Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-31 14:07:41    
Sekta ya uchapishaji wa kitarakimu yapata maendeleo ya kasi nchini China

cri

 

Katika miaka ya hivi karibuni, sekta ya uchapishaji wa kitarakimu imepata maendeleo ya kasi nchini China. Kwa mujibu wa takwimu zisizokamilika, katika mwaka 2006 mapato ya sekta ya uchapishaji wa kitarakimu yalikuwa yuan bilioni 20. Matumizi ya teknolojia ya uchapishaji wa kitarakimu yamekuwa nguvu kubwa ya kusukuma mbele maendeleo ya sekta za habari na uchapishaji.

Hivi sasa kutokana pilikapilika nyingi katika kazi na maisha, watu wachache zaidi wanakwenda dukani kununua vitabu na magazeti. Watu wengi wanasoma magazeti na vitabu kwenye mtandao wa Internet au kwenye simu za mkononi. Hivi sasa vitabu na magazeti kwenye vyombo vya elektroniki yanafurahiwa na Wachina wengi zaidi hasa vijana. Bi. Chen Yi mwenye umri wa miaka 24 anafanya kazi katika kampuni moja ya teknolojia ya mawasiliano IT mjini Beijing. Alimwambia mwandishi wetu wa habari akisema,

"Napenda kusoma vitabu, ninachukua vitabu kutoka kwenye mtandao wa Internet mara kwa mara. Vitabu vya karatasi ni vizito, lakini vitabu vilivyochukuliwa kutoka kwenye mtandao wa Internet ni vyepesi ambavyo vinaweza kuwekwa kwenye simu ya mkononi, hivyo ni rahisi kuvisoma."

Bi. Chen Yi alisema mara kwa mara anasafiri kwenda kwenye miji mingine kwa garimoshi kutokana na kazi yake. Kabla ya kufunga safari, anachukua vitabu kadhaa kutoka kwenye mtandao wa Internet na kuviweka kwenye simu yake ya mkononi, ili kuvisoma akiwa safarini. Habari zinasema uchapishaji wa kitarakimu unamaanisha uchapishaji na uuzaji wa vitabu kupitia mtandao wa Internet. Hivi sasa China imetoa karibu aina laki 3 za vinavyoweza kupatikana kwenye vyombo vya elektroniki ambavyo vinachukua nafasi ya kwanza duniani, na mapato ya uuzaji wa vitabu na magazeti yaliyochapishwa yanaongezeka kwa kasi.

Kampuni ya Fangzheng iliyoanza kujishughulisha na uchapishaji wa kitarakimu mwaka 2000, ni kampuni kubwa zaidi ya sekta ya uchapishaji wa kitarakimu nchini China. Kampuni hiyo inayapatia makampuni ya uchapishaji na waandishi huduma za teknolojia ya kulinda hakimiliki ya uchapishaji wa kitarakimu ya Apabi na teknolojia ya kushughulikia nyaraka zenye hakimiliki. Naibu mkuu wa kampuni ya Fangzheng Bw. Fang Zhonghua alipohojiwa na waandishi wa habari alisema,

"Lengo la kampuni yetu ni kuyapatia makampuni ya uchapishaji huduma ya teknolojia ya kisasa ya uchapishaji wa kitarakimu. Mfumo wa uchapishaji wa kitarakimu unaweza kumsaidia mtu yeyote kupata kwa urahisi vitabu na magazeti kwenye vyombo vya elektroniki kwa urahisi katika wakati wowote na sehemu yoyote."

Ili kuwasaidia wasomaji wapate vitabu na magazeti wanayopenda kwenye mtandao wa Internet, mwaka jana kampuni ya Fangzheng ilianzisha mfumo wa magazeti na tovuti moja inayotoa aina laki kadhaa za vitabu na magazeti yaliyochapishwa kitarakimu. Wasomaji wanaweza kusoma na kununua vitabu na magazeti wanayopenda.

Ingawa sekta ya uchapishaji wa kitarakimu imepata maendeleo ya haraka nchini China, lakini bado iko nyuma kuliko nchi zilizoendelea. Hakimiliki ya uchapishaji wa kitarakimu na usimamizi wa uchapishaji wa kitarakimu ni masuala muhimu yanayozuia maendeleo ya sekta hiyo. Hivi karibuni mkutano wa sekta ya uchapishaji wa kitarakimu ulifanyika hapa mjini Beijing.

Kwenye mkutano huo naibu mkurugenzi wa idara ya habari na uchapishaji ya China Bw. Sun Shoushan alisema, China imeamua njia na malengo ya kimkakati ya maendeleo ya uchapishaji wa kitarakimu. Alisema,

"China inafanya juhudi kusukuma mbele uchapishaji wa kitarakimu, ili kueneza habari na vitabu kwenye msingi wa kulinda hakimiliki; kuharakisha kutunga vigezo muhimu vya sekta hiyo; kuongeza nguvu utafiti wa teknolojia, ili kupata maendeleo makubwa katika pande nyingi zikiwemo kulinda hakimiliki ya uchapishaji wa kitarakimu, teknoljia ya uchapishaji wa kitarakimu, diski zinazoweza kuhifadhi nyaraka nyingi na karatasi za zinazotumika katika uchapishaji wa kitarakimu."

Idadi ya wachina wanaotumia mtandao wa Internet inachukua nafasi ya pili duniani. Katika hali hiyo watu wengi wamebadilisha njia ya kusoma. Magazeti na vitabu vilivyowekwa kwenye mtandao wa Interent vina sifa kubwa za kipekee kuliko vitabu na magazeti ya karatasi. Kwa mfano picha, sauti na video vinaweza kuwekwa katika vitabu hivyo kwenye mtandao wa Internet; watu wanaweza kutafuta maeneo kwa urahisi kwenye vitabu hivyo; gharama za uchapishaji wa kitarakimu ni nafuu; na kusoma vitabu hivyo ni rahisi. Wafanyakazi wa makampuni ya magazeti wanaweza kubadilishana maoni na wasomaji kwa urahisi kupitia magazeti yaliyochapishwa kitarakimu. Hivyo mustakabali wa uchapishaji wa kitarakimu ni mzuri sana. Bw. Sun Shoushan ana matumaini makubwa kuhusu mustakabali wa sekta hiyo, alisema,

"Kutokana na uungaji mkono mkubwa wa serikali ya China, makampuni mengi ya teknolojia ya kitarakimu na uchapishaji yanafanya juhudi kushiriki kwenye sekta ya uchapishaji wa kitarakimu, hakika sekta hiyo itapata maendeleo ya haraka zaidi, na sekta za habari na uchapishaji za China pia zitastawi zaidi."

Alipendekeza kuwa makampuni ya teknolojia ya uchapishaji wa kitarakimu na makampuni yanayotoa na kuuza vitabu vya kitarakimu yanatakiwa kuimarisha zaidi mawasiliano kati yao, ili kuongeza uwezo wa usimamizi wa uchapishaji wa kitarakimu, kutoa huduma nyingi zaidi, na kuinua teknolojia ya uchapishaji wa kitarakimu na uwezo wa ushindani kwenye soko la kimataifa.