Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-18 18:21:54    
Libya yatoa hukumu ya kifungo cha maisha kwa wauguzi watano na daktari mmoja wa Bulgaria waliohusika na kueneza virusi vya Ukimwi

cri

Kamati kuu ya sheria ya Libya tarehe 17 usiku huko Tripoli ilitoa taarifa ikitangaza kutoa kifungo cha maisha badala ya hukumu ya kifo kwa wauguzi watano na daktari mmoja wa Bulgaria walioshitakiwa kwa kuhusika na tukio la kueneza virusi vya ukimwi ya Benghazi.

Japokuwa taarifa hiyo haikueleza kama washitakiwa hao 6 waliofungwa kwa miaka 8 nchini Libya watarejeshwa nchini Bulgaria au la, lakini kutokana na kuwa Libya na Bulgaria zimesaini makubaliano ya kuwarejesha wahalifu nchini Bulgaria, hivyo baada ya kubadilishwa kwa hukumu yao, sasa wamepata matumaini ya kuachiwa huru. Kamati kuu ya sheria ya Libya ilipanga kufanya mkutano huo asubuhi ya tarehe 16, lakini wakati wa kufanya mkutano uliahirishwa mara kwa mara mpaka usiku wa tarehe 17. Ofisa husika wa Libya alidokeza kuwa, sababu ya kuchelewesha kwa kutangazwa matokeo hayo ni kuwa, watu walioambukizwa virusi vya ukimwi kutokana na tukio hilo na jamaa zao walikuwa bado hawajapata fidia zao, na walikataa kusaini mkataba husika. Hadi kufikia alasiri ya tarehe 17, msemaji wa walioathirika alithibitisha kuwa, matakwa ya fidia yaliyotolewa na familia zote 460 za walioathirika yalikuwa yametimizwa, yaani kila familia itapewa fidia kubwa ya dola za kimarekani milioni moja, hivyo walioathirika na jamaa zao walikubali kutoshikilia hukumu ya kifo kwa washitakiwa hao.

Tukio la kueneza virusi vya ukimwi huko Benghazi lilitokea mwishoni mwa karne iliyopita. Watoto 438 waliolazwa katika hospitali ya Benghazi waliambukizwa virusi vya ukimwi, na kusababisha vifo vya watoto 56. Wauguzi watano wa Bulgaria na daktari mmoja wa Bulgaria mwenye asili ya Palestina walishitakiwa kuhusika na kesi hiyo. Mwaka 1999 watu hao 6 walikamatwa na kufungwa hadi leo. Ingawa washitakiwa hao 6 walishikilia kutokuwa na hatia yoyote, lakini mwezi Mei mwaka 2004 mahakama ya Benghazi iliwahukumu adhabu ya kifo, na hukumu hiyo ilithibitishwa na mahakama kuu ya Libya tarehe 11 Mei ya mwaka huu.

Kamati kuu ya sheria ya Libya ni chombo cha juu kabisa cha sheria nchini Libya, hivyo uamuzi wa kamati hiyo ni uamuzi wa mwisho kwa washitakiwa hao 6. Hivi sasa kamati kuu ya sheria ya Libya imefanya uamuzi wa kutoa hukumu ya kifungo cha maisha badala ya hukumu ya kifo. Hukumu hiyo imepunguza hofu kwa watu waliokuwa wanafuatilia kesi hiyo, lakini wachambuzi wanaona kuwa, kamati kuu ya sheria ya Libya kufanya uamuzi huo ni jambo la wakati tu. Wamedhihirisha kuwa, tokea mwishoni mwa mwaka 2005 kiongozi wa Libya Muamar Gadafi alipotangaza kuacha kuendeleza na kutengeneza silaha kali, na kutaka kujiunga tena na jumuiya ya kimataifa, Libya siku zote ilikuwa inatafuta fursa ya kuafikiana na Marekani, Umoja wa Ulaya na Bulgaria kuhusu kesi ya Benghazi. Hivyo kutokana na msaada wa Marekani na Umoja wa Ulaya, Libya na Bulgaria zilianzisha mfuko wa kimataifa wa Benghazi, ili kuwafidia waathirika na familia zao.

Wachambuzi wanasema kamati kuu ya sheria ya Libya kutoa hukumu ya kifungo cha maisha badala ya hukumu ya kifo kwa washitakiwa 6, kumeleta fursa mpya kuondolewa kwa kesi ya kueneza virusi vya ukimwi ya Benghazi iliyozisumbua nchi hizo mbili kwa muda mrefu, na washitakiwa sasa wameongezewa matumaini ya kuachiwa huru. Hatua hiyo ya Libya pia itasaidia kuboresha uhusiano kati yake na nchi za magharibi, na kuondoa kikwazo kilichowekwa na nchi za magharibi dhidi yake kutokana na jambo hilo, ili ijiunge tena na jumuiya ya kimataifa.