Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-12 15:21:39    
Mahakama kuu ya Libya inaunga mkono hukumu ya awali ya kesi ya kueneza UKIMWI mjini Benghazi

cri

Tarehe 11 mahakama kuu ya Libya ilitangaza kuunga mkono hukumu ya awali ya kifo kuhusu kesi ya wauguzi watano na daktari mmoja wa Palestina ambaye sasa ni raia wa Bulgaria, kueneza virusi vya UKIMWI miaka minane iliyopita katika mji wa Benghazi nchini Libya.

Kesi hiyo ilitokea mwishoni mwa miaka tisini ya karne iliyopita katika hospitali ya watoto mjini Benghazi, watoto 438 waliambukizwa virusi vya UKIMWI katika hospitali hiyo, na kati yao watoto 56 wamekufa. Wakati huo wauguzi watano wa kike kutoka Bulgaria na daktari mmoja wa Palestina walituhumiwa kuhusika na kuueneza virusi vya UKIMWI na walitiwa mbaroni mwezi Februari mwaka 1999 hadi sasa.

Ingawa baada ya uchunguzi kufanyika kwenye hospitali hiyo wataalamu wanaona kuwa pengine chanzo cha maambukizo hayo kilitokana na mazingira mabaya ya hospitali hiyo, lakini mwezi Mei mwaka 2004 mahakama ya Benghazi iliwahukumu kifo watuhumiwa hao sita. Mwishoni mwa mwaka 2005 baada ya rais wa Libya kutangaza kuacha kabisa mpango wa silaha za nyukilia uhusiano kati ya nchi hiyo na nchi za magharibi umeanza kuwa mzuri. Kutokana na ombi la Marekani, Umoja wa Ulaya na Bulgaria, Libya iliamua kupitia upya kesi hiyo.

Lakini katika muda wa zaidi ya mwaka mmoja kesi hiyo ilipopitiwa upya, tofauti kubwa ilitokea kati ya Libya na Bulgaria kuhusu suala la fidia kwa watoto walioambukizwa virusi vya UKIMWI na jamaa zao. Bulgaria inaona kuwa kama ikikubali kutoa fidia ni sawa na kukiri hatia ya watuhumiwa hao sita, kwa hiyo kutokana na usuluhishi wa Umoja wa Ulaya, mwaka 2005 Bulgaria na Libya zilianzisha mfuko wa pande mbili kwa ajili ya kuwasaidia watoto walioathirika na jamaa zao. Lakini siku moja tu kabla ya mahakama kuu ya Libya kutangaza kuunga mkono hukumu ya awali kwa watuhumiwa hao sita, tarehe 10 msimamizi wa mfuko huo ambaye ni mtoto wa rais wa Libya alitangaza kuwa pande zote mbili zimeafikiana kuhusu suala la fidia. Kwa hiyo katika hali kama hiyo hukumu ya kifo kwa watuhumiwa sita inafanya watu wajiulize.

Vyombo vya habari vinaona kuwa katika siku ambayo mahakama kuu ya Libya ilitangaza kuunga mkono hukumu ya awali, waziri wa mambo ya nje wa Libya Bw. Rahman Shalgham alidokeza kuwa kamati kuu ya sheria ya Libya itakutana wiki ijayo na kufanya uamuzi kama itaahirisha au itafuta kabisa hukumu ya kifo kwa watuhumiwa hao sita. Kwa hiyo ni dhahiri kwamba "hukumu ya mwisho" inaweza kubadilika. Hivi sasa baadhi ya watu wanadhani kuwa Libya pengine itabadilisha hukumu ya kifo kuwa hukumu ya kifungo gerezani, na kwa mujibu wa makubaliano husika watuhumiwa hao sita watarudishwa nchini Bulgaria kutumikia vifungo vyao.

Wachambuzi wanaona hukumu ya mahakama kuu ya Libya inaonesha kuwa, kesi hiyo ni ya kutatanisha, kwamba ili Libya iboreshe uhusiano kati yake na Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya, imetumia fursa ya kupitia tena kesi hiyo na kutoa hukumu upya ili kukubaliana na nchi za magharibi, na kujipatia manufaa makubwa zaidi. Hii ndio sababu ya kuahirishwa tena na tena kwa kesi hiyo bila hukumu ya mwisho.

Idhaa ya kiswahili 2007-07-12