Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-12 15:02:55    
Wakulima wanufaika na maendeleo ya viwanda

cri

Uzalishaji wa kilimo ni mhimili wa uchumi wa mkoa wa Anhui, uliopo katikati ya China, ambapo asilimia 70 ya watu wa mkoa huo wanaishi vijijini na kilimo kinachukua nusu ya uzalishaji wa uchumi wa mkoa huo. Hata hivyo katika miaka ya hivi karibuni, viwanda vya kutengeneza viatu na nguo vilianza kukua kwenye sehemu za vijijini mkoani Anhui, ambapo wakulima wengi walianza kufanya kazi viwandani, jambo ambalo linawafanya wawe na mapato ya uhakika na muda mwingi zaidi wa kupata burudani.

Mwandishi wetu wa habari alitembelea familia moja ya wakulima katika kata iitwayo Suncun. Familia hiyo ina nyumba moja yenye ghorofa ambayo ina samani na zana mbalimbali za umeme. Kwenye ghorofa ya kwanza, kuna jiko, msala, sebule na vyumba viwili vya kulala, na kwenye ghorofa ya pili kuna vyumba vingine vitatu vikubwa vya kulala.

Wenye nyumba ni Bw. Jiang Tongming mwenye umri wa miaka 59 na mke wake, wanaishi pamoja na binti mdogo na mume wa binti huyo. Bw. Jiang alisema wanapanda mpunga kwenye shamba lenye eneo la hekta 0.2 na kupata mavuno ya kilo zaidi ya elfu moja kwa mwaka. Mbali na hayo wanafuga kuku kadhaa na nguruwe mmoja. Kutokana na makadirio, familia hiyo inaweza tu kujitosheleza chakula kwa kutegemea uzalishaji wa kilimo, lakini iliwezaje kupata pesa za kujenga nyumba kubwa ya ghorofa?

Mwenye nyumba Bw. Jiang Tongming alijibu swali hilo, akisema "Nyumba hiyo ilijengwa mwaka 2004, tulitumia pesa zote za akiba. Lakini binti yangu na mkwe wangu wanafanya kazi viwandani, hivyo tunaweza kuanza tena kuweka akiba."

Zamani neno ajira lilikuwa neno geni kwa wakulima, lakini hivi sasa huko wilayani Fanchang, mkoani Anhui, si jambo la ajabu kwa wakulima kupata ajira viwandani. Kwenye kata ya Sunchun anakoishi Bw. Jiang Tongming na familia yake, kuna viwanda zaidi ya 270 vya kutengeneza nguo, ambavyo vinatoa nafasi za ajira karibu elfu 20 kwa sehemu hiyo yenye watu wasiozidi elfu 60. Ndiyo maana sasa kilimo si njia pekee ya kupata pesa kwa wakulima wa huko.

Bibi Zhang Chunxia mwenye umri wa miaka 51 alimwambia mwandishi wa habari kuwa, binti yake anafanya kazi katika kiwanda cha nguo na mkwe pia ameajiriwa na kiwanda kingine katika kata hiyo, wao wawili wana mapato karibu Yuan elfu 30 kwa mwaka, kiasi ambacho ni sawa na dola za kimarekani elfu 4.

Mama huyo anasema "Nyumbani kwangu, nina sufuria ya umeme ya kupikia wali, pia kuna gesi. Napika wali kwa kutumia umeme, ni rahisi zaidi kuliko siku zilizopita ambapo tulitumia kuni. Mapato yameongezeka, sasa maisha ni mazuri mara 100 zadili kuliko zamani."

Lakini wakulima ni hodari katika shughuli za kilimo mashambani, je wanaweza kuzoea kazi za viwandani? Je, viwanda vinawalipa vipi wakulima hao?

Pamoja na maswali hayo, mwandishi wetu wa habari alitembelea kampuni ya kutengeneza nguo inayoitwa Shunda, iliyoko kwenye wilaya ya Fanchang. Mkurugenzi wa kiwanda hicho Bw. Wu Aijun alieleza kuwa, wafanyakazi wengi wa kiwanda hicho ni wakulima wa huko, kampuni hiyo inawapa mafunzo na kuwalipa vizuri.

