Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-31 15:06:12    
Barua 0729

cri

Msikilizaji wetu Fred Simiyu wa sanduku la posta 1962, Bungoma Kenya ametuletea barua akianza kwa salamu nyingi sana kutoka kwake na jamii yake, akitumai kuwa sisi tu wazima. Anasema angependa kuishukuru Radio China Kimataifa kwa kujitahidi kupeperusha matangazo yake kwa kupitia Shirika la utangazaji la Kenya KBC, kweli wasikilizaji wanapata matangazo yetu vyema sana. Na anawapongeza watangazaji kwa bidii zao kazini, anatushukuru sana kwa kumtumia kadi za salamu.

Lakini Bw Simiyu anasema anaona kuwa muda wa matangazo ya Radio China Kimataifa kwa kupitia Radio KBC ni mfupi sana, ingekuwa ni vyema sana kama muda huo ungeongezwa. Anasema ingekuwa vizuri pia kama matangazo ya FM huko Nairobi Kenya, yangeweza kusikika Kenya nzima ili wasikilizaji wanufaike zaidi.

Mwisho anaomba kama kuna uwezekano tuwafungulie wasikilizaji wetu vituo vya kukusanyia maoni na mapendekezo vijijini, ili wasikilizaji wa Radio China Kimataifa walioko vijijini ambao hawawezi kumudu gharama za mawasiliano waweze kupata urahisi wa kutoa maoni yao, anataka tukumbuke kuwa mteja ni mfalme.

Tunamshukuru sana Bw Fred Simiyu kwa barua yake na maoni na mapendekezo yake, kuhusu kuongezwa muda kwa matangazo yetu yanayopeperushwa hewani kwa kupitia KBC. Tunafahamu kuwa wasikilizaji wetu wengi wanapenda tuongeze muda wa matangazo, lakini kutokana na hali halisi ya sasa, hilo si rahisi, labda katika siku za usoni tutajitahidi kufanya hivyo. Vilevile tunatambua kuwa wasikilizaji wetu ni muhimu na tunajitahidi kurahisisha mawasiliano kati yetu. Kwa sasa tunajitahidi kuwatumia bahasha zilizolipiwa gharama za stempu, ili waweze kutuma barua bila malipo utaratibu huo unakubalika kwenye sehemu nyingi nchini Kenya, lakini hata hivyo tunashukuru maoni yake na tutaendelea na juhudi.

Msikilizaji wetu Mtanda Ayub Sharifu ametuletea barua pepe akianza kutoa salamu kwa watangazaji na wasikilizaji wenzake. Anasema kwenye kipindi kilichopita cha Sanduku la Barua kweli aliweza kufuatilia vizuri maelezo ya mama Chen na kwa kinaganaga alihisi kama yeye mwenyewe yuko kwenye studio hapa Beijing. Aliweza kuelewa na kufahamu jinsi mambo yalivyo. Vilevile na barua ambayo amepokea inamthibitishia kuwa Radio China Kimataifa inawajali wasikilizaji wake.

Anasema kuwa amewahi kutoa maoni kuhusu kuwepo kwa kipindi cha maoni ya wasikilizaji. Pia alisema ili kuboresha utoaji wa maoni ya wasikilizaji ni vizuri wasikilizaji wakawa na njia nyingine za kutuma maoni yao mbali na kutumia barua kama ilivyozoeleka. Yeye na wenzake wanapendekeza iwepo njia ya kutuma ujumbe mfupi kwa kutumia simu yaani sms, Barua pepe, na hata kupiga simu moja kwa moja ambapo wasikilizaji wataweza kupata fursa ya kutoa maoni yao bila kukawia. Anasema kipindi kama hiki kinaweza kujulikakana kama Sauti ya wasikilizaji.

Vilevile kutokana na kuwepo kwa kipindi hiki wasikilizaji wanaweza kupewa nafasi ya kutuma salamu au kutoa anuani zao kwa wale wanaohitaji mawasiliano haswa kwa marafiki, jamaa zao na kujuliana hali. Fursa hii itaziwezesha klabu za wasikilizaji kutoka pande zote za dunia kubadilishana maoni jinsi zinavyoendelea. Jambo lingine anasema anapenda walau kuwe na utaratibu waandishi wa CRI kutembelea wasikilizaji hata ni kama mara moja kwa mwaka. Hii itakuwa njia moja ya kuleta ushirikiano na maelewano zaidi na ya kipekee na wasikilizaji kutoka Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo. Kutembeleana kutakuwa na mwendelezo mzuri wa kuhakikisha uhusiano unadumu milele. Kwa mfano yeye amejitolea kutoa shamba na kupanda maua na miti tofauti, ili wasikilizaji wengine waweze kuona mandhari nzuri kama ya Radio China Kimataifa na kula matunda pamoja.

