Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-26 16:23:54    
Watu wa Korea ya Kusini waliotekwa nyara na Taliban wako hatarini

cri

Polisi wa mkoa wa Ghazni tarehe 25 walithibitisha kuwa mmoja kati ya watu 23 wa Korea ya Kusini waliotekwa nyara na kundi la Taliban wiki iliyopita aliuawa kando ya barabara baada ya kupigwa risasi, na wanadiplomasia wa nchi za magharibi walidokeza kuwa mateka wanane wameachiwa huru. Ingawa kuna habari nyingi tofauti kuhusu mateka hao wa Korea ya Kusini, lakini hali ilivyo ni kuwa bado wako hatarini.

Habari zinasema, mtu aliyeuawa alipigwa risasi nyingi kichwani na kifuani, alikutwa kando ya barabara katika mkoa wa Ghazni. Kabla ya hapo, msemaji wa Taliban Bw. Yousef Ahmadi alisema kundi la Taliban limemwua mtu huyo kutokana na kuwa serikali ya Afghanistan haikukidhi matakwa ya kubadilishana mateka. Habari nyingine zinasema mateka nane wa Korea ya Kusini, wanawake sita na wanaume wawili, wameachiwa huru, na wamehamishiwa kwenye kituo cha jeshi la Marekani kilichoko mkoani Ghazni, lakini habari hiyo bado haijathibitishwa na serikali ya Afghanistan.

Mateka wa Korea ya Kusini ni waumini wa dhehebu moja la Kikristo, walitekwa nyara wiki iliyopita walipokuwa wakisafiri kwa basi lililokuwa linapita mkoani Ghazni kuelekea mji wa Kabul, mji mkuu wa Afghanistan. Habari zinasema watu hao walikuwa nchini Afghanistan kwa ajili ya kuwasaidia watu wa Afghanistan walioathirika na vurugu za vita. Baada ya kutekwa nyara tarehe 18, kundi la Taliban lilitaka Korea ya Kusini iondoe jeshi lake kutoka Afghanistan, na baadaye lilitaka kubadilishana watu hao na watu waliotekwa na serikali ya Afghanistan, na kutishia kwamba kama matakwa yao hayatatimizwa basi wataendelea kuwaua kwa mfululizo. Baadaye kundi la Taliban lilirefusha mara tatu muda wa kuwaua mateka hao na kauli ya mwisho ya kutaka kuwaua ilikuwa ni alfajiri ya Alhamisi.

Baada ya kutokea kwa tukio hilo, balozi wa Korea ya Kusini nchini Afghanistan aliongozana na maofisa wa serikali ya Afghanistan kwenda mkoani Ghazni kuanza shughuli za kuwaokoa. Wakati huo serikali ya Korea ya Kusini ilituma mjumbe kwenda nchini Afghanistan kufanya juhudi za uokoaji akitumai mateka hao watasalimishwa kwa njia ya mazungumzo. Lakini kadiri mazungumzo yanavyozidi kuwa magumu, ndivyo mateka hao 23 wanavyozidi kuwa hatarini. Hivi sasa serikali ya Afghanistan na Korea ya Kusini zinajaribu kufanya majadiliano kupitia wazee wa makabila ya Afghanistan ili kukwepa mauaji. Kuhusu majadiliano, kuna habari zinazosema Korea ya Kusini italipa dola nyingi za Kimarekani kwa Taliban ili mateka hao waachiwe, lakini habari hiyo bado haijathibitishwa na serikali ya Afghanistan. Wizara ya mambo ya nje ya Korea ya Kusini imetoa taarifa ikiwataka watu wa Korea ya Kusini 200 waondoke Afghanistan mapema iwezekanavyo. Rais wa Korea ya Kusini Bw. Roh Moo-Hyun tarehe 24 aliwataka wananchi wa nchi yake watulie na kusema serikali itafanya kila iwezalo kuwaokoa.

Katika siku za karibuni matukio mengi ya utekeji nyara yametokea nchini Afghanistan, na wengi wa wanaotekwa ni waandishi wa habari na wageni wanaotoa huduma kwa jamii. Baada ya Wakorea Kusini kutekwa nyara, serikali ya Afghanistan imewaasa wageni wasiondoke Kabul bila kutoa ombi kabla ya saa 24 na kupata ruhusa.

Wachambuzi wanaona kuwa kutekwa nyara kwa wageni kumeonesha kuwa hali ya usalama nchini Afghanistan inazidi kuwa mbaya. Kwa mujibu wa takwimu za jeshi la Marekani nchini Afghanistan zinasema mwaka huu matukio ya kigaidi nchini humo yameongezeka kwa mara mbili kuliko mwaka jana wakati kama huu. Kwa upande mwingine tukio hili limeonesha kuwa hatua ya serikali ya Afghanistan kuwaachia huru wanamgambo wa Taliban ili kumwokoa mwandishi wa habari wa Italia, sasa imeleta athari mbaya. Ni dhahiri kwamba baada ya Taliban kuonja utamu huo sasa inazidi kutaka mengine. Wanamgambo wa Taliban wanatumai kuwateka nyara watu wengi zaidi ili kushinikiza majeshi ya nchi za nje yaondoke nchini humo au kuwaokoa watu wa Taliban. Lakini kwa sababu majeshi ya nchi za nje yanatoka nchi nyingi za NATO, ni vigumu kuwa na msimamo wa namna moja, kwa hiyo matukio ya utekaji nyara kwa wageni ni kama mtihani mgumu kwa nchi za NATO katika kusawazisha misimamo.

Idhaa ya kiswahili 2007-07-26