Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-16 18:42:31    
Mkutano wa kimataifa wa kujadili suala la Darfur wafunguliwa

cri

Mkutano wa kimataifa wa kujadili suala la Darfur ulifunguliwa tarehe 15 huko Tripoli, Libya, ukilenga kuweka ratiba kwa ajili ya kuanza tena kwa mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Sudan na makundi yote ya waasi katika jimbo la Darfur, nchini Sudan.

Huu ni mkutano wa pili wa namna hii kufanyika nchini Libya mwaka huu. Pamoja na wajumbe kutoka serikali ya Sudan na makundi ya waasi, watu wanaohudhuria mkutano huo wa siku mbili ni wajumbe kutoka Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Umoja wa nchi za kiarabu, Umoja wa Ulaya, nchi jirani za Sudan na nchi tano zenye uanachama wa kudumu kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Mjumbe maalumu wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Jan Eliasson alisema, mkutano huo utasaidia pande zinazohusika za Sudan ziimarishe ushirikiano kwa ajili ya kurudisha mazungumzo ya amani, kuamua kazi za Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika katika suala la Darfur, na kuzishirikisha nchi jirani za Sudan zitoe mchango katika kuleta utatuzi wa suala hilo.

Mjumbe wa Umoja wa Afrika Bw. Salim Ahmed Salim alisema mapigano yanayoendelea huko Darfur yatazidi kuharibu utulivu na usalama wa sehemu hiyo, na pande zinazohusika za Sudan zote zinatakiwa kujiunga na mazungumzo ya amani ya kujadiliana mustakabali wa sehemu hiyo. Aliongeza kuwa kwenye mchakato wa siasa utakaoanzishwa hivi karibuni huko Darfur, maoni na mapendekezo ya wakazi wa Darfur yatasikilizwa.

Mkutano huo utazungumzia masuala mawili. La kwanza ni kuweka ratiba kwa ajili ya kuanza tena kwa mazungumzo ya amani, mambo yatakayoamuliwa ni pamoja na tarehe, mahala na mada za mazungumzo hayo. Hivi sasa pande mbalimbali bado zina maoni tofauti kwamba, serikali ya Sudan imeeleza wazi kuwa, haitajadili upya vifungu vya mkataba wa Abuja, wakati makundi ya waasi yanataka mkataba huo ufanyiwe marekebisho makubwa ili yanufaike zaidi.

Suala lingine muhimu la mkutano huo ni jeshi la mseto la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika litakalowekwa huko Darfur. Kutokana na makubaliano ya mwanzo yaliyofikiwa kati ya serikali ya Sudan na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, jeshi hilo litakuwa na watu elfu 26 na kuongozwa na mtu atakayeteuliwa na Umoja wa Afrika. Habari zinasema baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatazamiwa kupitisha azimio, ambalo litaruhusu jeshi hilo lichukue mbinu mbalimbali za lazima litakapotekeleza jukumu lake.

Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Bw. Al Sammani Al Wasila anayehudhuria mkutano huo, alisema serikali ya Sudan inashikilia kuwa hatua za kijeshi hazisaidii utatuzi wa suala la Darfur, usalama na utulivu wa sehemu hiyo hautatimizwa bila njia ya amani inayozishirikisha pande mbalimbali. Aliongeza kuwa maandalizi ya mazungumzo kati ya serikali ya Sudan na makundi ya waasi yataanza kwa haraka, na mazungumzo ya duru ya kwanza yanatazamiwa kufanyika kabla ya mwezi Septemba mwaka huu.