Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-26 16:35:02    
Ufundi wa watu wa kabila la wamiao mkoani Guizhou wa kuweka michoro kwenye vitambaa kwa kutumia nta

cri

Kuweka michoro kwenye vitambaa kwa kutumia nta, ni moja ya ufundi wa jadi wa kutengeneza vitu vya sanaa ya mikono nchini China, yaani kuweka michoro kwenye vitambaa kwa kutumia nta kwenye vitambaa vilivyofumwa kwa nyuzi asilia zilizotengenezwa kwa katani, hariri, pamba na sufu, halafu kuwekwa rangi. Sehemu zilizowekwa nta haziwezi kupata rangi, hivyo baada ya nta kuondolewa kutoka kwenye sehemu zilizowekwa kwenye kitambaa, sehemu iliyokuwa na nta inaonekana kama ni maua meupe yanayopendeza.

Katika sehemu ya kusini magharibi, hasa sehemu wanakoishi watu wa makabila madogo madogo mkoani Guizhou nchini China, ufundi wa kuweka michoro kwenye vitambaa kwa kutumia nta unarithiwa kizazi kwa kizazi. Kuweka michoro kwenye vitambaa kwa kutumia nta ni ufundi wanaostahili kuwa nao wanawake wa kabila la Wamiao wa mkoa wa Guizhou katika maisha yao. Wanawake wa kabila la wamiao wanaoishi kwenye wilaya ya Danzhai, ni hodari sana kuweka michoro kwenye vitambaa kwa kutumia nta. Bi. Wang Jing wa kampuni ya mavazi ya Zhuangding ya wilaya ya Danzhai alisema, michoro yote inayowekwa kwenye vitambaa inabuniwa na wanawake wenyewe. Alisema:

"Michoro hiyo yote inabuniwa na wanawake wa kabila la wamiao, hakuna mifano maalum, kama vile samaki mmoja anaweza kubuniwa michoro mia kadhaa."

Wilaya ya Danzhai mkoani Guizhou inajulikana kwa kuwa na wasanii wengi wa kuweka michoro kwenye vitambaa kwa kutumia nta. Msanii maarufu wa kuweka michoro kwenye vitambaa kwa kutumia nta wa wilaya hiyo Bwana Wang Ayong, aliwahi kwenda Marekani mara mbili kuonesha ustadi wake, na alisifiwa kuwa "msanii wa mashariki". Mwaka 1986 na 1988 msanii mwanamke Bi. Yang Fang alialikwa kufanya maonesho ya kuweka michoro kwenye vitambaa kwa kutumia nta mjini Hong Kong na Beijing. Hivi karibuni vitambaa kama hivyo vya wilaya ya Danzhai vilishiriki kwenye tamasha la pili la utamaduni wa makabila madogo madogo. Kwenye maonesho ya vitu vya urithi wa utamaduni usioonekana vya makabila madogo madogo, sehemu ya maonesho ya vitambaa vilivyowekwa michoro kwa kutumia nta vya wilaya ya Danzhai, ilivutia watazamaji wengi. Mtazamaji mmoja alisema:

"Nafurahi sana kuona ufundi huo, sijawahi kuona vitu vizuri vya sanaa kama hivi. Naona ni muhimu sana kurithi na kukuza vitu vya sanaa vya jadi."

Kwenye sehemu ya kuonesha vitambaa vilivyowekwa michoro kwa nta vya wilaya ya Danzhai, mwandishi wetu wa habari aligundua kuwa, wasanii wote hodari wa sanaa hiyo ni wanawake. Kutokana na desturi ya kabila la wamiao, wanawake wote wanawajibika kurithisha ufundi huo, mama anatakiwa kuwafundisha mabinti zake kuweka michoro kwenye vitambaa kwa kutumia nta. Hivyo wanawake wa kabila la wamiao wanatakiwa kujifunza ufundi huo walipokuwa watoto, wanafuma vitambaa, kutia rangi kwenye vitambaa na kuweka michoro kwa kutumia nta.

Ili kuhifadhi na kurithisha vizuri zaidi ufundi huo wa jadi, wilaya ya Danzhai ilianzisha shirikisho la kiraia la kuweka michoro kwenye vitambaa kwa kutumia nta na viwanda vya mavazi. Jukumu la shirikisho hilo ni kufanya utafiti kuhusu kazi ya kuweka michoro kwenye vitambaa kwa kutumia nta, na ufundi wa kutarizi vitambaa. Bi. Wang Jing kutoka kiwanda cha mavazi cha Danzhai alisema:

"Hivi sasa kuna watu wengi wanaojishughulisha na kazi hiyo nchini China, hivyo tunapaswa kufuatilia zaidi sifa ya kazi ili kuvifanya vitu hivyo vipendwe na watu wengi."

Naibu mkuu wa jumba la maonesho ya makabila madogo madogo ya China Bi. Wei Ronghui alisema, lengo kubwa la kufanya tamasha la utamaduni wa makabila madogo madogo ni kuwahimiza watu wote, jamii yote na sehemu za makabila madogo madogo kuhifadhi urithi wa utamaduni wao. Maonesho mengi katika tamasha hilo yalifanyika katika sehemu karibu na eneo la kibalozi la Beijing, kuonesha mavazi na ufundi wa kutengeneza mavazi hayo ya makabila madogo madogo. Bi. Wei Ronghui alisema, mwaka kesho jumba hilo litaendelea kufanya tamasha la utamaduni wa makabila madogo madogo. Akisema:

"Maonesho hayo yamevutia watazamaji wengi, ambao wengi wao wanataka kununua bidhaa. Lakini mara hii lengo letu kubwa ni kufanya maonesho bali siyo kuuza vitu, hivyo hatukuleta bidhaa nyingi kwa ajili ya kuuza. Mwaka kesho siku ya utamaduni wa makabila madogo madogo itaandaliwa vizuri zaidi."

Idhaa ya kiswahili 2007-07-26