Mkutano wa kimataifa kuhusu suala la Darfur ulimalizika tarehe 16 huko Tripoli, mji mkuu wa Libya. Mkutano huo umeonesha wazi mwelekeo wa utatuzi wa mgogoro wa Darfur.
Kwanza, mkutano huo umebaini kuwa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na nchi jirani za Sudan ni nguvu muhimu ya kutatua mgogoro wa Darfur. Taarifa iliyotolewa wakati mkutano huo ulipomalizika imesifu sana juhudi zilizofanywa na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, nchi za Libya, Misri na nchi nyingine jirani za Sudan kwa ajili ya kurudisha amani ya Darfur na kutaka nchi na jumuyia hizo ziwe na mawasiliano na serikali ya Sudan, vikundi mbalimbali vya upinzani na wajumbe wa wakimbizi na kufahamu misimamo yao kuhusu mazungumzo ya amani. Taarifa pia imevitaka vikundi ambavyo bado havijasaini "Makubaliano ya Amani ya Darfur" vishiriki kwenye mkutano wa kuandaa mazungumzo ya amani utakaofanyika tarehe 3 hadi 5 Agosti nchini Tanzania, na kuvitaka vikundi vya Darfur vishauriane kuhusu mahali na wakati wa kufanya kwa mazungumzo hayo. Taarifa pia inawataka mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa watoe mwaliko rasmi kwa wajumbe watakaoshiriki kwenye mazumgumzo ya amani kabla ya mwishoni mwa Agosti.
Pili, mkutano unavihimiza vikundi vyote vya upinzani vya Darfur visawazishe misimamo yao na kufanya mazungumzo na serikali ya Sudan. Hivi sasa serikali ya Sudan iko tayari kufanya mazungumzo na vikundi vyote vya upinzani vinavyotaka kweli kuleta amani ya Darfur hadi kusaini makubaliano katika msingi wa "Makubaliano ya Amani ya Darfur". "Makubaliano ya Amani ya Darfur" yalitiwa saini mwezi Mei mwaka 2006 kati ya serikali na kikundi kimoja kikubwa cha upinzani. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, vikosi vya upinzani vitavunjwa na watanyang'anywa silaha. Lakini vikundi vingine vya upinzani vya Darfur vilikataa kusaini makubaliano hayo. Vikundi hivyo vilitaka makubaliano hayo yarekebishwe ili vijipatie manufaa makubwa zaidi na kunufaika na madaraka na maliasili huko. Kuhusu suala hilo Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika pamoja na nchi jirani za Sudan zilifanya majadiliano mara nyingi. Hivi sasa mkutano huo unataka vikundi vyote vya upinzani visawazishe misimamo yao na kushiriki kwenye maandalizi ya mazungumzo ya amani. Hili ni jambo muhimu sana.
Tatu, mkutano huo unafurahia makubaliano ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na serikali ya Sudan kuhusu kupanga jeshi la muungano la kulinda amani na kutaka pande mbalimbali zisimamishe vita mara moja katika sehemu ya Darfur na kushiriki kwenye mchakato wa makubaliano ya kisiasa hadi kufikia makubaliano ya kisiasa ya kumaliza kabisa mgogoro. Mkutano unaonesha wazi kwamba jeshi la muungano linasaidia kumaliza hali mbaya ya Darfur na kumaliza maafa ya kibinadamu yaliyodumu kwa zaidi ya miaka minne.
Mkutano huo umesifiwa sana na pande husika. Mjumbe maalumu wa China kuhusu suala la Darfur Bw. Liu Guijin kwenye hotuba yake alionesha uungaji mkono kwa juhudi zinazofanywa na Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na nchi jirani za Sudan. Alisema ili kusukuma mchakato wa kisiasa Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na serikali ya Sudan ni nguvu muhimu na pande mbalimbali husika zinapaswa kuvishawishi vikundi mbalimbali vya Darfur vifanye mazungumzo ya kisiasa na serikali ya Sudan. Ameitaka jumuyia ya kimataifa itilie maani ukarabati na misaada halisi ya hali na mali kwa ajili ya maendeleo ya Darfur.
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Afrika Bw. Salim Ahmed Salim alisisitiza kuwa mkutano huo ni muhimu kwa Darfur na hata kwa nchi nzima ya Sudan, na unaonesha kuwa wakati wa kurudisha mazungumzo ya amani na kutekeleza mpango wa "ramani ya amani" umewadia.
Idhaa ya kiswahili 2007-07-17
|