Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-24 14:57:27    
Mikoa ya magharibi ya China yatafuta ushirikiano katika maonesho ya kimataifa ya sayansi na teknolojia ya Beijing

cri

Maonesho ya kimataifa ya shughuli za sayansi na teknolojia ya Beijing yanayofanyika kila mwaka, si kama tu ni jukwaa kwa viwanda vyenye teknolojia mpya na hali ya juu vya China na nchi za nje kuonesha bidhaa mpya kabisa za sayansi na teknolojia, bali pia yametoa fursa kwa mikoa ya magharibi ya China kuonesha shughuli zenye umaalum wa hali ya mikoa ya sehemu ya magharibi, maliasili zenye nguvu za ushindani na kutoa matangazo na kuvutia wafanyabiashara. Kwenye maonesho ya 10 ya shughuli za sayansi na teknolojia ya Beijing yaliyofanyika mwezi Mei, wajumbe kutoka mikoa ya magharibi ya China sio tu walileta bidhaa mpya za sayansi na teknolojia, bali pia waliweka mkazo katika kufanya ushirikiano na mawasiliano kati yao na makampuni ya nchini na ya nchi za nje.

Ujumbe kutoka nchi na sehemu zaidi ya 30 duniani na makampuni karibu 2,000 ya nchini na nchi za nje yalishiriki kwenye maonesho ya 10 ya shughuli za sayansi na teknolojia ya Beijing. Mikoa na miji zaidi ya 20 ya China ilishiriki kwenye maonesho hayo, miongoni mwa makampuni hayo karibu nusu yalitoka kwenye sehemu za magharibi. Ujumbe wa sehemu za magharibi si kama tu umeleta bidhaa mpya kabisa za sayansi na teknolojia, bidhaa zenye umaalum wa kienyeji na miradi yenye nguvu za ushindani, bali pia ulifanya shughuli mbalimbali za kutoa matangazo ya bidhaa zao na kuvutia wafanyabiashara. Kwenye maonesho hayo, mkuu wa mkoa wa Gansu wa China, Bw. Xu Shousheng alisema,

"Mkoa wa Gansu unatilia maanani sana maonesho ya shughuli za sayansi na teknolojia ya Beijing. Gansu ni mkoa wa ndani, hivyo kiwango cha mageuzi na ufunguaji mlango na maendeleo ya soko kiko nyuma kuliko Beijing na mikoa mingine, kwa hiyo serikali ya mkoa imethibitisha kuwa inapaswa kutumia fursa hii kuitangaza na kuijulisha Gansu, ili marafiki wengi zaidi wa nchini na nchi za nje waufahamu, na kuuendeleza na kuujenga kwa pamoja mkoa wa Gansu."

Mkoa wa Gansu uko katika kaskazini magharibi mwa China, njia maarufu ya hariri inapita mkoa huo. Baada ya mkakati wa kuendeleza sehemu ya magharibi kuanza kutekelezwa, uchumi wa mkoa wa Gansu umeendelezwa kwa kasi. Ili kuharakisha hatua za kufungua mlango, na kuharakisha maendeleo ya sayansi na teknolojia na marekebisho ya miundo ya shughuli, kuanzia mwaka 2000 mkoa wa Gansu ulianza kushiriki kwenye maonesho ya sayansi na teknolojia ya Beijing. Hivi sasa, kwa kupitia maonesho hayo Gansu imeanzisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na nchi na sehemu zaidi ya 130 duniani.

Imefahamika kuwa kwenye maonesho ya mwaka huu, Gansu ilileta bidhaa zaidi ya 200 ya sayansi na teknolojia, ambazo zinahusika na teknolojia ya safari za anga ya juu, bidhaa za kibaiolojia, kilimo cha sehemu kavu, maumbile ya mbuga na udhibiti wa hali ya jangwa, na baadhi ya matokeo ya utafiti wa kisanyasi na kiteknolojia yamefikia kiwango cha juu cha kimataifa. Mkoa wa Gansu ulisaini miradi 32 kwenye maonesho hayo, ambayo thamani yake ilifikia Yuan za RMB zaidi ya bilioni 3.4, na utekelezaji wa miradi hiyo utachangia kusukuma mbele maendeleo ya uchumi wa mkoa huo.

