Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-16 15:40:02    
Mcheza Filamu Mwanamke Yu Feihong

cri

Yu Feihong ni mcheza filamu nyota nchini China, ingawa yeye bado ni kijana na jina lake linavuma sana miongoni mwa watazamaji, lakini anaishi kimya na kawaida kabisa.

Yu Feihong alipata umaarufu kutokana na mchezo mfululizo wa T.V. "Kushikamana Mikono" aliocheza miaka mitano iliyopita. "Kushikamana Mikono" ni mchezo unaonesha maisha ya kifamilia, ukieleza kuwa wasomi wawili, mume na mke, baada ya kuoana mke alikuwa akishughulika na kazi za nyumbani na kutunza familia kwa moyo wote, lakini kadiri siku zilivyopita mumewe aliona mkewe hakuwa anamvutia kama hapo awali, katika hali hiyo ya kutokuwa na mapenzi, alianza kuwa na mpenzi nje ya ndoa, mikwaruzano ikaanza kutokea na furaha ya familia yake ikapotea. Mchezaji filamu Yu Feihong aliigiza kama "mpenzi" huyo katika mchezo huo, ambaye ameanza tu kazi baada ya kumaliza masomo ya chuo kikuu. Ni msichana aliyetamani kuwa na mapenzi, mwenye roho nzuri na elimu. Alimhurumia mfanyakazi mwenzake na kuelewa vema usumbufu wa mwanamume huyo asiyekuwa na mapenzi na mkewe. Katika maingiliano ya kawaida, bila makusudi mapenzi kati yao yalianza kuonekana. Msichana huyo alipotanabahi kuwa amekuwa "kimada", alizama katika hali ya utatanishi wa mawazo, kwamba kwa upande mmoja aliona mwanamume huyo anastahili kujinasua kutoka ndoa isiyo na mapenzi, kwa upande mwingine, aliona mke wake anaendelea kumpenda sana mumewe, mwenendo wake utatia chumvi katika jeraha la familia hiyo. "Kimada" huyo mara kwa mara aliwaza na kuwazua, na mwishowe aliamua kujitoa kutoka mapenzi hayo na kwenda mbali pasipojulikana.

Kutokana na jinsi jamii inavyoendelea nchini China, dhana za Wachina kuhusu ndoa: "mume na mke kuishi mpaka mwisho", zimekabiliwa na changamoto, hali ya kuwa na mpenzi nje ya ndoa inashamiri na kulaaniwa na jamii. Filamu "Kushikamana Mikono" ilifanikiwa kutokana na mchezaji Yu Feihong kucheza vizuri. Nafasi aliyoigiza "hawara" nje ya ndoa, badala ya kuwachukiza watazamaji iligeuza uchukivu wa baadhi ya watazamaji kuhusu "hawara".

Katika mchezo huo, Yu Feihong alikuwa kama binti wa majirani ya watazamaji, kwamba ni msichana mwenye tabia nzuri hakuonekana kama anacheza mchezo bali anaonekana anaishi katika maisha halisi. Alipolia watazamaji walimhurumia kama wanavyomhurumia binti yao. Watazamaji wanampenda "hawara" huyo, ambaye aliigizwa na Yu Feihong, basi Yu Feihong yeye mwenye amekuwa mchezaji anayependwa na watazamaji.

Baadhi ya watazamaji wanaona kuwa Yu Feihong amepata umaarufu kwa bahati tu, lakini yeye mwenyewe anaona kuwa ufanisi huo ni matokeo ya juhudi zake za miaka mingi. Alisema, "Kama nisingecheza mchezo huu, nitacheza mwingine, na ningecheza vizuri katika mchezo mwingine pia ningepata umaarufu huo."

Yu Feihong alizaliwa katika mji wa Hangzhou, kusini mwa China. Tokea alipokuwa na umri wa miaka 8 alianza kuonesha uhodari wake wa uchezaji wa filamu, na kuanzia hapo aliwahi kucheza michezo mingi ya filamu. Alipokuwa kidato cha kwanza katika sekondari ya juu, kwa mara ya kwanza aliiigiza mhusika mkuu katika filamu moja ya "Jambazi na Mhofu". Katika filamu hiyo Yu Feihong aliigiza kama msichana mwongozaji wa watalii, huyo mwongozaji alipokuwa pamoja na mchumba wake alikutwa na jambazi, aliporwa na kachafuliwa. Katika tukio hilo alisononeka jinsi mchumba wake alivyotishika bila kumwokoa. Kisha baadaye mchumba huyo alijilaumu na alisononeka vibaya, hata mwishowe alikiuka sheria kumchoma kwa jambia jambazi yule baada ya kumpata tena ili aondoe sononeko rohoni mwake, lakini akawa mhalifu. Kuona ujasiri wa mchumba wake, mwongozaji huyo alijawa na mchanganyiko wa furaha na simanzi, alijitahidi kumtetea hata kwa ushahidi wa uwongo. Katika filamu hiyo mchezaji Yu Feihong mwenye umri wa miaka 15 tu wakati huo aliigiza vizuri sana jinsi alivyosumbuliwa mbele ya adhabu ya kisheria na mpenzi wake.

Baada ya kumaliza masomo ya sekondari alijiunga na Chuo Kikuu cha Filamu, na alibaki chuoni kuwa mwalimu. Alisema, "Nilibakizwa chuoni na kuwa mwalimu, niliona elimu yangu haikuwa ya kutosha, sikuweza kuwafundisha wanafunzi wangu yale yale niliyoyapata kutoka kwa mwalimu wangu bila kuwa na yangu mwnyewe. Nilitaka kuwa na elimu zaidi na kuwa na hisia zangu mwenyewe."

Yu Feihong aliondoka kwenye chuo chake na kwenda Marekani kujiendeleza kimasomo. Alijishupaza ugenini na kupambana na adha ya maisha. Alipokuwa katika hali ya upweke, alilia, aliwapigia simu watu wengi wenzake, akisema anataka kurudi nyumbani, lakini alivumilia mpaka alipomaliza masomo yake. Maisha aliyoishi nchini Marekani yalimpatia kumbukumbu zisizosahaulika.

Ingawa yeye ni mchezaji nyota, lakini anaishi maisha ya kikawaida kabisa. Ni nadra sana kumwona katika sehemu za burudani. Hamu yake katika mapumziko ni kusoma, kuongea na wazazi wake na kutalii. Anaona kuwa mtu kuwa na moyo wa kawaida mbele ya mafanikio atakuwa na maisha ya furaha. Alisema, "Ukiwa na moyo mkubwa utapata furaha nyingi, usipokuwa na moyo mkubwa utakosa furaha nyingi. Mimi nataka nifurahi, kazi yangu ya kuwaburudisha watazamaji ndio furaha yangu."

Idhaa ya kiswahili 2007-07-16