Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-24 15:10:38    
Barua 0722

cri

Msikilizaji wetu Mutanda Ayubu Shariff wa Bungoma Kenya ametuletea barua pepe akisema, angependa kututumia salamu kutoka kwa jamii yake pamoja na kwa wasikilizaji wengine kutoka huko Bungoma Kenya. Anasema huko Bungoma Kenya, anaendelea kutupata hewani bila shida yoyote. Lakini analalamika akisema anaona kama muda wa kipindi cha sanduku la barua ni mfupi. Vilevile anashangaa kuwa hapo nyuma kidogo kulikuwa na barua pamoja na mashairi ambayo ametutumia lakini hayajasomwa. Vilevile amepokea barua kutoka kwa Bw. Ras Franz Manko Ngogo akisema ni muda sasa tangu aandike barua kwa Idhaa ya Kiswahili kwa Radio China kimataifa lakini mpaka sasa bado haijasomwa. Kwa hivyo anauliza, tatizo linaweza kuwa wapi? Je wasikilizaji labda hawaandiki barua nzuri, au waandikaji na wasomaji wa barua hizo wamepungua?

Lakini hata hivyo anafurahia jambo moja kutoka kwa Bw Ngogo kuwa kwa sasa ana uwezo wa kutuma barua pepe, hata kama ni mara moja kwa mwezi au wiki. Bila kusahau jambo hili wakati alitembelea mji mkuu wa Kenya aliweza kufuatilia vipindi vizuri na kupata kujua yote ni shwari kabisa. Lakini vilevile anasema kama kuna uwezekano wa kuwa na kipindi kama vile SAUTI ya wasikilizaji, itakuwa vizuri sana.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Bw Mutanda Ayubu Shariff kwa barua yake yenye maoni na maswali. Kwanza tunafurahi sana kusikia kuwa mnafuatilia matangazo yetu, na hata mnapenda kusikia barua zenu zikisomwa hewani. Ni kweli katika siku chache zilizopita kipindi cha sanduku la barua hakikupata barua nyingi. Ingawa mara kwa mara tunapata barua kutoka kwa wasikilizaji wetu, lakini mara nyingi barua hizi zinakuwa na kadi za salamu kutoka kwa wasikilizaji. Kuna wengine ambao wanatuandikia barua, lakini barua zao zinakuwa ni fupi kiasi kwamba hatuwezi kuzisoma kwenye kipindi hiki. Na kuhusu barua kutoka kwa Bw Franz Manko Ngogo, kweli na sisi tulikuwa tunashangaa ni kwanini hatujapata barua kutoka kwake kwa muda mrefu, lakini tunafahamu kuwa amewahi kutuma ujumbe kwenye simu ya mkononi kwa mfanyakazi wa idhaa yetu. Lakini wiki iliyopita kwenye kipindi hiki tulipata barua kutoka kwa Bw Ngogo na msikilizaji mwingine wa Kemogemba na tulizisoma hewani.

Hata hivyo tunaomba mkumbuke kuwa mawasiliano kwa njia ya barua yanapitia mikono mingi, barua ikitumwa kutoka Kenya au Tanzania, inapitia mikono mingi na kuchukua siku nyingi hadi kutufikia. Kwa hiyo kuchukua muda mrefu kabla ya kutufikia ni jambo la kawaida kabisa. Lakini tunapenda kuwahakikishia wasikilizaji wetu kuwa, barua zenu zote mnazotutumia zinazotufikia tunazithamini sana na tunahakikisha kuwa tunazisoma. Mnafahamu kuwa kila tukiona barua zenye maoni na mapendekezo au mashairi tulizotumiwa na wasikilizaji wetu tunasoma kwa furaha, hatuwezi kufanya uzembe. Maoni ya Bwana Mutanda ni mazuri, ambayo yanatukumbusha tusisahau wasikilizaji wetu wakati wowote, kwani wasikilizaji wetu wanatufuatilia kwa makini. Ni matumaini yetu kuwa, wasikilizaji wetu wengi zaidi watatuletea barua na kutoa maoni na mapendekekezo kwa makini juu ya matangazo ytu ili kutusaidia kuandaa vizuri matangazo yetu na kuwafurahisha wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Mwidadi Hassan wa Kilifi sanduku la Posta 271 nchini Kenya ametuletea barua ambayo ameanza kutushukuru kwa zawadi za kalenda, picha za aina mbalimbali na kadi nyingi za salamu alizopata. Pia anatupa pongezi kwa ajili ya kipindi cha Chemsha Bongo, kwani anasema alikifuatilia sana lakini kwa sababu kadhaa hakuweza kuwa mshindi. Pia anasema siyo rahisi kwa mtu anayetuma majibu yake kwa njia ya Posta kuwa mshindi kwani kutuma barua kutoka Kilifi mpaka China inachukua zaidi ya miezi miwili, hivyo barua ikifika shindano linakuwa limekwisha.

