Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-19 15:34:30    
Kilimo na ufugaji maalum wa sehemu ya Linzhi mkoani Tibet

cri

Sehemu ya Linzhi iko kusini mashariki mwa mkoa unaojiendesha wa Tibet, ina mandhari nzuri, na wanaishi watu wa makabila madogo madogo kama vile kabila la Wamenba na kabila la Waluoba. Katika miaka ya hivi karibuni, sehemu ya Linzhi inapojitahidi kulinda na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa nafaka mbalimbali, pia imechukua hatua mwafaka kuhimiza kilimo na ufugaji wenye umaalum wa kipekee, na maisha ya wakulima na wafugaji wa huko yanaboreshwa mwaka hadi mwaka.

Katika kijiji cha Jiadingga cha wilaya ya Linzhi, Bi. Yangjin anajulikana kwa kulima mboga. Katika shamba lake la mboga amelima nyanya, matango, mabiringanya na mboga nyingine. Mapato yake kutokana na mauzo ya mboga kwa mwaka yanazidi Yuan elfu 60. Alisema:

"Mwanzoni nilikuwa nalima nafaka tu, kutokana na mavuno kuwa madogo na bei kuwa ya chini, tuliishi maisha magumu. Mwaka 2002 nilianza kulima mboga, mapato yangu yamekuwa yanaongezeka mwaka hadi mwaka."

Kijiji cha Jiadingga kina familia 50 za wakulima, na shamba la kilimo hekta 49. Ofisa wa serikali ya kijiji hicho Bwana Nima alisema, hivi sasa familia 48 kati ya 50 za kijiji hicho zinalima mazao ya biashara na kufuga mifugo. Kwa jumla kijiji hicho kina magari makubwa na madogo na mitambo ya kilimo zaidi ya 30, na wastani wa mapato ya wanakijiji kwa mtu mmoja unafikia Yuan elfu kumi.

Bw. Nima anayewaongoza wanakijiji wenzake kujiendeleza kiuchumi, mwenyewe ni hodari sana katika kujiendeleza. Alikuwa mfanyabiashara wa kwanza katika kijiji cha Jiadingga, pia alikuwa mtu wa kwanza wa kijiji hicho kujishughulisha na uchukuzi. Hivi sasa wanakijiji wengi wamejenga nyumba mpya kwa chuma cha pua na zege, na hayo yanatokana na kujishughulisha na kilimo na ufugaji wenye umaalum wa kipekee. Alisema:

"Wakulima wengi wa kijiji chetu walianza kulima mboga kuanzia mwaka 2000, ilipofika mwaka 2006 wastani wa mapato ya wanakijiji ilikuwa imefikia Yuan 11,900. Lengo letu ni kuwa, ifikapo mwaka 2010 wastani wa mapato wa wanakijiji ufikie Yuan elfu 20."

Sehemu ya Linzhi ina raslimali nyingi za kilimo na utalii. Maendeleo ya kijiji cha Jiadingga ni mfano mdogo wa sehemu ya Linzhi. Katika miaka ya hivi karibuni, sehemu ya Linzhi imeenzi ubora wake wa kuwa na raslimali nyingi kuendeleza shughuli maalum za miti ya kibiashara, mitishamba na mboga. Pia kuendeleza shughuli za ufugaji kama vile kufuga nguruwe wa kitibet na kuku wa kitibet, na kutimiza malengo ya kupanuka kwa kiwango cha kilimo maalum, kuongezeka kwa mazao ya kilimo maalum na kuongezeka kwa mapato ya wakulima.

Ili kuendeleza kilimo maalum, sehemu ya Linzhi imeunda mashirika ya aina mbalimbali kama vile "Jumuiya ya kiuchumi ya kufuga nguruwe wa kitibet", "Jumuiya ya ushirika wa kufuga kuku wa kitibet", "Jumuiya ya ushirika wa kiuchumi ya uyoga wa misonobari", na "Jumuiya ya ushirika ya mboga ya wakulima wa Jiadingga". Sehemu ya Linzhi pia ilichukua fursa ya kuanzisha miradi ya uzalishaji maalum wa kilimo na mifugo kujenga makampuni zaidi ya 10 yanayozalisha mazao ya kilimo na mifugo kwa wingi. Mkuu wa idara ya kilimo na ufugaji ya Linzhi Bwana Wang Jie alisema:

"Katika miaka ya karibuni, sehemu ya Linzhi inashikilia kanuni ya kutoa kipaumbele kuwekeza katika sehemu yenye raslimali nyingi, kuweka mkazo kuongeza mapato ya wakulima na kufanya marekebisho ya uzalishaji, kuongeza uwezo wa wakulima na wafugaji wa kujiendeleza."

Hivi sasa teknolojia nyingi za kilimo na ufugaji kama vile kuzaliana na kufuga nguruwe wa kitibet, kuatamiza mayai ya kuku wa kitibet na kuwafuga, kuzalisha na kusindika mitishamba ya kitibet na kilimo cha mboga na matunda yasiyo na uchafuzi zimetumiwa na wakulima na wafugaji wa huko, kiwango cha kilimo maalum kinainuliwa siku hadi siku. Mwaka jana sehemu ya kuanzisha miradi ya shughuli maalum za uzalishaji ilizinufaisha familia zaidi ya 3900 zenye idadi ya watu 22,000. Kutokana na maendeleo ya kilimo na ufugaji maalum, inaaminika kuwa maisha ya wakazi wa makabila madogo madogo waishio katika sehemu ya Linzhi bila shaka yataboreshwa siku hadi siku.

Idhaa ya kiswahili 2007-07-19