Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-30 19:07:24    
Umuhimu wa kupata ubingwa kwa timu ya Iraq ni mkubwa zaidi kuliko mchezo wa soka

cri

Katika fainali ya soka ya kombe la Asia la mwaka 2007 iliyofanyika tarehe 29 mwezi Julai mjini Jakarta Indonesia, timu ya Iraq iliishinda timu ya Saudi Arabia kwa bao moja kwa bila, na kupata ubingwa wa kombe la Asia katika historia, kwa kuishinda timu ya Saudi Arabia, ambayo ilipata ubingwa kwa mara tatu. Wapenzi wengi wa soka nchini Iraq bila kujali amri ya marufuku ya serikali na tishio la mashambulizi ya kigaidi, walimiminika barabarani wakiwa wamebeba bendera ya taifa huku wakiimba na kucheza ngoma. Vyombo vya habari vinaona kuwa ushindi wa timu ya soka ya Iraq ulileta furaha kubwa, moyo wa kujivunia na imani kwa Iraq inayokumbwa na maafa ya vita kwa miaka mingi, umuhimu wa ushindi huo umekuwa mkubwa zaidi kuliko mchezo wa soka.

Hii ni mara ya tatu mfululizo kwa timu ya soka ya Iraq kuingia kwenye nafasi nne za mwanzo katika mashindano makubwa. Kwenye michezo ya Olimpiki iliyofanyika mjini Athens mwaka 2004 timu ya Iraq ilichukua nafasi ya nne; kwenye michezo ya Asia iliyofanyika mjini Doha mwaka 2006 timu ya Iraq ilichukua nafasi ya pili, mafanikio hayo yanafanya watu kutoweza kabisa kuyahusisha na nchi moja inayokumbwa na migogoro ya kivita.

Timu ya soko ya Iraq iliyoshiriki kwenye mashindano ya soka imeundwa na wachezaji wa madhehebu ya ki-suni na ki-shia pamoja na wa Kurd. Wachezaji hao walishirikiana vizuri na kuondoa matatizo ya aina mbalimbali, hatimaye waliwashinda wapinzani wao wenye nguvu kubwa. Ushindi wa mchezo wa soka unafanya watu wa Iraq wasahau migongano ya madhehebu hayo ya kidini, wachezaji hao walinyanyua juu bendera ya taifa, huku wakikumbatiana, kurukaruka kwa furaha, na kulengwa na machozi ya furaha.

Vyombo vya habari vinaona kuwa umuhimu wa kupata ushindi kwa timu ya soka ya Iraq kwenye mashindano ya kombe la Asia ni mkubwa zaidi kuliko mchezo wa soka. Kwanza ushindi wa timu ya soka kwenye uwanja wa mpira umeleta furaha kubwa na imani, ambayo wairaq hawakuipata katika miaka ya karibuni; pili, katika mazingira, ambayo mapambano kati ya madhehebu ya kidini nchini Iraq yanapamba moto siku hadi siku, timu ya soka ya Iraq inachukuliwa kama ni alama ya umoja wa taifa. Ushindi wa timu ya soka ya Iraq pamoja na hali ya furaha ya watu, inaonesha kuwa watu wa Iraq wanaweza kutupilia mbali tofauti na migongano kati ya madhehebu ya kidini na kutimiza umoja na maafikiano. Au kwa msemo mwingine, kwa uchache kabisa ushindi wa timu ya soka ya Iraq unawafanya watu kuona mustakabali mzuri wa taifa lao. Lakini furaha na imani iliyoletwa na ushindi huo kwa watu wa Iraq ni ya muda mfupi, watu wa nchi hiyo hawana budi kukabiliana na ukweli wa hali ya kikatili ya nchini mwao.

Ili kuzuia kutokea kwa matukio ya kimabavu yanayozushwa na washabiki wa soka, idara ya usalama ya Iraq ilitoa amri ya marufuku ya kutoka nje kabla ya kuanza kwa mchezo wa fainali ya kombe la Asia, ikitangaza kufanya udhibiti mkali kuhusu magari na kupiga marufuku kuadhimisha kwa kupiga bunduki. Katika baadhi ya sehemu, viongozi wa dini wakitumia vipaza sauti waliwataka watu wajizuie na waache kufyatua risasi. Hata hivyo, watu wengi walikuwa bado wanafyatua risasi kuonesha furaha, ambapo hali hiyo ilisababisha vifo vya zaidi ya watu 7 na majeruhi kumi kadhaa.

Hali ya usalama nchini Iraq kwa sasa bado ni mbaya. Katika muda wa miaka minne iliyopita tangu kulipuka kwa vita ya Iraq, kila siku wakazi zaidi ya mia moja wanakufa au kujeruhiwa katika matukio mbalimbali ya nguvu ya kimabavu. Tarehe 25 mwezi Julai, timu ya Iraq ilipoishinda timu ya Korea ya kusini kwa penalti na kuingia fainali, mashabiki wengi wa soka nchini Iraq waliingia barabarani kufurahia. Lakini watu wenye msimamo wa siasa kali, waliwachukulia wakazi hao kama ni shabaha za kushambulia, matukio mawili ya milipuko yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 55 na wengine 135 kujeruhiwa. Hivi sasa mchakato wa usuluhisho wa kisiasa nchini Iraq umesimama kabisa, madhehebu ya Suni na Shia pamoja na wa-Kurd wamekuwa na migongano mingi na kutoaminiana kabisa. Matatizo hayo ya muda mrefu hayawezi kutatuliwa katika siku moja, hivyo watu wa Iraq sasa bado wako mbali sana na umoja na usuluhisho wa kweli wa taifa lao.