Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-30 15:04:53    
Mwandishi wa vitabu ambaye pia ni askari polisi, Cao Naiqian

cri

Bw. Cao Naiqian mwenye umri wa miaka 59 ni askari polisi katika mji wa Datong mkoani Shanxi. Lakini tofauti na askari polisi wengine, yeye pia ni mwandishi mashuhuri wa vitabu. Vitabu vyake zaidi ya 30 vimetafsiriwa kwa lugha za kigeni na kusambazwa katika nchi za Japani, Marekani, Canada na Uswis. Mjumbe wa kamati ya waamuzi wa tuzo ya Nobel ya fasihi duniani Bw. Goran Malmqvist anaona kuwa Bw. Cao Naiqian ni mmoja kati ya waandishi wa vitabu wa China wenye matarajio na kupata tuzo ya Nobel.

Bw. Cao Naiqian alizaliwa katika kijiji cha Xiamayu mkoani Shanxi. Katika miaka ya 60 na 70 aliwahi kuwa mchimbaji wa makaa ya mawe na mpigaji ala katika kundi la wasanii, baadaye akawa askari polisi hadi sasa.

Bw. Cao Naiqian anaonekana kama ni mkulima, ni mtu mwenye kuvaa kizibao, viatu vya kitambaa na ana mivunjo mengi usoni.

Cao Naiqian alianza kuandika riwaya mwaka 1987, hadi sasa ameandika vitabu vyenye maneno karibu milioni moja. Mwanzo wake wa kuandika riwaya ulitokana na kushindana na rafiki yake mmoja. Rafiki yake alisema hana uwezo wa kuandika riwaya, lakini yeye hakukubali kabisa. Tokea hapo aliandikia riwaya ambayo ilichapishwa kwenye gazeti moja la mkoa. Baadaye aliandika riwaya kwa ajili ya jarida moja la fasihi la mjini Beijing, riwaya yake ilisomwa na mwandishi mmoja mkubwa wa vitabu. Mwandishi huyo wa vitabu alipenda sana makala aliyoandika na kutaka kumlea kifasihi. Hivyo ndivyo alivyoanza maisha ya uandishi.

Kitabu chake cha kwanza ni riwaya inayoeleza maisha yake na sufii mmoja wa dini ya Buddha. Jina la kitabu hicho kinaitwa "Upweke wa Sufii wa Buddha". Kuanzia umri wa miaka tisa Bw. Cao Naiqian aliishi katika hekalu moja chakavu, sufii mmoja aliyekuwa huko alikuwa mtu pekee wa kukaa naye. Wao walikuwa pamoja katika kucheza bao na kusoma. Bw. Cao Naiqian alisema alikuwa na bahati kuishi pamoja na sufii huyo.

"Nilipokuwa na umri wa miaka tisa nilianza kuishi katika hekalu moja chakavu, na niliishi huko miaka zaidi ya 40. katika hekalu hilo kuna sufii mmoja, katika kitabu changu sikueleza mambo ya dini, ni mambo kati yetu ambayo yalinisukuma niyaeleze."

Bw. Cao Naiqian alisema, sufii huyo alikuwa ni rafiki yake pekee, alimfundisha kusoma na kumwelezea kuhusu msahafu, ingawa mara nyingi hakufahamu. Jinsi anavyoongea Bw. Cao Naiqian ni kama naye alikuwa na maisha pamoja na sufii, kwamba anavyokaa kitako anainua kiuno kama sufii anapokuwa anaomba dua. Anaposindikiza mgeni na kuagana naye hukutanisha viganja vya mikono kifuani na kukutakia baraka mpaka unapotoweka machoni mwake.

Maisha ya miaka mingi akiwa pamoja na sufii katika hekalu pia yameathiri hulka yake, kwamba anaacha mambo yaendelee yenyewe bila kuyataka yafikie lengo fulani kwa lazima, anapuuza sifa na mali na kuridhika na maisha ya kawaida. Alisema yeye anaandika vitabu kwa ajili ya kueleza fikra zake, na hajali kama shirika fulani la uchapishaji litachapisha kitabu chake au la,, na vile vile hajali kitakachosemwa na wahakiki. Anapofahamu kuwa kuna baadhi ya wasomaji wanaopenda vitabu vyake anafurahi sana, na anapofahamu kuwa baadhi ya watu hawavifahamu vitabu vyake, pia anaendelea kuandika.

