Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-25 15:32:07    
Marekani na Iran zafanya mazungumzo ya ngazi ya kibalozi kwa mara ya pili

cri

Marekani na Iran tarehe 24 zilifanya mazungumzo ya ngazi ya kibalozi kwa mara ya pili kuhusu usalama wa Iraq mjini Baghdad. Mazungumzo ya mara ya kwanza yalifanyika tarehe 28 mwezi Mei.

Mazungumzo hayo yalifanyika katika makazi ya waziri mkuu wan chi hiyo yaliyoko kwenye sehemu ya kijani mjini Baghdad na yaliendeshwa na waziri mkuu wa Iraq Bw. Nouri Maliki. Balozi wa Marekani nchini Iraq Bw. Ryan Crocker, balozi wa Iran nchini Iraq Bw. Hassan Kazemi Qomi na waziri wa mambo ya nje wa Iraq Bw. Hoshyar Zebari walihudhuria mazungumzo hayo. Baada ya mazungumzo hayo Bw. Ryan Crocker alidokeza kuwa mazungumzo yalikuwa "magumu". Kwenye mazungumzo alishutumu Iran kutoa misaada ya silaha na mafunzo kwa watu wenye siasa kali. Anaona kuwa ingawa kwa maneno Iran inaeleza kuiunga mkono serikali ya Nouri Maliki lakini hali ilivyo ni kuwa "shughuli za watu wenye silaha wanaoungwa mkono na watu wa Iran zinaongezeka badala ya kupungua." Bw. Ryan Crocker alikanusha kuwa mazungumzo yamepata mafanikio yoyote. Lakini amethibitisha kuwa katika siku ya mazungumzo Marekani, Iran na Iraq zimekubaliana kuunda kamati ya usalama na kufanya mazungumzo kuhusu kurudisha usalama na utulivu nchini Iraq.

Tokea mwaka 1980 Marekani na Iran zilipovunja uhusiano wa kibalozi, nchi hizo mbili zimekuwa katika hali ya uhasama. Hivi sasa pande hizo mbili zina mgongano kuhusu suala la Iraq. Marekani inataka Iran isitie mkono wake kwenye mambo ya Iraq, na kusimamisha misaada yake ya kisilaha, kifedha, kimafunzo na kutuma watu wenye silaha kwa madhehebu ya Shia nchini Iraq, na Iran inataka Marekani iondoe jeshi lake kutoka Iraq. Tarehe 28 mwezi Mei Bw. Ryan Crocker na Hassan Kazemi Qomi walifanya mazungumzo ya kwanza kuhusu usalama wa Iraq. Ingawa pande mbili zilionesha msimamo wa kuunga mkono serikali ya Iraq na kukubali serikali hiyo itekeleze mamlaka yake yote, lakini tofauti kati yao hazikutatuliwa. Mabishano kati ya pande mbili yaliendelea hadi kwenye mazungumzo ya pili. Marekani inaona kuwa baada ya mazungumzo ya mara ya kwanza Iran inaendelea kuunga mkono vikosi vya madhehebu ya kidini kupambana na jeshi la Marekani. Tarehe 23 mwezi huu Bw. Crocker alitaka Iran isimamishe uungaji mkono kwa watu wenye silaha wa madhehebu ya Shia na kuishutumu Iran kwa kuhamasisha shughuli za kiugaidi nchini Iraq. Na Bw. Qomi aliishutumu Marekani kwa kutolisaidia jeshi la Iraq kwa silaha za kutosha, na kusema kwamba Iran inapenda kutoa mafunzo kwa jeshi la Iraq. Msemaji wa Iran tarehe 24 alisisitiza kuwa njia nzuri ya kutatua suala la usalama nchini Iraq ni kuuheshimu kikweli uhuru wa wananchi wa Iraq na kukabidhi haki ya kuamua mustakbali wa Iraq kwa watu wa Iraq.

Vyombo vya habari vinaona kuwa wakati Marekani na Iran zinapogongana kuhusu suala la usalama wa Iraq, serikali ya rais George Bush haina budi kuendelea na mawasiliano kati yake na Iran kutokana na hali inavyozidi kuwa mbaya nchini Iraq na shinikizo kutoka nchini Marekani. Kwa mujibu wa sheria iliyopitishwa na bunge la Marekani, mwezi Septemba mwaka huu serikali ya George Bush italazimika kutoa ripoti kuhusu hali ya Iraq, kwa hiyo serikali hiyo inatumai kuboresha hali ya nchi hiyo kabla ya mwezi huo. Kutokana na sababu hiyo rais George Bush aliamua kuendelea na mazungumzo na Iran baada ya kushauriana na Condoleezza Rice.

Wachambuzi wanaona kuwa ni vigumu kutatua tofauti kati ya Marekani na Iran na kuboresha hali mbaya ya Iraq kwa kufanya mazungumzo ya mara moja au mbili. Hata hivyo, mazungumzo hayo ya mara mbili yamevunja hali ya kutowasiliana kati ya pande mbili, na hakika yataleta maana kwa usalama wa Iraq na hata kwa usalama wa kikanda.

Idhaa ya kiswahili 2007-07-25