|
Tarehe 12 serikali ya Marekani imetoa ripoti kuhusu hali ya Iraq ikijaribu kupunguza malalamiko kutoka bungeni na kwa raia wa Marekani, ya kutaka kuondoa jeshi la Marekani kutoka Iraq, lakini baraza la chini la bunge la Marekani halikudanganywa na ripoti hiyo, bali katika siku ya ripoti hiyo ilipotangazwa bunge lilipitisha sheria moja ikitaka serikali ya George Bush iondoe kabisa jeshi la Marekani kutoka Iraq kabla ya tarehe mosi Aprili mwaka kesho.
Ripoti hiyo yenye kurasa 12, inasema, kati ya malengo yanayowekwa na Marekani malengo 8 hayakutimizwa kama yanavyotakiwa, na malengo 8 yametimizwa kama yanavyotakiwa na malengo mawili yametimizwa vizuri na vibaya nusu kwa nusu, na katika malengo 8 ambayo hayakutimizwa kama yanavyotakiwa yanahusiana na uwezo wa jeshi la Iraq kupigana vita peke yake, utungaji wa sheria kuhusu mgawanyo wa maliasili ya mafuta, miradi ya ukarabati yenye thamani ya dola za Marekani bilioni kadhaa na suala la kusuluhisha migogoro kati ya madhehebu ya kidini. Ripoti inasema, ingawa serikali ya Iraq imepata mafanikio katika sekta fulani, lakini hali ya Iraq bado ni ya kutatanisha na ni changamoto kubwa, mustakabali wa uchumi haujawa wazi, maafikiano ya kisiasa yanasuasua. Katika majira ya joto mwaka huu, Iraq itakabiliwa na "mapambano magumu", jeshi la Marekani nchini humo na jeshi la Iraq litachukua hatua kali.
Ripoti pia inasema, sababu ya serikali ya Iraq kushindwa kutimiza malengo muhimu ni migogoro mikali iliyomo nchini humo, lakini Iraq bado ni nchi yenye matumaini lakini inahitaji muda zaidi.
Ripoti hiyo inasema, hali mbaya ya Iraq pia inatokana na Syria na Iran. Ikisema, Syria kila mwezi inatoa washambulizi wanaojilipua kati ya 50 hadi 80 kwa Al-Qaida nchini Iraq, na Iran inavisaidia kifedha vikundi mbalimbali vyenye siasa kali nchini Iraq.
Isitoshe, ripoti hiyo inatetea sera ya Marekani kuhusu Iraq, ikisema mpango wa kuongeza askari nchini Iraq umeanza tu kutekelezwa, sauti za kutaka kuondoa jeshi la Marekani zinaathiri mchakato wa maafikiano ya kisiasa nchini Iraq, kwa sababu viongozi wa Iraq wanahofu kuwa Marekani haina ahadi ya muda mrefu. Ripoti inaendelea kusema, ingawa mpango wa kuongeza askari nchini Iraq umeanza tu kutekelezwa, lakini hali ya Iraq imeanza kuwa nzuri, na kadiri muda wa jeshi la Marekani unavyoendelea zaidi, ndivyo hali ya Iraq itakuwa nzuri zaidi.
Baada ya ripoti hiyo kutangazwa, wanachama wa chama cha Democratic waliikosoa vikali ripoti hiyo. Kiongozi wa chama cha Democratic chenye viti vingi katika baraza la juu la bunge Bw. Harry Reid alisema, ni bora rais George Bush asikilize kwa makini kauli ya raia wa Marekani na "kufanya mambo yenye maana ya kulinda Marekani", akitaka serikali ya Bush ikubali kushindwa kwa sera zake kuhusu Iraq na kumtaka ashirikiane na bunge ili kutunga sera mpya na kuweka mkazo kwenye mapambano dhidi ya kundi la Al-Qaida.
Spika wa baraza la chini la bunge la Marekani Bibi Nancy Pelosi wa chama cha Democratic alisema, sera za Bush kuhusu Iraq katika miaka mitano iliyopita zimeshindwa, na sasa kazi ya bunge sio tu kueleza maoni yake bali ni kusimamisha vita nchini Iraq kupitia upigaji kura.
Pamoja na hayo, bunge la Marekani ambalo chama cha Democratic kina viti vingi zaidi linaendelea kuishinikiza serikali ya Bush. Baraza la chini la bunge la Marekani lilipitisha sheria ikitaka serikali ya Bush iondoe vikosi vyake vya vita kuanzia tarehe mosi Aprili mwaka kesho.
Kabla ya hapo ikulu ya Marekani iliwahi kusisitiza mara nyingi kuwa, ripoti hiyo ya tarehe 12 ni ripoti ya kutathmini sera ya Bush kuongeza askari katika kipindi cha katikati cha utekelezaji wa sera hiyo, na kabla ya ripoti nyingine kuhusu hali ya Iraq itakayotolewa mwezi Septemba, sera zote za ikulu ya Marekani kuhusu Iraq hazitabadilika.
Idhaa ya kiswahli 2007-07-13
|