Sababu nyingine iliyomfanya msikilizaji wetu huyu ashindwe kushiriki kwenye chemsha bongo, ni muda mrefu uliopo kati ya kutuma barua na kuzipata. Anasema barua zetu ambazo huzituma kwa wasikilizaji wetu zikiwa na maswali ya chemsha bongo huwa zinachelewa kumfikia, na anapozipata muda wa chemsha bongo unakuwa umepita. Anaendelea kusema kuwa ana uhakika kuwa alijibu maswali vizuri sana, lakini majibu yake yalichelewa kutufikia.

Kwa wale wanatumia barua pepe au njia nyingine ndiyo wanaoshinda, kwani majibu yao hufika mapema sana kuliko ya kwao. Hivyo anasema kama tukiwatumia chemsha bongo tuzingatie njia hizi mbili kwani kuna malalamiko mengi. Kwa upande wa kadi za salamu anasema kadi za salamu zipewe nafasi kubwa kwani nazo kufika huku zinachukua muda ikiwezekana zisomwe mara mbili ili kutoa muda wa kadi nyingine ziweze kufika.

Pia anasema kwa kuwavutia mashabiki wa salamu tuwe na zawadi ya kila wiki kwa anayetuma kadi nyingi katika wiki moja. Kila Jumapili kuwe na mshindi tutakayempa zawadi nzuri itakayomsaidia kimaisha kama vile China inavyoyasaidia mataifa mbalimbali. Mwisho anasema kwa kufanya hivyo watu wengi watashiriki na kadi nyingi sana zitatumwa japo gharama ya kutuma kadi ni kubwa.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Bw Mwidadi Hassani kwa Barua yake. Kwa kweli tunapenda wasikilizaji wetu waelewe kuwa dosari ya kuchelewa kwa mawasiliano kati yetu hatuifurahii, lakini iko nje ya uwezo wetu. Na kwa upande wa gharama za kutuma barua kwa wasikilizaji wetu, tumejaribu kuweka utaratibu wa kuwapatia wasikilizaji wetu bahasha ambazo zimelipiwa gharama za stempu, tunatumai kuwa Posta nyingi zitaendelea kutambua bahasha za namna hiyo. Barua zote ambazo mnazotutumia iwe ni kwa njia ya posta au barua pepe, kwetu zote zina uzito sawa na zote tunazisoma bila kujali njia iliyotumiwa kuzifikisha. Na kuhusu wasikilizaji wanaotutumia barua pepe ni kweli kuwa barua pepe zinatufikia haraka sana, zenyewe hazina kuchelewa kama ilivyo kwa barua za kawaida. Lakini hii haina maana kuwa tunatoa kipaumbele kwa barua pepe kuliko barua za kawaida, kwetu zote ni sawa kabisa. Na ushindi kwenye shindano la chemsha bongo unategemea majibu sahihi, lakini hautegemei njia iliyotumiwa kutuma majibu, kwa hiyo tunawaomba wasikilizaji wetu msio na nafasi ya kutuandikia barua pepe msiwe na hofu hata kidogo.

Msikilizaji wetu mwingine T.S. Amooti wa sanduku la Posta 114 Kasese nchini Uganda, yeye kwenye barua yake anasema ana furaha kutuandikia barua kwa mara nyingine kwa lengo la kutaka kutuambia kuwa kuanzia mwezi wa tatu matangazo ya Radio China Kimataifa yamekuwa hayasikiki vizuri huko kwao nchini Uganda. Pamoja na hayo anaomba tumtafutie marafiki wa kalamu nchini China na pia tukiweza tumtumie vitabu vya lugha ya Kichina.

Idhaa ya kiswahili 2007-07-24