Kundi la Taleban liliwateka nyara wakorea hao tarehe 19 alasiri katika mkoa wa Ghazni ulioko katikati ya nchi hiyo, mwanzoni kundi hilo liliitaka Korea ya Kusini iondoe jeshi lake kutoka nchini Afganistan, na baadaye iliitaka serikali ya Afghanistan iwaachie huru wanachama 23 wa Taleban wanaoshikiliwa na serikali na kutishia kuwaua mateka hao saa 1 jioni ya tarehe 22 kama matakwa ya kundi hilo hayatatimizwa. Naibu waziri wa mambo ya nje na biashara wa Korea ya Kusini Bw. Cho Jung-pyo aliwasili Afghanistan tarehe 22 kushughulikia tukio hilo. Msemaji wa wizara hiyo alisema, serikali ya Korea ya Kusini inajitahidi kuwasiliana na kundi la Taleban kwa njia mbalimbali, maofisa wa Afghanistan na wazee wa makabila wa nchi hiyo pia wamewasiliana na kundi hilo ili kutafuta ufumbuzi wa kuwaachia mateka wakiwa salama. Jeshi la usalama la Afghanistan na jeshi la Marekani nchini humo yameizingira sehemu ambayo mateka wa Korea ya Kusini wanashikiliwa, lakini bado hayajaanza mashambulizi.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-Moon tarehe 21 alitoa taarifa kupitia msemaji wake akiitaka serikali ya Afghanistan ifanye juhudi zote ili kuhakikisha mateka hao wanaachiwa huru mapema. Taarifa hiyo inasema, Bw. Ban Ki-moon alimpigia simu rais Hamid Karzai wa Afganistan, rais Karzai alisema anashiriki moja kwa moja kwenye shughuli za kuwaokoa mateka, na serikali ya Afghanistan imeunda kikundi cha wataalamu ili kushughulikia tukio hilo.
Kutokana na hali ya usalama nchini Afghanistan kuzidi kuwa mbaya, mwaka huu matukio ya utekaji nyara yanayofanywa na kundi la Taleban yanatokea mfululizo. Wachambuzi wanaona kuwa, kwa kuwa kundi hilo haliwezi kupambana moja kwa moja na jeshi la serikali ya nchi hiyo na majeshi ya kulinda usalama ya kimataifa nchini humo, linajitahidi kuvunja nguvu ya kupambana na ugaidi na kuharibu mchakato wa ukarabati wa Afghanistan kwa njia zozote ikiwemo utekaji nyara. Lakini kutokana na vizuizi mbalimbali, hali ya mvutano huo bado itaendelea kuwepo.
Kwanza matukio hayo yameifanya serikali ya Karzai ikabiliwe na shinikizo kubwa kutoka nchini na kutoka kwa jumuiya ya kimataifa. Baadhi ya watu wanaona kuwa, serikali haipaswi kufanya usuluhishi na magaidi, kwa upande mwingine, bunge la Afghanistan linaitaka serikali ifanye mazungumzo na kundi la Taleban. Hali hiyo imeathiri moja kwa moja kazi ya utungaji wa sera za usalama za nchi hiyo.
Pili, kufufuka kwa nguvu ya Taleban kumedhirinisha kuwa, mbinu ya kijeshi peke yake haiweza kutatua kikamilifu suala la usalama nchini Afghanistan.
Mwishowe kutokana na kuwa hali ya usalama ya nchi hiyo inazidi kuwa mbaya, ahadi za jumuiya ya kimataifa hazijatimizwa na mdogo chini wa serikali ya nchi hiyo, mchakato wa ukarabati wa Afghanistan hivi sasa unaendelea polepole. Hali hiyo imesababisha kutoboreshwa kwa maisha ya watu wa nchi hiyo na kuathiri moja kwa moja uungaji mkono wao kwa serikali. Aidha, mazingira mabaya ya kiuchumi na kijamii yametoa fursa ya kuendelea kwa shughuli za dawa za kulevya, na shughuli hizo zimekuwa chanzo kikubwa cha fedha kwa makundi yanayoipinga serikali. Mzunguko mbaya kama huo ukiendelea kuwepo, unaleta wasiwasi mkubwa kwa hali ya usalama na ya kisiasa nchini humo katika siku za baadaye.
|