Kwenye maonesho ya 10 ya sayansi na teknolojia ya Beijing, eneo la maonesho ya mkoa unaojiendesha wa kabila la Wazhuang wa Guangxi China, lilikuwa moja ya sehemu zilizovutia watu wengi kabisa. Bidhaa zenye umaalum zilizotolewa na mkoa wa Guangxi kama vile vinywaji vya golden camellia, vipodozi vilivyotengenezwa kwa vitu asilia, dawa asilia zinazosaidia afya na vidani vya lulu zilivutia watu wengi. Meneja mkuu wa kampuni ya lulu na vito za Yongming ya Nanning mkoani Guangxi Bw. Ou Qizhen alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, walishiriki maonesho hayo kwa miaka 7 na 8 hivi, na bidhaa zao za lulu na vito zinakaribishwa sana. Akisema kwa fahari:

"Tumeleta lulu za Nan zenye sifa nzuri kabisa duniani, ambazo zinazalishwa huko Hepu mkoani Guangxi. Kampuni ya lulu ya Yongming inatawala soko mkoani Guangxi. Kupitia maonesho hayo, wateja wengi waliagiza bidhaa zetu, na wafanyabiashara wa soko kubwa la uuzaji wa lulu wanafanya mazungumzo nasi."

Wakati huohuo ili kuhimiza viwanda muhimu kuingiza teknolojia, kujifunza na kufanya uvumbuzi, mkoa wa Guangxi unapanua njia ya ushirikiano wa sayansi na teknolojia kati ya makampuni ya Guangxi na vyuo vikuu vya Beijing kupitia maonesho hayo. Hivi sasa vyuo vikuu vingi vya Beijing vimefanya utafiti wa sayansi na teknolojia katika raslimali za madini, sekta za vipuri vya magari, nishati ya viumbe na nyinginezo kutokana na mahitaji ya mkoani Guangxi. Katibu mkuu wa serikali ya mkoa unaojiendesha wa kabila la Wazhuang wa Guangxi Bw. Song Xiaotian alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema, anatumai kuwa makampuni na viwanda vya Guangxi na vyuo vikuu vya Beijing vitatumia nguvu na hali maalumu za kila upande kupanua sekta za ushirikiano, kwa kupitia njia za kuhamisha matokeo ya utafiti wa sayansi na teknolojia, kutoa ruhusa ya kutumia teknolojia, kufanya utafiti na uendelezaji kwa ushirikiano na kuanzisha viwanda kwa ushirikiano. Alisema:

"Mkoa wa Guangxi ukitaka kuharakisha maendeleo ni lazima utegemee njia za sayansi na teknolojia. Tunaona kuwa vyuo vikuu vingi vya Beijing vinaweza kuusaidia. Beijing ina vyuo vikuu vingi maarufu, ambavyo vina wataalamu na watu wenye ujuzi wa sekta mbalimbali. Mara hii tumekuja kujifunza, hii ina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya mkoa wetu Guangxi."

Mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uygur ulioko kaskazini magharibi mwa China ni mkoa wenye eneo kubwa kabisa nchini China, pia ni sehemu wanakoishi watu wa makabila madogomadogo, ambao wanafuata mila na desturi za kikabila. Mkoa huo una jangwa kubwa na mbuga mzuri, tena una nishati ya upepo ya kutosha. Kwenye maonesho ya mwaka huu, ujumbe wa Xinjiang uliagiza mabanda 9, na bidhaa kwenye maonesho ni pamoja na mifano ya mtambo mkubwa wa kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo, bidhaa za sayansi na teknolojia za kiviumbe na bidhaa nyingi za mitambo.

Wataalamu wanasema maonesho ya sayansi na teknolojia ya Beijing yametoa fursa nzuri kwa mikoa ya magharibi ya China kufanya mawasiliano na ushirikiano na nje. Kwa kutumia fursa hiyo, mikoa mbalimbali ya magharibi ilifanya juhudi kutafuta ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika uchumi na sayansi na teknolojia, na imepata matokeo mazuri. Hayo yote yatahimiza maendeleo ya mambo ya uchumi, sayansi na teknolojia ya sehemu za magharibi, na kutimiza kazi ya kuinua kiwango cha viwanda na marekebisho ya miundo.

Idhaa ya kiswahili 2007-07-24