Rais Omar Al Bashir wa Sudan kuanzia tarehe 21 hadi 23 Julai alifanya ukaguzi kwenye sehemu ya Darfur, magharibi mwa Sudan, na kufanya mazungumzo na mawaziri wa serikali na maofisa wenyeji kuhusu namna ya kutatua suala la Darfur. Ukaguzi na uchunguzi umethibitisha kwa mara nyingine tena kuwa, suala la Darfur haliwezi kutatuliwa bila kuzingatia maendeleo ya huko, na usalama na amani ni masharti ya lazima ya kuleta maendeleo kwenye sehemu hiyo.
Sehemu ya Darfur inakabiliwa na hali mbaya ya hewa, upungufu wa raslimali za kimaumbile kama vile maji na ardhi inayolimika, na hali duni ya matibabu, elimu na miundo mbinu, hivyo wakazi wa huko wanaishi maisha magumu. Kutokana na kupungua kwa mvua, hali ya jangwa ya sehemu hiyo imezidi kuwa mbaya, pamoja na kuongezeka kwa haraka kwa idadi ya watu, mazingira ya kuishi huko yanakabiliwa na shinikizo kubwa. Ili kugombea raslimali ya maji na ardhi, migongano kati ya makabila mbalimbali ya huko imeongezeka, na hatimaye kusababisha mgogoro mkubwa wa kijeshi na wimbi kubwa la wakimbizi mwaka 2003.
Rais Bashir alitangulia kukagua jimbo la Darfur Kusini lenye idadi kubwa zaidi ya watu katika sehemu ya Darfur. Tarehe 21 Julai kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Nyala, mji mkuu wa jimbo hilo rais Bashir aliwataka watu wa Darfur waungane na kusukuma mbele maendeleo ya huko. Alisema watu wote wanatakiwa kulinda amani na umoja ili kuweka mazingira ya kujenga miundo mbinu kama vile hospitali, barabara na mawasiliano ya simu. Pia aliyataka makundi ya upinzani yajiunge na mchakato wa amani ili kuanzisha harakati ya kujiendeleza na kufanya ukarabati kwenye sehemu ya huko.
Tarehe 22 rais Bashir aliendesha mkutano wa kamati ya mawaziri wa serikali ya Sudan huko Fashir, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini. Alisema katika safari yake ya kufanya ukaguzi ameona kuwa, sehemu nyingi za Darfur ina usalama na utulivu, habari zinazotolewa na vyombo vya habari vya nchi za magharibi haziambatani kabisa na ukweli wa mambo. Alisisitiza kuwa kutimiza amani, utulivu na maendeleo ni lengo la kwanza kwa serikali ya Sudan, na serikali ya Sudan itaunga mkono kikamilifu mpango wa maendeleo ya sehemu ya Darfur. Alisema serikali ya Sudan itaweka mkazo kusukuma mbele mchakato wa amani wa Darfur, mambo 3 yatakayowekwa mkazo ni kutekeleza makubaliano ya amani ya Darfur, kuwarejesha watu wasiokuwa na makazi nyumbani kwao na kuyasihi makundi ya upinzani yasiyosaini makubaliano ya amani yajiunge na mchakato wa amani.
Tarehe 23 rais Bashir alifanya ukaguzi katika jimbo la Darfur Magharibi, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika huko Juneina, mji mkuu wa jimbo hilo alisema kuwa, serikali ya Sudan si kama tu itatimiza maendeleo ya mijini, bali pia itahimiza maendeleo vijijini, na kuwa na usalama na amani ni masharti ya lazima ya kutimiza malengo hayo. Alizilaumu baadhi ya nchi za magharibi kwa kuwafarakanisha watu wa Darfur. Siku hiyo rais Bashir pia alikata utepe kwa ujenzi wa kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Juneina. Alisema baada ya ujenzi wa kiwanja hicho kukamilika, kiwanja hicho cha ndege si kama tu kitawahudumia wakazi wa huko, bali pia kitatoa huduma kwa watu wa nchi jirani.
Rais Bashir pia alifanya ukaguzi katika miji na vijiji vilivyoko pembezoni mwa eneo hilo, na kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na wajumbe wa wakimbizi na watu wa fani nyingine. Vyombo vya habari vya huko vimedhihirisha kuwa, kufanyika kwa mafanikio kwa ukaguzi wa siku tatu kwa rais Bashir kumeonesha vya kutosha kuwa, hali ya jumla ya Darfur ni tulivu na salama, na hii imeimarisha moyo wa watu wa Sudan wa kutimiza amani nchini humo.
Idhaa ya kiswahili 2007-07-25
|