Bodi ya wakurugenzi ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki tarehe 9 ilifanya mkutano na kuidhinisha pendekezo lililotolewa tarehe 3 na mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Bw. Mohamed el-Baradei. Kwa mujibu wa pendekezo hilo shirika hilo litatuma tena kundi la wakaguzi wa nyukilia kwenda nchini Korea ya Kaskazini ili kuhakikisha zana za nyukilia zilizopo Yongbyon zinafungwa.
Baada ya mkutano, Bw. Baradei alisema anafurahishwa na mwenendo wa mchakato wa ukaguzi wa zana za nyuklia. Alisema, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki limefikia makubaliano na Korea ya Kaskazini kuhusu kufunga zana nne za nyukilia huko Yongbyon na mpango wa kufunga zana za nyukilia za Korea ya Kaskazini umeanza kutekelezwa rasmi. Kutokana na kuwa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki linaweza tu kutuma kundi la wakaguzi baada ya kupata mwaliko kutoka Korea ya Kaskazini, kwa hiyo tarehe ya kuondoka kwa kundi hilo bado haifahamiki. Bw. Baradei alisema anatumai kuwa kundi hilo litaweza kwenda huko ndani ya wiki moja au mbili. Kwa mujibu wa shirika la habari la Korea ya Kaskazini, kundi lenye watu wanane litakwenda kati ya tarehe 14 hadi 17.
Suala la nyukilia la peninsula ya Korea lilianza mwanzoni mwa miaka 90 ya karne iliyopita. Wakati huo kwa mujibu wa uchunguzi wa setilaiti, Marekani ilishutumu Korea ya Kaskazini kuendeleza silaha za nyukilia, lakini Korea ya Kaskazini ilisema haina uwezo wa kuendeleza silaha hizo, mgogoro wa nyukilia wa peninsula ya Korea ukaanza. Mwaka 2003 Korea ya Kaskazini ilitangaza kujiondoa kutoka "Mkataba wa Kutoeneza Silaha za Nyukilia", suala la peninsula ya Korea likawa linazingatiwa sana duniani. Tarehe 13 Februari mwaka huu "waraka wa pamoja wa utekelezaji wa taarifa ya pamoja" uliopitishwa kwenye duru la tano la mazungumzo ya pande sita umekuwa kumbukumbu muhimu ya kihistoria. Waraka huo wa tarehe 13 Februari umeweka ratiba ya utekelezaji wa taarifa ya pamoja. Kwenye waraka huo, Korea ya Kaskazini iliahidi kufunga zana za nyukilia za huko Yongbyon na kuwaalika wakaguzi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki kwenda Korea ya Kaskazini, na pande nyingine zitatoa misaada ya kiuchumi, kinishati na kibinadamu.
Naibu mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki Bw. Olli Heinonen tokea tarehe 26 Juni hadi 30 alipokuwa ziarani nchini Korea ya Kaskazini, Korea ya Kaskazini iliahidi kutekeleza ahadi zake kwenye waraka wa tarehe 13 Februari zikiwa ni pamoja na kufunga zana za nyukilia na kuruhusu wakaguzi kuwepo kwenye ufungaji wa vifaa vya kudhibiti na kuangalia shughuli za zana. Katika hali hiyo, tarehe 3 mwezi huu Bw. Baradei aliwasilisha ripoti yake kwenye bodi ya wakurugenzi ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki na kuufurahia ushirikiano unaotolewa na Korea ya Kaskazini.
Baadhi ya wachambuzi wanaona kuwa hivi sasa suala la nyuklia la peninsula ya Korea ya Kaskazini linaelekea kwenye utatuzi. Kwa kutumia fursa ya kusaini waraka wa tarehe 13 Februari, Korea ya Kaskzini inajaribu kuboresha uhusiano kati yake na Korea ya Kusini, Marekani na Japan. Mwezi Machi Korea ya Kaskazini ilifanya mazungumzo na nchi hizo tatu na kujadili suala la kuanzisha uhusiano wa kawaida, na mazungumzo kati ya naibu waziri wa mambo ya nje wa Korea ya Kaskazini na msaidizi wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani yalichukuliwa kama ni hatua ya kwanza kuelekea kwenye uhusiano wa kawaida. Bw. Baradei anaona kuwa mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Marekani na Korea ya Kaskazini ni sababu muhimu ya kupata maendeleo katika suala la nyukilia la peninsula ya Korea.
Pamoja na hayo, wachambuzi wengine wanaona kuwa mchakato wa kutokuwa na silaha za nyukilia katika peninsula umekwisha haribiwa, suala la nyukilia la peninsula ya Korea ni suala hasa la kueneza silaha za nyukilia, utatuzi wa suala hilo ni "kuacha silaha za nyukilia ili kupata usalama", lakini kwenye waraka wa tarehe 13 Februari yamewekwa masharti mengi, na si rahisi hata kidogo kutekeleza masharti yote. Kwa hiyo, mchakato wa kutokuwepo kwa silaha za nyukilia katika peninsula ya Korea utakuwa na safari ndefu.
Idhaa ya kiswahili 2007-07-10
|