Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-11 15:36:39    
Tukio lililotokea kwenye Msikiti Mwekundu nchini Pakistan lakaribia kumalizika

cri

Msemaji wa jeshi la Pakistan Bw. Waheed Arshad tarehe 10 alisema, katika siku hiyo jeshi la Pakistan lilichukua hatua na limedhibiti sehemu nyingi za Msikiti Mwekundu, kiongozi wa pili wa msikiti huo Bw. Abdul Rasheed Ghazi aliuawa kwa kupigwa risasi. Wachambuzi wanaona kuwa tukio ambalo lilianza tokea tarehe 3 katika Msikiti Mwekundu, limekaribia kumalizika.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jioni ya siku hiyo Bw. Waheed Arshad alisema, siku hiyo alfajiri saa kumi na nusu jeshi la serikali lilianza kuchukua hatua na hadi sasa limedhibiti sehemu karibu zote za msikiti huo na shule zilizo chini ya uongozi wa msikiti huo. Aliongeza kuwa jeshi la serikali liliwaua kwa kuwapiga risasi watu wenye silaha zaidi ya 50, na askari wanane wa jeshi la serikali waliuawa, wengine 29 kujeruhiwa katika mapambano hayo. Pamoja na hayo, watu wenye silaha 50 walisalim amri, na wakati wa mapambano wanafunzi wasiopungua 26 walikimbia kutoka katika msikiti huo. Bw. Waheed Arshad alisisitiza kuwa jeshi la Pakistan lilikuwa na subira kadiri liwezavyo, na lilifanya juhudi nyingi ili kukwepa kuwadhuru watu wasio na hatia. Hakuna habari yoyote inayoeleza kama kuna wanawake na watoto waliouawa au kujeruhiwa katika mapambano ya siku hiyo.

Tokea tarehe 4 mwezi huu serikali ya Pakistan ilipoamua kuchukua hatua dhidi ya tukio la msikiti huo, kutokana na shinikizo kubwa la "taarifa ya mwisho" ya jeshi la Pakistan viongozi na wanafunzi wengi walitoka msikitini na shuleni na kujisalimisha kwa serikali, hali ikawa ikielekea kuwa ya amani. Lakini baadaye watu wenye siasa kali walioongozwa na kiongozi wa pili wa msikiti huo Bw. Abdul Rasheed Ghanzi waliwateka nyara wanawake na watoto, na operesheni ya jeshi la Pakistan ikalazimika kusimama. Kadiri muda ulivyokuwa unaendelea, watu wa sekta mbalimbali wa Pakistan walishikwa na wasiwasi kuhusu hali ya mateka na vurugu za jamii, wakitaka msikiti uwaachie huru na serikali itatue tatizo hilo haraka kwa njia ya amani.

Kutokana na idhini ya rais Pervez Musharraf mwenyekiti wa chama tawala Bw.Chaudhary Shujaat Hussain pamoja na mawaziri kadhaa na wasomi wa kidini wa Pakistan tarehe 9 walifanya mazungumzo na viongozi wa msikiti huo kwa muda wa saa 11 wakiwa na lengo la kutatua tukio hilo kwa amani, lakini hawakufanikiwa. Baada ya mazungumzo kuvunjika, jeshi la Pakistan lililazimika kuushambulia msikiti huo kwa pande zote.

Kwa muda mrefu mambo yanayohusu wanawake na mambo ya kidini yanachukuliwa kuwa kama ni masuala nyeti nchini Pakistan. Ili kukwepa kuwadhuru watu wasio na hatia, serikali ya Musharraf ilionekana kuwa na subira isiyo ya kawaida. Watu wanaelewa kwamba ingawa mwishowe serikali ya Pakistan ililazimika kuchukua hatua za kijeshi lakini serikali hiyo toka mwanzo ilifuata kanuni ya kuwalinda raia wasio na hatia kadiri iwezavyo, kwa hiyo haikutokea hali ya watu wengi kuuawa na kujeruhiwa. Msimamo wa uvumilivu na subira uliochukuliwa na serikali ya Pakistan unaungwa mkono na watu wa Pakistan.

Idhaa ya kiswahili 2007-007-11