Tunashukuru Bwana Mutanda Ayubu Shariff kwa barua yake na mapendekezo yake, tunaona maoni na mapendekezo yake ni mazuri, lakini katika mazingira ya sasa si rahisi kuyatekeleza. Kwa mfano, kuwapigia simu wasikilizaji wetu huwa ni vigumu, hata kila mara tukitaka kumpigia simu mwandishi wetu wa habari aliyeko Nairobi Kenya, ni vigumu kumpata, hatujui ni kwanini, labda njia ya simu bado haipitiki vizuri. Lakini tuna imani kuwa baada ya kufanya juhudi za pamoja tutajitahidi kuboresha vipindi vyetu. Kama wasikilizaji wetu wanaweza kutuletea barua na kuandika mambo mbalimbali halisi, hayo yatatusaidia kusoma na kuongeza mvuto wa vipindi vyetu.

Msikilizaji wetu Jums Violet wa sanduku la posta 528 Busia Kenya ametuletea barua akisema yeye ni shabiki sugu wa Radio China Kimataifa, ana furaha isiyo ya kifani kutuandikia barua kwa mara nyingine kutoa maoni na mapendekezo yake kuhusu idhaa hii. Kwanza kabisa angependa kutushukuru kwa majibu yetu. Maoni yake ni kama yafuatayo, Radio China Kimataifa imeweza kumpa habari zinazoendelea katika nchi tofauti kupitia kwenye taarifa na maelezo baada ya habari ambapo yeye huelimika na kujua mambo kulingana na wakati. Anasema pia anapenda kipindi cha kuwa nami jifunze kichina, huwa anaburudishwa na jinsi maneno ya Kichina yanavyotamkwa. Vilevile katika vipindi vya burudani, yeye huburudika sawasawa kwani nyimbo zenyewe huimbwa kwa mvuto mkubwa na kwa sauti nzuri kama za ndege.

Anasema angependa kupongeza kipindi hiki na vilevile kutoa maoni kuwa, muda wa kipindi cha salamu zenu uongezwe, pia kama kuna uwezekano kuwe na utaratibu wa wasikilizaji kutuma salamu kwa sauti zao kwa jamaa na marafiki. Na kuhusu kipindi cha kuwa nami jifunze Kichina, angeomba kuwa tunapowaelezea maelezo wasikilizaji wetu tungekuwa na utaratibu wa kuwachagua mashabiki kadhaa ili waweze kuja China na kuzuru nchi hiyo na kuelewa zaidi hali halisi. Mwisho anazidi kushukuru idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, kadhalika kuwapongeza waandaaji wa mpango wa matangazo, na ataendelea kuwa shabiki wetu daima. Ni matumaini yake kuwa tutazidi kumkumbuka na kumjibu, na atafurahi sana kama tutamjibu haraka iwezekanavyo.

Tunamshukuru Bwana Violet kwa barua yake ya kututia moyo, kwani ndiyo kutokana na uhimizaji wa mashabiki wengi kama yeye, tunafanya juhudi za kuchapa kazi kila siku ili tuandae vizuri zaidi matangazo yetu kwa ajili ya wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Karani Mbui wa sanduku la posta 37 Mikinduri Kenya ametuletea barua akianza kwa kutusalimu. Anasema anatuomba tuendelee na moyo wa kutoa habari ili kuwawezesha wasikilizaji wajue mengi kuhusu China, na ulimwengu mzima. Anaomba radhi kwani hakuweza kushiriki kwenye shindano la chemsha bongo kuhusu Mkoa wa Sichuan, maskani ya Panda, kwani alipata barua ya maswali na majibu ikiwa imechelewa. Anatushukuru kwa zawadi tulizomtumia za kalenda na picha ndogo ya ukuta mkuu wa China, hata hivyo angetuomba ikiwezekana tumtumie picha kubwa ya ukuta mkuu.

Mwisho angetaka kusema kuwa hajawahi kutembelea tovuti ya Radio China Kimataifa ya idhaa ya Kiswahili kwenye mtandao wa internet kwani matangazo huwajia wakati wa kazi. Hata hivyo huwa anajaribu kusikiliza Radio China Kimataifa mara kwa mara anapopata nafasi hasa siku za jumamosi na jumapili.

Msikilizaji wetu Felix Barasa Sanduku wa kanisa la Yesu Kenya sanduku la posta 1031 Bungoma Kenya ametuletea barua akianza kwa kutoa salamu kwa watangazaji na wasikilizaji wenzake. Anasema anapenda kutumia nafasi hii kutupongeza sana kwa kazi yetu nzuri ya matangazo ya kipindi cha salamu zenu na vipindi vingine. Anasema yeye husikiliza matangazo ya Radio China Kimataifa kila siku, anafurahia vipindi vyetu na anafurahia matangazo yetu.

Haya basi tunawashukuru wasikilizaji wetu wote popote walipo wanaotufuatilia, ni matumaini yetu kuwa tutadumisha mawasiliano na urafiki kati yetu.

Idhaa ya kiswahili 2007-07-31