Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-18 19:04:29    
Kazi ya kushughulikia simu za mikononi zilizotumika nchini China

cri

Kutokana na maendeleo ya kasi ya uchumi wa China, bidhaa mbalimbali za elektroniki zimekuwa zinatumiwa sana na watu, na uchafuzi unaosababishwa na takataka za elektroniki sasa umeanza kufuatiliwa. Simu za mikononi ni moja ya bidhaa za kielektroniki zinazotumiwa mara kwa mara katika maisha yetu, na kama hazishughulikiwi vizuri, basi zinaweza kuleta uchafuzi mkubwa kwa mazingira yetu.

Kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa na wizara ya upashanaji habari ya China, hivi sasa idadi ya watumiaji wa simu za mikononi nchini China imefikia milioni 480, China imekuwa nchi yenye watumiaji wengi kabisa wa simu za mkononi duniani. Lakini kutokana na maendeleo ya kasi ya teknolojia ya simu za mikononi, watumiaji wanabadilisha simu mara kwa mara, simu nyingi zilizotumika zinatupwa na kushughulikiwa pamoja na takataka za kawaida. Simu hizo na betri zake zikizikwa ardhini, vitu vya metali nzito vilivyomo kwenye simu hizo, vikiwemo dhahabu, zebaki, risasi na cadmium, vinachafua moja kwa moja ardhi na maji ya chini ya ardhi. Na kama zikiteketezwa, gesi za sumu zinazotolewa na takataka hizo, pia zinaweza kuchafua hewa na kuleta madhara makubwa kwa afya ya binadamu.

Kwa hivyo ili kutatua suala la kushughulikia simu zilizotumika, jambo muhimu na pia ufumbuzi bora ni kuanzisha utaratibu wa kushughulikia takataka za kielektroniki unaounganisha shughuli za utengenezaji, uuzaji na utumiaji wa bidhaa hizo. Kampuni ya huduma za simu za mkonini ya China Mobile ambayo ni kampuni kubwa kabisa ya huduma hiyo nchini China, inashirikisha makampuni kadhaa ya kuzalisha simu za mikononi, yakiwemo Motorola na Nokia, na kuanzisha harakati moja ya hifadhi ya mazingira iitwayo 'mpango wa sanduku la kijani'. Naibu mwenyekiti wa bodi ya kampuni hiyo Bw. Sha Yuejia alisema:

"shughuli za kushughulikia, usimamizi na utumiaji tena kwa simu za mikononi zilizotumika si kama tu ni matakwa ya ujenzi wa jamii inayoishi vizuri na mazingira, bali pia ni matakwa ya shughuli za ujenzi wa jamii inayobana matumizi ya nishati nchini China. Kampuni yetu inaahidi kwa makini kwamba, tutaongeza nguvu zaidi katika shughuli za kushughulikia bidhaa hizo zilizotumika, na pia tunakaribisha makampuni mengi zaidi yanayozalisha au kuuza bidhaa hizo yashiriki kwenye mpango wa "sanduku la kijani", ili kutoa mchango kwenye kuhifadhi mazingira yetu tunayoishi."

Imefahamika kuwa mpango wa sanduku la kijani umeanza kutekelezwa katika miji 40 muhimu nchini China, masanduku ya kijani yakuhifadhia simu zilizotumika na sehemu zake yamewekwa kwenye vituo zaidi ya 1000 vya utoaji huduma za kampuni ya China Mobile, vituo 300 vya uuzaji na utengenezaji wa simu za mikononi za Motorola na Nokia nchini China.

Mpango huo umetatua kikamilifu suala la njia ya kuzirudisha viwandani simu zilizotumika, na pia umesanifu kisayansi utaratibu wa kuzirudisha simu hizo viwandani. Kila simu na sehemu zinakorudishwa kwenye sanduku hilo zinaandikishwa na kufungwa. Simu zote zinazorudishwa zinashughulikiwa na idara maalum, ili kuondoa madhara yake na kurudisha kiwandani sehemu zake zinazoweza kutumika tena. Hatua hiyo si kama tu imehamasisha makampuni ya kutengeneza simu za mikononi, bali pia imehimiza kuinuka kwa mtizamo wa umma kuhusu hifadhi ya mazingira, na kuwashirikisha kwenye shughuli za kuboresha mazingira ya kijamii na kimaumbile. Naibu mwenyekiti wa bodi ya kampuni ya China Mobile Bw. Sha Yuejia alisema:

"tulikuwa na mpango kamili kabla ya kutekeleza mpango wa sanduku la kijani, tuliwasiliana na makampuni yanayotengeneza na kuuza simu za mkononi, na raslimali nyingi zimetumika kwa ajili ya mpango huo."

Shughuli za kurudisha viwandani simu za mkononi na betri zilizotumika zina maslahi ya kiuchumi na kijamii yasiyoonekana. Kwa mfano wa betri peke yake, kila betri ya simu ya mikononi ina gram 6 hivi za kitu cha cobalt, hivi sasa kila mwaka simu za mikononi zaidi ya milioni 100 nchini China zinabadilishwa. Kama betri milioni 100 za simu hizo zikirudishwa kiwandani na kushughulikiwa kila mwaka, zinaweza kutoa tani 600 za cobalt. Hivyo shughuli hizo zitaweza kuwa kama 'mgodi wa dhahabu mijini'.

Ili kupanua athari za mpango huo, kuimarisha mtizamo wa umma kuhusu uhifadhi wa mazingira na kuwashirikisha watu wengi zaidi kwenye mpango huo, kampuni ya China Mobile pia iliwaalika watu wengi mashuhuri kushiriki kwenye shughuli mbalimbali husika. Mmoja wao ni bingwa wa Jimnastiki kwenye michezo ya Olimpiki Bw. Teng Haibing, alisema:

"mpango huo unaitikia 'Olimpiki ya kijani' na kuhimiza watu waweke simu za mikononi zilizotumika na sehemu zake kwenye "sanduku la kijani", ili kurahisisha shughuli za kurudisha na kupunguza uchafuzi kwa mazingira. Shughuli hiyo ina umuhimu mkubwa, sote tushiriki kwenye mpango huo."

Hivi sasa mpango wa hifadhi ya mazingira wa "sanduku la kijani" unatambuliwa na kuitikiwa na watu wengi zaidi. Mkazi wa Beijing Bw. Yue Wei alisema:

"nadhani kuwa shughuli hizi za China Mobile zina umuhimu mkubwa, natumai kuwa kwa kupitia shughuli hizo, watu wengi zaidi wataunga mkono shughuli za uhifadhi wa mazingira na kutunza mazingira ya mji wa Beijing na kuijenga Beijing iwe nzuri zaidi."

Wataalamu wanasema, ili kuzuia uchafuzi unaosababishwa na simu za mkononi zilizotumika, mbali na kutekeleza mpango wa sanduku la kijani, makampuni ya kutengeneza simu za mikononi yanapaswa kuzingatia shughuli za usanifu na utengenezaji wa simu hizo kwa mtizamo wa "usanifu wa kijani" na "usanifu wa kiikolojia", na pia yanapaswa kupunguza matumizi ya malighafi yenye sumu katika utengenezaji wa simu na kuendeleza malighafi isiyo na sumu, na inayoweza kutumika tena kwa uvumbuzi wa kisayansi.