Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-20 15:06:21    
Mazungumzo ya pande nne kuhusu suala la Mashariki ya Kati yafanyika mjini Lisbon

cri

Mazungumzo ya pande nne kuhusu suala la Mashariki ya Kati yalifnyika tarehe 19 mjini Lisbon, mji mkuu wa Ureno, na kujadili pendekezo la Marekani la "kuitisha mkutano wa kimataifa kuhusu amani ya Mashariki ya Kati". Huu ni mkutano wa kwanza wa ngazi ya juu kufanyika baada ya kundi la Hamas kuudhibiti ukanda wa Gaza na baada ya waziri wa zamani wa Uingereza Bw. Blair kuteuliwa kuwa mjumbe maalumu wa pande nne anayeshughulikia suala la Mashariki ya Kati. Kwa hiyo mkutano huo unafuatiliwa sana.

Waliohudhuria mkutano huo ni katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon, mjumbe wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia sera za kidiplomasia na usalama Bw. Javier Solana, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Condoleezza Rice na waziri wa mambo ya nje wa Russia Bw. Sergei Lavrov. Kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya mkutano huo Bw. Ban Ki-moon alisoma taarifa akisema pande nne zinafurahia taarifa iliyotolewa tarehe 16 na rais George Bush. Bi. Condoleezza Rice alisema jumuyia ya kimataifa imebadilisha mpango husika ili kutunga sera kuhusu kuwepo kwa nchi mbili za Israel na Palestina. Bw. Blair alifurahia nguvu mpya ya kusukuma mchakato wa amani kati ya Israel na Palestina. Alisema, mpango wa kuwepo kwa nchi mbili una umuhimu mkubwa, kwani Israel inaweza kupata uhakikisho wa usalama na Palestina itakuwa na vyombo vya utawala vyenye nguvu.

Siku kadhaa kabla ya kufanyika kwa mkutano huo, rais wa Marekani Bw. George Bush alitoa taarifa akitaka uitishwe mkutano wa kimataifa utakaoshirikisha wajumbe kutoka Israel, mamlaka ya utawala wa Palestina na nchi kadhaa za Kiarabu ili kuanzisha tena mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati. Msimamizi wa mkutano huo ambaye pia ni nchi mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya na waziri wa mambo ya nje wa Ureno Bw. Luis Amado, tarehe 19 baada ya kukutana na Bi. Condoleezza Rice kwenye mkutano na waandishi wa habari alisema, mkutano huo wa pande nne umeitishwa kwa pendekezo la rais George Bush. Bi. Condoleezza Rice alisisitiza kuwa kuitisha mkutano huo kulihitaji maandalizi mengi. Alisema, "Ni lazima tuhakikishe kila kazi iwe tayari vya kutosha kabla ya kufanyika, kwa sababu hatutaki kuona tena matokeo mabaya ya mazungumzo."

Jambo linalostahili kuzingatiwa ni kuwa, katika siku ya kufanyika kwa mkutano huo, Marekani, Russia na Umoja wa Ulaya zilitoa taarifa za kuunga mkono msimamo wa mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Mahmoud Abbas. Bi. Condoleezza Rice alipozungumza na waandishi wa habari alisema, Bw. Mahmoud Abbas ni kiongozi aliyechaguliwa na wananchi wa Palestina, Marekani inamchukulia kuwa ni mwenzi mzuri na inafurahia kuwasiliana naye. Anaona kuwa msimamo wa kundi la Hamas wa kukataa kutambua haki ya kuwepo kwa Israel kunazuia mazungumzo ya amani. Waziri wa mambo ya nje wa Ureno Bw. Luis Amado pia alisema, kama kundi la Hamas halitabadilisha msimamo wake basi Umoja wa Ulaya hautaanzisha uhusiano mpya na kundi hilo. Waziri wa mambo ya nje wa Russia pia alisema Russia inamwunga mkono mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Mahmoud Abbas aliyechaguliwa na watu wa Palestina.

Ingawa pande zote tatu za Marekani, Russia na Umoja wa Ulaya zinachukua msimamo wa kulitenga kundi la Hamas, lakini mkutano huo umetoa ahadi ya kuwasaidia watu wa Palestina waliopo katika ukanda wa Gaza. Kabla ya hapo, mashirika kadhaa ya kutoa misaada yaliwahi kutaka jumuyia ya kimataifa ilegeze vikwazo vya kibiashara dhidi ya ukanda wa Gaza, kwa sababu vikwazo hivyo vinafanya maisha ya wakazi wa Gaza yawe magumu.

Hapo awali mazungumzo ya pande nne kuhusu suala la Mashariki ya Kati yalipangwa kufanyika tarehe 6, lakini tarehe 14 Juni baada ya kundi la Hamas kudhibiti sehemu ya Gaza, mazungumzo hayo yalilazimika kuahirishwa, mkutano huo ulifanyika tarehe 19 katika hali mpya kabisa. Wachambuzi wanaona kuwa baada ya Hamas kukalia Gaza hali ya kisiasa imebadilika kabisa, tokea hapo itakuwa ni vigumu zaidi kwa amani kupatikana. Lakini bila kushiriki kwa Hamas na bila kutatua mgogoro wa ndani ya Palestina, hata mikutano ya kimataifa au mazungumzo ya pande nne vyote havitakuwa na matokeo ya kuridhisha.

Idhaa ya kiswahili 2007-7-20