Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-11 15:04:38    
Mmea unaoweza kuwa tiba ya kudumu ya malaria

cri

Wataalamu wa afya nchini Tanzania wamekuwa mstari wa mbele kuisaidia serikali kutafiti vyanzo mbalimbali vya mimea na miti inayoweza kuwa dawa, kama hatua ya kutokomeza kabisa tatizo la malaria ambalo linasababisha vifo kwa watu wengi. Mmea wa Artemesia Annua ambao jina lake mama ni Asteraceae pia unajulikana kwa majina kama Wormwood, Sagewort au Qinghao na umeanza kulimwa kwenye baadhi ya maeneo nchini Tanzania, baada ya utafiti kuonesha kwamba umeleta mafanikio makubwa katika nchi mbalimbali duniani. Mbali na kutibu malaria, wataalamu wa afya wanasema kuwa mmea huo una uwezo wa kutibu magonjwa mbalimbali pamoja na saratani ya matiti na umekuwa ukitumika kama dawa ya kutibu magonjwa hayo kwa zaidi ya miaka 2000 nchini China, na kwenye nchi nyingine za bara la Asia.

Mtaalamu mmoja wa mimea na miti dawa ambaye pia ni tabibu wa mitishamba nchini Tanzania na mwanachama wa Shirika la Kijerumani la dawa za asili linalojulikana kama Action for Natural Medicine (ANAMED) Dk. Edwin Stevern Shunda anasema dawa inayotoka kwenye mmea huo hujulikana nchini China kwa jina la Qinghaosu au Artemisinin kwa kitaalamu .

Dawa hiyo ndiyo inayotumika kutengenezea dawa za malaria aina ya Arinate, Cotexcin, Artemether na dawa mseto (ALU) ambazo hutumika kutibu kwa mtindo unaotambulika kitaaluma kama Artemisinin Combined Therapies (ACT) pamoja na mchanganyiko wa dawa ya Artemether na Lumefantrine (ALU).

Ugonjwa wa malaria umekuwa sugu kwa kutumia dawa za Chloroquine, SP na nyinginezo, na baada ya tafiti mbalimbali kufanywa, imedhihirishwa kwamba matibabu yanaweza kufanywa kwa ufanisi kwa kutumia dawa mchangayiko (ACT).

Mtaalamu huyo anasema pamoja na kutibu malaria, dawa ya Artemesia Annual ina uwezo wa kuongeza kinga ya mwili kwa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi, hivyo kuwafanya wawe na afya nzuri ya kuweza kuepuka kushambuliwa na magonjwa nyemelezi.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limebainisha kwamba mahitaji ya dawa mchanganyiko za kutibu malaria yameongezeka kwa kiasi kikubwa. Akielezea kuhusu mmea huo, Dk. Shunda anasema hulimwa na kustawi katika nchi mbalimbali duniani, na umeingia kwenye nchi za Afrika baada ya kuonekana kuleta mafanikio ya tiba ya malaria katika nchi hizo.

Katika nchi za Afrika Mashariki, Tanzania inaongoza katika kulima Artemisia Annua kwa kiwango kikubwa ambapo hulimwa kwenye maeneo yenye mwinuko kama vile Arusha, Tanga, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Njombe na maeneo ya maziwa hasa Bukoba mkoani Kagera na Musoma mkoani Mara. Utafiti umeonesha kwamba ubora wa dawa ipatikanayo kwenye artemesia annua inayolimwa nchini Tanzania, ni mara 10 hadi 15 ikilinganishwa na ile inayolimwa nchini China na Thailand.

Utafiti wa masuala wa kisanyansi unaohusiana na aina ya udongo na uzalishaji mazao ya kilimo unaonesha kwamba wilaya ya Lushoto mkoani Tanga ni sehemu inayoweza kutoa artemisia annua yenye ubora wa hali juu ikilinganishwa na maeneo mengine.

Upatikanaji wa mmea huo nchini Tanzania unatokana na ubunifu wa wataalamu wa afya, mimea na miti dawa mingine kutokana na tatizo sugu la ugonjwa wa malaria kuwa tishio nchini humo na matibabu yake kutumia dawa mbalimbali na kuonekana sugu katika matibabu.