Anasema  "Wao ni wanavijiji wa hapa hapa au kutoka sehemu za karibu. Hapa tuna wafanyakazi zaidi ya 100, tunasaini mikataba ya ajira na wafanyakazi hao, kuwaandalia utalii kila wakati wa sikukuu, na tunajadili hatua ya kuwaingiza wafanyakazi ambao wamefanya kazi hapa kiwandani kwa miaka kadhaa kwenye bima ya matunzo ya uzeeni."

Katika karakana pana ya kiwanda hicho, wafanyakazi wanawake wanatumia kwa ustadi cherehani. Dada Wu Lian anaishi hapa kijijini, alieleza kufurahia kupata ajira kiwandani. Anasema  "Kazi yangu ni kutengeneza nguo za mfano. Mshahara wangu ni kati ya Yuan 1,400 na 1,500 kwa mwezi, naridhika sana. Sasa ninaishi kwenye mabweni ya kiwanda, yana mazingira mazuri, naweza kupata mshahara kwa wakati kila mwezi. Na kila mwaka tunakwenda kutalii, mwaka huu tulitembelea Suzhou."

Dada huyo pia alimwambia mwandishi wa habari kuwa, hivi sasa huko Fanchang, watu wa vizazi vitatu kutoka familia nyingi za wakulima wanafanya kazi viwandani, wana mapato ya uhakika zaidi kuliko walipojishughulisha na kilimo au ufugaji. Zaidi ya hayo wana nafasi nyingi zaidi za kujiburudisha.

Katika kijiji cha Jiulian, huko Fanchang, wakulima walianzisha makundi mawili ya wanamitindo, wakifanya mashindano ya kuonesha nguo kila baada ya kipindi fulani, na nguo nyingi walizoonesha zinatoka kwenye viwanda wanakofanya kazi. Wanajivunia kwa kuvaa nguo walizotengeneza wenyewe.

Suala la matibabu ni suala linalowakabili wakulima wengi. Zamani wakulima wa wilaya ya Fanchang walihofia kuugua, wakiumwa hawakuthubutu kwenda hospitali kutokana na gharama kubwa za matibabu. Hivi sasa utaratibu wa matibabu ya ushirikiano umeanzishwa hapa vijijini, kila mkulima anachangia Yuan 10 tu kwa mwaka, anaweza kulipiwa kiasi fulani cha gharama za matibabu. Mama Zhang Chunxia alisema "Mwezi Agosti na Septemba mwaka jana, nilifanyiwa upasuaji wa kuondoa kidole tumbo nilitumia Yuan elfu 3 na 4 hivi. Nililipiwa Yuan zaidi ya elfu moja, nilipata pesa hizo mara baada ya kutoka hospitali."

Kuinuka kwa kiwango cha maisha pia kunabadilisha mtizamo wa wakulima hao. Zamani walifurahia kuzaa watoto wa kiume ili kuongeza nguvu kazi, ndiyo maana wanandoa wengi waliozaa watoto wa kike walikuwa wakifanya chini juu kuzaa watoto wa kiume. Lakini hivi sasa maendeleo ya uchumi na kukamilika kwa mfumo wa huduma za jamii kunawaondolea wasiwasi kuhusu matunzo ya uzeeni. Wakulima hao wameanza kuacha mtizamo wa mfumo dume. Kiongozi wa kata ya Suncun, Bw. Chen Cesen alisema  "Mume anapotimiza umri wa miaka 60 na mke akiwa na umri wa miaka 55, serikali ya kata inampa kila mmoja Yuan 60 kwa mwezi. Sasa wazee wanatunzwa vizuri, kwa hiyo wanakijiji vijana wa umri wa miaka 30 hivi wanaona kuzaa watoto wa kike au wa kiume hakuna tofauti kubwa."

Idhaa ya kiswahili 2007-07-12