wengi wana hamu ya kujifunza Kichina. Hivi karibuni Darasa la Confucius limezinduliwa rasmi huko Nairobi Kenya, na hivi sasa tunafanya maandalizi ya masomo mapya ya kujifunza Kichina, tunawakaribisha wasikilizaji wetu wasikilize kwa makini matanazo yetu. Na kuhusu barua alitutumia huchelewa kusomwa kwenye kipindi chetu, tunaona ni kutokana na tatizo la posta, kwani kila mara tulichelewa kupata barua za wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu huyo huyo Jackline Andeyo Savala pia ametuletea shairi linaloitwa "Lipi la kuwapa wachina iwe fidia yao". Anasema katika shairi lake kuwa

Ndugu zangu waadhama, leo nawauliza

Wakenya na Wachina wote mpate sikia

Wazima hata vilema, rai zenu nanuia

Kipi cha kuwapa wachina, iwe yao fidia?

Katika miaka mingi, kipindi kuanza

Kwa uwezo wa ukarimu, kipindi kikaendelea

Ni kidogo sijasema, kuenea kote duniani

Kipi cha kuwapa wachina, iwe yao fidia?

Kudharau nilidharau, kipindi kikaendelea

Ilipofika saa, nawasha redio haraka

Nawashukuru walioniamsha, kutoka usingizini

Kipi cha kuwapa wachina, iwe yao fidia?

Japo mwanzo nilidharau, hakikuniridhisha kamwe

Mafunzo mengi nikapata, na mengi kuhusu China

Chanipa mengi maarifa, ni nini nitawalipia?

Kipi cha kuwapa wachina, iwe yao fidia?

Niwape darahimu, naona sijatimia

Maoni na nyingi shukurani, sioni kama fidia

Zawadi zote kupima, yakuwapa sijajua

Kipi cha kuwapa wachina, iwe yao fidia?

Kwa mpangilio mwema, na utangazaji bila shida

Kwa heshima yao njema, kwaheri nawapungia

Naondoka hima, swali langu naacha

Kipi cha kuwapa wachina, iwe yao fidia?

Idhaa ya kiswahili 2007-07-10