Dk. Shunda pia aliongeza kusema kuwa mahitaji ya dawa ya artemisinin itokanayo na mmea huo yameongezeka mara dufu kiasi kwamba kiwango kinachopatikana hakiwezi kukidhi mahitaji.

Kutokana na sababu hiyo WHO imekuwa mstari wa mbele kuhamasisha ulimaji na uhifadhi endelevu wa artemisia annua ili kuweza kukidhi mahitaji. Yote hii ni kwa lengo la kusaidia upatikanaji wa malighafi kwa viwanda vya ndani badala ya kununua kutoka nje ya nchi.

Ugonjwa wa malaria umekuwa tishio kwa jamii nchini Tanzania ambako watu wanaokadiriwa kufikia 100,000 hufa kila mwaka kwa ugonjwa wa malaria, wengi wao wakiwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano. Watafiti na wadau mbalimbali nchini Tanzania kwa kushirikiana na serikali ya nchi hiyo wamekuwa wakifanya njia mbalimbali zitakazowezesha upatikanaji wa dawa za kutibu malaria na magonjwa mbalimbali na kupatikana kwa kiasi cha kutosha, na kwa gharama nafuu ambayo wananchi wa kawaida wataweza kumudu.

Juhudi hizo zimewezesha kutengenezwa kwa dawa ya malaria aina ya malather inayotokana na mmea wa Artemisia annua viwanda viwili vya dawa vya Tanzania, ambayo bei yake ni nafuu ikilinganishwa na dawa zile zinazotengezwa nje ya nchi hiyo.

Wananchi wa Tanzania wakihamasishwa na kuelimishwa vya kutosha wanaweza kulima mmea huo kwa wingi na hivyo kuifanya Tanzania kuwa muuzaji mkubwa wa Artemisia annua nchi za nje na hivyo kuchangia kukuza uchumi wa Taifa.

Dk. Shunda pia alisema mwananchi ataweza kujikwamua kiuchumi kwa kujiongezea kipato baada ya kuuza majani ya mmea wenyewe, hasa wale wa mikoa ambayo mmea huo unastawi vizuri kama Arusha na Iringa ambao wameanza kulima siku nyingi kama zao la biashara na muhimu katika kuwapatia kipato.

Anasema viwanda vya dawa ya malaria nchini Tanzania, hulazimika kupata malighafi ya artemisininn kutoka nje ya nchi baada ya majani yanayovunwa ya Artemisia annua kusafirishwa kwenda nje ambapo dawa hiyo ya artemisinin husindikwa. Anasema endapo jamii itahamasishwa na kuwezeshwa kulima mmea huo kwa wingi, na mkakati endelevu ikafanywa ili kujenga viwanda vya dawa asilia vitakavyosindika dawa ghafi ya artemisia annua ili kupata dawa ya artemisinin, ni wazi kwamba Tanzania itakuwa na uwezo wa kutengeneza dawa za malaria kutokana na mmea huo, ambazo zitaweza kuuzwa kwa bei ya chini itakayowezesha mwananchi wa chini kumudu.

Pia taifa litaweza kuuza nje malighafi ya dawa ya artemisinin kwa bei ya juu na ubora ulioongezeka (added value) badala ya kuuza majani ya artemesia annua kwa bei ya chini. Hadi sasa mahitaji ya artemisinin kwenye soko la dunia bado hayajatosheleza hivyo, Tanzania na nchi nyingine zinazozalisha majani hayo, zinaweza kuwa miongoni mwa wauzaji wakubwa wa malighafi hiyo muhimu kwa ajili ya kutengenezea dawa za malaria.

Mtaalamu huyo pia alisema utafiti unaendelea kufanywa ili kupatikana mbegu za artemesia annua zitakazowezesha kupatikana kwa artemisinin yenye ubora zaidi wa kuweza kufikia kiwango cha asilimia 1.5 na zaidi.