Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-19 14:52:31    
Jeshi la Marekani lamkamata kiongozi mwandamizi wa tawi la Al-Qaida nchini Iraq

cri

Tarehe 18 jeshi la Marekani lilitangaza kuwa kiongozi mwandamizi wa tawi la Al-Qaida nchini Iraq Khalid al-Mashhadani alikamatwa tarehe 4 na jeshi la Marekani katika mji wa Mosul kaskazini mwa Iraq.

Jeshi la Marekani lilisema Bw. Mashhadani ni rafiki mkubwa wa mkuu wa tawi la Al-Qaida nchini Iraq Bw. Abu Ayyub al-Masri, na aliwahi kuwa kiongozi wa kikosi cha Al-Qaida nchini Iraq. Miaka miwili na nusu iliyopita alijiunga na Al-Qaida na kushughulikia uenezi katika tawi la Al-Qaida nchini Iraq. Mwaka 2006 Bw. Masri alichukua wadhifa wa Zarqawi aliyeuawa na jeshi la Marekani, na Mashhadani pia alipandishwa cheo kuwa kiongozi mwandamizi miongoni mwa Wairaq katika tawi la Al-Qaida nchini Iraq. Kutokana na kuwa Bw. Mashhadani anawajibika kufikisha mawasiliano kati ya Masri na kiongozi wa pili wa Al-Qaida, anafahamu habari nyingi kuhusu Al-Qaida. Kwa mujibu wa maelezo aliyotoa Bw. Mashhadani baada ya kukamatwa, Abu Omer al-Baghdadi ni "mtu aliyebuniwa", hotuba yake ilitokana na rekodi ya mwigizaji mmoja wa filamu, lengo la kumbuni mtu huyo asiyekuwepo ni kwa ajili ya kuwaambia watu kuwa kundi la Al-Qaida linaongozwa na Mwiraq.

Kadiri ongezeko la askari elfu 30 wa Marekani linavyokamkilishwa nchini Iraq, ndivyo jeshi la Marekani nchini Iraq linavyozidi kufanya operesheni mjini Baghdad na sehemu za pembezoni mwa mji huo. Kabla ya hapo jeshi la Marekani liliwahi kutangaza kuwa katika miezi miwili tu ya Mei na Juni jeshi la Marekani liliwaua au kuwakamata maofisa 26 wa Al-Qaida nchini Iraq. Kukamatwa kwa Mashhadani hakika ni mafanikio makubwa yaliyopatikana katika msako wa jeshi la Marekani katika mwezi Julai. Lakini wachambuzi wanaona kuwa kukamatwa kwa Bw. Mashhadani hakuwezi kuboresha hali mbaya ya usalama wa Iraq, kwa hiyo hakuna umuhimu mkubwa katika mambo ya usalama na siasa.

Kwanza, mfumo wa Al-Qaida nchini Iraq bado haujavunjwa bali unaendelea, tishio lake kwa Marekani katika mambo ya uchumi, siasa na usalama halijapungua. Tokea tukio la "Septemba 11" lililotokea mwaka 2001, Marekani ilichukua hatua nyingi dhidi ya Al-Qaida, lakini hatua hizo hazikufua dafu, badala yake Al-Qaida inafufuka siku hadi siku hadi kufikia kiwango kama ilipokuwa katika siku za tukio la "Septemba 11". Ripoti iliyotolewa na Marekani hivi karibuni imesema, tawi la Al-Qaida nchini Iraq ni kikundi chenye nguvu kubwa na ni kikundi pekee kilichotangaza kufanya ushambulizi nchini Marekani. Baadhi ya raia wa Marekani wanashutumu na kusema kuwa vita vya Marekani dhidi ya Iraq vimegawanya nguvu ya kupambana na ugaidi.

Pili, hali mbaya ya usalama nchini Iraq haitabadilika kutokana na kukamatwa kwa kiongozi fulani wa tawi la Al-Qaida nchini Iraq. Tokea vita vya Iraq vianze, Marekani imetumia fedha nyingi na watu wengi ili kupambana na vikundi vinavyopinga Marekani na kufanya misako mara nyingi zisizohesabika, lakini matokeo yake ni madogo sana. Hivi sasa askari wa Marekani nchini Iraq wamefikia laki 1.56, na askari polisi laki 3.4 wa Iraq waliofundishwa na Marekani kwa fedha dola za Kimarekani milioni 1.9 bado hawawezi kuwajibika peke yao, na hata baadhi yao wanashiriki kisiri siri kwenye vitendo vya kuipinga Marekani na serikali. Kwa kutegemea kuongeza nguvu za kijeshi, Marekani na serikali ya Iraq haziwezi kuboresha hali ya usalama wa Iraq.

Zaidi ya hayo, ingawa kukamatwa kwa kiongozi fulani wa tawi la Al-Qaida nchini Iraq kunasaidia serikali ya George Bush na kupunguza shinikizo la kutaka kuondoa jeshi la Marekani kutoka Iraq, lakini mfarakano ndani ya serikali ya Iraq unakuwa wazi siku baada ya siku, na tofauti kati ya madhehebu ya kidini na mgogoro kuhusu mgawanyo wa maliasili umekuwa ukiongezeka, kwa hiyo jeshi la Marekani likiendelea kubaki nchini Iraq kwa muda mrefu zaidi na kuongeza askari zaidi, ndivyo litakavyozidi kuzama kwa kina ndani ya matope nchini Iraq.

Idhaa ya kiswahili 2007-07-19