Hadi sasa Bw. Cao Naiqian amemaliza riwaya ndefu tatu na riwaya fupi kumi kadhaa, riwaya zote hizo zinatokana na maisha yake halisi. Kabla ya kuwa askari polisi aliwahi kuwa mchimba makaa ya mawe, maisha yake yalikuwa magumu sana. Kutokana na maisha ya wachimba makaa ya mawe aliandika kitabu chake kiitwacho "Dhahabu Nyeusi" kikieleza maisha ya uchimbaji makaa yalivyo magumu. Mwaka huu amemaliza kitabu chake kingine kiitwacho "Wakulima wa Kijiji cha Wenjiayao" kikieleza maisha duni ya wakulima katika sehemu alikoishi miaka 40 iliyopita. Bw. Cao Naiqian alisema bila kuwa na maisha halisi asingeweza kuandika kitabu.

"Vitabu vyangu vyote nimeviandika kutokana na maisha halisi, bila kuwa na maisha yenyewe sina uwezo wa kutunga. Siwezi kuandika kitabu fulani kwa kusikia tu habari fulani."

Kitabu chake cha "Wakulima wa Kijiji cha Wenjiayao" alimaliza kuandika miaka zaidi ya kumi iliyopita, lakini hakikupokelewa na shirika la uchapishaji mpaka mwaka huu. Lakini profesa wa Kichina wa Chuo Kikuu cha Uswis Bw. Goran Malmqvist anapenda sana riwaya zake, anaona vitabu vyake vinafaa kutafsiriwa. Kitabu cha "Wakulima wa Kijiji cha Wenjiayao" kimetafsiriwa na profesa huyo na kitachapishwa mwaka huu.

Hivi sasa Bw. Cao Naiqian anaandika riwaya moja ndefu inayomwelezea mama yake, kwa sasa iko nusu, kutokana na mpango atakamilisha riwaya hiyo kabla ya yeye kustaafu ili kukidhi matakwa yuake ya miaka mingi. Mama wa Cao Naiqian alikuwa ni mgonjwa wa kiakili, hakujiweza kimaisha. Ili kumtunza mama yake Bw. Cao Naiqian aliacha uandishi wake kwa miaka sita mpaka mama yake alipofariki dunia. Bw. Cao Naiqian ana masikitiko, na anataka kumkumbuka mama yake kwa kuandika kitabu na kumshukuru kwa wema wake. Alisema,

"Karibu nimemaliza nusu ya kitabu hiki, kitabu kizima kitakuwa na maneno laki nane hadi tano hivi. Wengine wanasema, kitabu kitakuwa kinene na kunishawishi nipunguze, mimi nasema sijali kama kitakubaliwa kuchapishwa, lakini nitakamilisha na kutimiza nia yangu."

Bw. Cao Naiqian alisema yeye ni mtu bahili, hataki kununua nguo za bei ghali, hataki kula chakula kinono, chakula anachopenda ni mbatata tu. Lakini ili aweze kuandika vitabu, yeye ni mkarimu wa kutumia pesa. Alisema,

"Sina tabia ya kutumia pesa nyingi, hii ni sare ya askari polisi niliyopewa. Lakini ninaponunua vitabu sijali natumia pesa kiasi gani. Mtu mmoja alitaka kununua vitabu vyangu kwa Yuan laki tatu lakini sikuuza. Sebule yengu ni mita za mraba 20, pande zote tatu ni rafu za vitabu toka chini mpaka juu, kuna jumla ya vitabu elfu tano hivi."

Bw. Cao Naiqian ni mmoja wa waandishi wa vitabu wanaotumia kompyuta kuandika vitabu. Mwanzoni mwa miaka ya 90 katika karne iliyopita katika kituo chake cha polisi kulikuwa hakuna kompyuta, yeye alinunua kompyuta moja kwa mishahara yake ya nusu mwaka. Amezoea kuamka saa tisa na robo usiku, na baada ya kuamka anaanza kuandika kila siku.

Idhaa ya kiswahili 2007-07-30